1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

2023 ni mwaka wa changamoto kwa walinda amani wa UN Afrika

27 Desemba 2023

Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vimepata mafanikio madogo mwaka 2023. Nchini DR Congo, walipambana na raia na kulazimika kuondoka huko. Na pia hiyo sio nchi pekee ya Kiafrika wanayoondoka.

Jahmhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | Picha ya ukutani Goma
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa haujafanikiwa kurejesha amani Mashariki wa DR Kongo.Picha: Pablo Porciuncula/AFP/Getty Images

Jumbe za kulinda amani za Umoja wa Mataifa zimepambana mwaka 2023 kuwalinda raia na kuleta utulivu katika nchi wanazoendesha shughuli zao hasa barani Afrika.

Katika nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Sudan Kusini, Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wamepata mafanikio madogo.

Kulingana na baadhi ya wachambuzi, vikosi vya Umoja wa Mataifa vinavyofanya kazi chini ya miongozo mikali vimeelemewa katika baadhi ya nchi hizo.

"Kisa cha wazi ni Mali,  ambako hali ya usalama haijatengama kwa sababu siku baada ya siku ghasia zinaonekana kuwa mbaya zaidi," Adib Saani, mkurugenzi wa Kituo cha Usalama wa Binadamu na Ujenzi wa Amani cha Jatikay, aliiambia DW. "Inaonekana kana kwamba ujumbe wa UN hauna msaada."

Kwa wachambuzi kama Saani, utendaji duni wa hivi karibuni wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika baadhi ya maeneo ya Afrika unakatisha tamaa.

Wachambuzi wanasema Afrika bado inawahitaji walinda amani wa Umoja wa Mataifa.Picha: Ishara S. Kodikara/AFP/Getty Images

"Wameshindwa mara kwa mara kukabiliana na mzunguko wa vurugu katika nchi hizo na sababu yenyewe ya kuletwa hapo awali," Saani alisema.

Vikwazo vya mamlaka kwa walinda amani wa UN

Jumbe za Umoja wa Mataifa zina mamlaka ya wazi ya utendaji ambayo yanazuia shughuli zao. Kwa mfano, operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa hazizingatiwi kuwa zana za utekelezaji.

Soma pia: Sudan yataka ujumbe wa kulinda amani UNITAMS uondolewe mara moja

Hawaruhusiwi kutumia nguvu ya kuua isipokuwa katika kujilinda au kutetea mamlaka waliyopewa. Baadhi ya wataalam wanalaumu mamlaka "dhaifu" kwa matatizo ya ulinzi wa amani.

"Siwezi kusema kwamba jumbe zoze za Umoja wa Mataifa barani Afrika zinashindwa, lakini ni muundo wa mamlaka yao ambao unazuia ufanisi au ufanisi wao katika maeneo ambako zinakusudiwa kufanya kazi," Fidel Amakye Owusu, mtaalamu wa utatuzi wa migogoro aliiambia DW.

Alisisitiza kuwa kikomo cha utendakazi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wakati mwingine huwaweka katika hali mbaya ambapo wananchi wanaziona kuwa hazina tija katika kuleta utulivu katika hali tete.

Nchini Mali, raia waliupinga ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (MINUSMA) mwaka huu, na mwezi Juni, serikali inayoongozwa na jeshi ilitaka kujiondoa kwa ujumbe huo, takwa ambalo lilikubaliwa. 

Ujumbe huo ulitumwa muongo mmoja uliopita ili kuzima uasi wa wanaotaka kujitenga na wapiganaji wa Kiislamu kaskazini mwa Mali, lakini serikali ya kijeshi ilivishutumu vikosi hivyo kwa kuzidisha hali ya wasiwasi.

Mwezi Oktoba, Umoja wa Mataifa ulisema ujumbe huo ulikuwa mbioni kuondoka katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufikia Desemba 31 na "umejitolea kikamilifu kuheshimu muda huu."

Wanajeshi wa mwisho wa jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, waliotumwa Mali kama sehemu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, MINUSMA, tayari wameondoka. Waliondoka Mali mwezi huu.

Wakaazi Kivu washinikiza kuondolewa MONUSCO DRC

02:15

This browser does not support the video element.

Soma pia: Kikosi cha UN Mali chaondoka mapema kutokana na ukosefu wa usalama

Ujerumani ilituma jumla ya wanajeshi 20,000 katika kipindi cha ujumbe wa kulinda amani - wakiwakilisha idadi ya pili kwa ukubwa ya wanajeshi wa kigeni wa Bundeswehr nyuma ya Marekani katika uvamizi wa Afghanistan.

Serikali za kulaumiwa kwa utendaji mbaya wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa

Owusu alisema serikali, kama ile ya Mali, pia ndizo za kulaumiwa kwa kuhatarisha utendakazi wa jumbe za amani.

"Kwa upande wa Mali, ungetambua kwamba katika siku za hivi karibuni, kwa sababu ya kuingia kwa Wagner, ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ujumla ulikuwa na kikomo kuhusu kile ambacho ungeweza kufanya."

Kundi la Wagner, ambalo ni kampuni ya kijeshi ya kibinafsi ambayo mara nyingi huelezewa kama kikosi cha mamluki cha Urusi, linapendelewa na watawala wa kijeshi wa Mali kuwasaidia kukabiliana na vitisho vya jihadi huko.

Hali za migogoro barani Afrika hubadilika na hazitabiriki, na kulingana na Owusu, muundo wa mamlaka ya Umoja wa Mataifa unafanya kuwa vigumu sana kuitikia katika hali tete.

Utawala wa kijeshi wa Mali uliamuru vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa kuondoka ncini humo mwezi Juni.Picha: SOULEYMANE AG ANARA/AFP/Getty Images

"Kwa hivyo mara nyingi, inaonekana kana kwamba hawafanyi wawezavyo," Owusu alisema. "Hata hivyo, inahusiana na mipaka ya mamlaka yao kuliko namna vikosi vilivyo na ufanisi au ujumbe wenyewe."

Ujumbe wa kulinda amani wa UN bado unahitajika Afrika

Hata hivyo, Owusu alionya dhidi ya kuvifanya vikosi vya Umoja wa Mataifa kuwa visivyotakiwa na kuvitaka viondoka kama zilivyofanya Mali na Kongo, akisema inaweza kuwa isiyo na tija.

Kwa upande wa Mali na eneo la Sahel, "bado tunapata ongezeko la matukio ya ugaidi," Owusu alisema. Wanachama wa kundi la itikadi kali, "Dola la Kiislamu," bado wako karibu na, anasema, "wana ujasiri na kuteka maeneo kila siku, kila wiki."

Soma pia: Mali kusitisha mizunguko ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa MINUSMA

Jumbe za Umoja wa Mataifa zinakabiliwa na shinikizo, na umuhimu wake unatiliwa shaka, lakini kulingana na Mohamed Amara kutoka Chuo Kikuu cha Barua na Sayansi ya Binadamu mjini Bamako, jukumu lao bado ni muhimu.

Aliiambia DW kuwa ana wasiwasi, kwa mfano, kwamba mara baada ya ujumbe kushindwa na kuondoka, serikali zinaweza kuhangaika kuziba pengo lililoachwa nyuma na kuondolewa kwa vikosi vya kulinda amani.

"Ni muhimu kusisitiza kwamba MINUSMA, mahali fulani, inafanya kazi kama kizuizi kati ya mamlaka ya Mali na maeneo mengine. Ikiwa MINUSMA itaondoka, itakuwa muhimu kujaza nafasi hizi zote za usalama zinazokaliwa na MINUSMA," Amara aliongeza.

Kushawishi nyoyo na akili za wenyeji

Lakini walinda amani pia hawajafanya vya kutosha ili kupata imani ya nchi wenyeji wao. Baadhi yao wameshutumiwa kwa unyonyaji na unyanyasaji wa kingono.

Umoja wa Mataifa ulikirudisha nyumbani kikosi cha wanajeshi 60 wa kulinda amani kutoka Tanzania kwa madai ya utumikishaji na unyanyasaji wa kingono katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka huu.

Saani alisema madai kama hayo ya unyanyasaji yanapokosa kuchunguzwa na wahusika kutoadhibiwa haraka, inatatiza kazi ya ujumbe.

Soma pia:Ujumbe wa UNAMID wapendekezwa kuondolewa Darfur 

"Kwa mfano, katika mkoa wa Darfur kulikuwa na baadhi ya madai ya unyonyaji na walinda amani, ambayo lazima niseme ilivuruga ujumbe wa kulinda amani katika eneo hilo katika sifa mbaya," alisema.

"Kwa mfano, katika mkoa wa Darfur kulikuwa na baadhi ya madai ya unyonyaji na walinda amani, ambayo lazima niseme yaliuingiza ujumbe wa kulinda amani katika eneo hilo katika sifa mbaya," alisema.

Makabiliano kati ya walinda amani na raia mjini Goma yalisababisha maafa mwaka huu.Picha: Stringer/AA/picture alliance

"Kwa hiyo uaminifu ni, lazima niseme, ni tatizo. Na kuna mtazamo mwingine kwa hilo. Wengine wanahisi kwamba ni njama ya madola ya Magharibi kuresha tena, kama naweza kusema, mamlaka na udhibiti wao juu ya mataifa ambako walinda amani hawa wanafanya kazi."

Wasiwasi mwingine ni kukosekana kwa utulivu wa kisiasa katika baadhi ya nchi ambako jumbe hizo zinafanya kazi. Kulingana na Saani, hakuna jipya litakalopatikana ikiwa kuna ukosefu wa mifumo madhubuti ya kidemokrasia.

Mageuzi UN yanahitajika

"Sababu mojawapo ni kukosekana kwa utulivu wa kisiasa. Unaweza kufanikiwa tu ikiwa kuna dhamira thabiti ya kisiasa. Ikiwa hakuna dhamira hiyo, inakuwa ngumu sana kwao," Saani alisema.

Owusu anahimiza mageuzi katika utendaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa ikiwa wanataka watafanikiwe katika miaka ijayo barani Afrika.

Soma pia:Wanajeshi wa Monusco kuondoka Kongo ifikapo Disemba 

"Pengine jumbe za Umoja wa Mataifa kwenda mbele lazima zifafanuliwe upya, labda kwa kupanua mamlaka yao au kuzifanya kuwa wazi zaidi," Owusu alisema.

Saani anakubali, akisisitiza kuwa kazi ya jumbe za Umoja wa Mataifa bado ni muhimu barani Afrika.

"Siwezi kukataa ukweli kwamba Afrika haiwezi kufanya hivyo peke yake. Hatujitegemei. Hata hivyo, nafikiri kinachopaswa kutokea ni kwa Umoja wa Mataifa kujipanga upya," Saani alisema.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW