1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

2014 ulikuwa mwaka mbaya zaidi kwa mauaji ya raia

2 Januari 2015

Umoja wa Mataifa umesema kuwa ghasia zilizotokea nchini Iraq mwaka uliopita wa 2014, zimesababisha vifo vya raia 12,282, na hivyo kuwa mwaka mbaya zaidi wa mauwaji tangu yalipotokea mauwaji mengine mwaka 2006 na 2007.

Mapigano yakiendelea kwenye wilaya ya Mosul
Mapigano yakiendelea kwenye wilaya ya MosulPicha: picture-alliance/E. Yorulmaz /Anadolu Agency

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa karibu vifo 8,500 vimetokea wakati wa nusu ya pili ya mwaka, kutokana na kuongezeka kwa uasi wa wapiganaji wa Kisuni wa kundi lenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu-IS, mwezi Juni nje ya jimbo la Anbar na hivyo kusababisha mapigano kati yake na vikosi vya usalama.

Mkuu wa ujumbe wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Nickolay Mladenov, amesema hata hivyo bado raia wengine wa Iraq wanaendelea kutaabika kutokana na ghasia na ugaidi na kwamba hali hiyo inasikitisha sana.

Kundi la Dola la Kiislamu bado linadhibiti theluthi moja ya sehemu ya Iraq. Jeshi la Iraq likishirikiana na wapiganaji wa Kishia pamoja na vikosi vya Kikurdi vya Peshmerga wanaendeleza mapambano dhidi ya IS.

Umoja wa Mataifa umesema takwimu zinaonyesha kuwa ghasia zimeendelea tangu mwaka 2013 wakati ambapo raia 7,818 waliuawa. Hata hivyo, idadi ya mauwaji ya mwaka 2014 bado ni ya chini ikilinganishwa na ile ya mwaka 2006 na 2007. Umoja huo umesema mwezi Disemba, jumla ya Wairaq 1,101 waliuawa kutokana na ghasia, wakiwemo raia 651, askari polisi 29 na wanajeshi 421 wa vikosi vya usalama.

Mtu mmoja akilikagua gari baada ya bomu kuripuka BaghdadPicha: picture-alliance/dpa/Ali

Maelfu ya wapiganaji wa IS na wa ushirikiano wa vikosi vya serikali wauawa

Maelfu ya wanajeshi wa serikali ya Iraq, wapiganaji wa IS, vikosi vya kikabila na wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga, wameuawa katika mapambano kati yao. Umwagikaji damu ulikuwa mbaya zaidi mwezi Disemba kwenye mji mkuu wa Iraq, Baghdad, ambako raia 320 waliuawa, ukifatiwa na jimbo la Anbar ambako raia 164 waliuawa.

Wakati huo huo, watu 20 wakiwemo watoto wameuawa baada ya kombora kupiga kwenye nyumba za mji wa Fallujah uliopo magharibi mwa Iraq. Shirika huru la habari la Iraq, Alsumaria limesema hospitali kuu ya Fallujah leo imepokea maiti 20 za wakaazi wa mji huo. Watu wengine 30 wamejeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea kwenye mji muhimu wa jimbo la Anbar

Ama kwa upande mwingine watu wenye silaha wamewaua viongozi watatu wa kidini wa madhehebu ya Sunni kwenye jimbo la kusini la Basra lenye wakaazi wengi wa madhehebu ya Kishia.

Viongozi wengine wawili wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iraq, Mohammed Ghabban ameamuru uchunguzi wa shambulio hilo ufanyike. Taarifa ya wizara hiyo imewalaumu wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu kwa kuhusika na mauwaji hayo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,DPAE,AFPE
Mhariri:Gakuba Daniel

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi