1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

20 wauawa katika shambulio dhidi ya uwanja wa ndege Aden

30 Desemba 2020

Mlipuko mkubwa umeutikisa uwanja wa ndege katika mji wa kusini mwa Yemen wa Aden leo Jumatano, muda mfupi baada ya kutua kwa ndege iliyokuwa imewabeba wajumbe wa baraza jipya la mawaziri.

Jemen l Explosion am Flughafen in Aden
Picha: Fawaz Salman/REUTERS

Chanzo cha mlipuko huo bado hakijajulikana na hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio dhidi ya uwanja huo. Picha za video kutoka eneo la tukio ziliwaonesha mawaziri wa serikali wakishuka kwenye ndege wakati mlipuko huo ukitokea, na kufuatiwa na milio ya risasi.

Waziri wa mawasiliano wa YemenNaguib al-Awg, ambaye alikuwa kwenye ndege ya serikali, aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba alisikia milipuko miwili, akiamini lilikuwa shambulio la ndege zisizotumia rubani.

Waziri wa habari Moammar Al-Eryani na waziri mkuu Moeen Abdulmalik Saeed walisema kwamba wajumbe wote wa serikali walikuwa salaama.

Wayemeni wakiwakaribisha wajumbe wa serikali mpya ya umoja katika uwanja wa ndege wa Aden, Desemba 30,2020, kabla ya mlipuko kutikisa uwanja huo.Picha: Saleh Al-OBEIDI/AFP

Saeed alisema katika ujumbe wa twitter kwamba "shambulio hilo la kigaidi lilikuwa sehemu ya vita vilivyoanzishwa dhidi ya Yemen na watu wake," lakini alisita kuwatuhumu waasi wa Kihouthi.

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen, Martin Griffiths, amelaani shambulio hulo alilolitaja kama kitendo cha vurugu kisichokubalika.

Soma pia: Mamia warejea nyumbani katika ubadilishaji wafungwa Yemen

Amesema katika ujumbe wa Twitter kuwa shambulio hilo na ukumbusho juu ya umuhimu wa kuirejesha haraka Yemen kwenye njia ya amani.

Baraza jipya linalenga kuimarisha nguvu dhidi ya Wahuthi

Mawaziri hao walikuwa wanarejea mjini Aden baada ya kuapishwa wiki iliyopita kama sehemu ya mabadiliko kufuatia makubaliano na mahasimu wa serikali wa vuguvugu linalotaka kujitenga.

Serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa imefanya kazi yake kwa sehemu kubwa kutokea uhamishoni katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo vilivyodumu miaka kadhaa.

Vumbi likipanda baada ya mlipuko uwanjani Aden, muda mfupi baada ya kuwaisli kwa ndege iliyokuwa imewabeba wajumbe wa baraza jipya la mawaziri wa serikali ya umoja, Desemba 30,2020.Picha: Al Arabiya/Reuters TV

Rais wa Yemen Abdu Rabbu Mansour Hadi, alieko uhamishoni Saudi Arabia, alitangaza mabadiliko ya baraza la mawaziri mapema mwezi huu, yaliotazamwa kama hatua muhimu katika kuziba mwanya kati ya serikali yake na wapiganaji wa kusini wanaoungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Soma pia: Pande zinazohasimiana Yemen zakutana kwa mazungumzo

Serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabia iko vitani na waasi wa Kihuthi wanaoungwa mkono na Iran, na wanadhibiti sehemu kubwa ya Yemen Kaskazini pamoja na mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW