26 wauwawa katika shambulio la bomu katika hoteli Somalia
13 Julai 2019Afisa wa ngazi ya juu wa kimkoa amesema leo Jumamosi (13.07.2019) kuwa mshambuliaji wa kujitoa muhanga aliigonga gari iliyokuwa na miripuko katika hoteli ya Medina katika mji wa bandari wa Kismayo jana Ijumaa kabla ya watu kadhaa wenye silaha nzito kulazimisha kuingia ndani ya hoteli hiyo, wakifyatua risasi wakati wakiingia ndani.
Mzingiro huo ulidumu kwa takriban masaa 12 na ulimalizika tu alfajiri ya Jumamosi baada ya mapambano na majeshi ya usalama.
Wakenya watatu, Watanzania watatu, Wamarekani wawili, Muingereza mmoja na raia mmoja wa Canada ni miongoni mwa watu 26 waliouwawa katika shambulio hilo, rais Ahmed Mohamed Islam wa jimbo lenye mamlaka yake ya ndani katika jimbo la Jubaland amewaambia waandishi habaei.
"Kuna pia raia wawili wa China waliojeruhiwa," ameongeza.
Shirika la habari la AFP limethibitisha pamoja na wana familia kuwa kiasi ya watu wanne waliofariki wana uraia pacha.
"Majeshi ya usalama yana udhibiti hivi sasa na gaidi wa mwisho alipigwa risasi na kufariki", Mohamed Abdiweli, afisa wa usalama alisema.
Hoteli yavamiwa
"Kuna miili ya watu waliofariki na ile ya waliojeruhiwa ikiwa imezagaa ndani ya hoteli hiyo," Abdiweli alisema.
Amesema maafisa wanaamini watu wanne waliokuwa na silaha, ambao mtu mmoja aliyeshuhudia aliwaeleza kuwa walivalia sare za jeshi la polisi la Somalia, walihusika katika shambulio hilo.
Shabaab , kundi lenye mafungamano na kundi la al-Qaeda , limedai kuhusika na mzingiro huo na kuueleza kuwa ni "shambulio la mashahidi".
"Kuna mtafaruku ndani , niliona miili kadhaa ya watu waliofariki ikichukuliwa kutoka katika eneo la tukio na watu wanakimbia kutoka katika majengo ya karibu," Hussein Muktar aliyeshuhudia alisema wakati wa shambulio hilo.
"Mripuko ulikuwa mkubwa sana," aliongeza.
Shambulio hilo ni la hivi karibuni kabisa katika mlolongo mrefu wa mashambulio ya mabomu na mapambano ya bunduki yanayodaiwa kufanywa na al-Shabaab.
Watu walioshuhudia wamesema miongoni mwa waliouwawa ni mwanaharakati maarufu katika mitandao ya kijamii na mwandishi habari wa Somalia.
Mwandishi na mwanaharakati wauwawa
"Ndugu wa mwandishi habari Mohamed Sahal wamethibitisha kifo chake na naelezwa kuwa mwanaharakati katika mitandao ya kijamii Hodan Naleyeh na mume wake pia wamefariki katika mripuko huo, mtu aliyeshuhudia Ahmed Farhan amesema.
Chama cha waandishi habari nchini Somalia SJS kimethibitisha madai ya kifo cha mwandishi huyo. Ni siku ya masikitiko makubwa kwa waandishi habari wa Somalia," katibu mkuu wa chama hicho Ahmed Mumin amesema katika taarifa.
Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa, wengi wa wale wanaoishi katika hoteli hiyo walikuwa ni wanasiasa na wafanyabiashara kabla ya uchaguzi ujao wa kimkoa.
"Jengo lote limekuwa gofu, kuna miili ya watu waliokufa na waliojeruhiwa ambao wametolewa kutoka ndani. Majeshi ya usalama yamezuwia eneo lote," amesema mtu mmoja aliyeshuhudia Muna Abdirahman.
Wapiganaji wa al-Shabaab wamepigana kwa zaidi ya muongo mmoja kuiangusha serikali ya Somalia. Kundi hilo la wanamgambo lilitokana na mahakama za Kiislamu ambao walikuwa wakati fulani wakidhibiti eneo la kati na kusini mwa Somalia na wanakadiriwa kufikia wapiganaji kati ya 5,000 na 9,000.
Mwaka 2010 kundi la al-Shabaab lilitangaza utiifu wao kwa al-Qaeda.
Katika mwaka 2011 , walikimbia maeneo yao ambayo waliwahi kuyashikilia mjini Mogadishu, na tangu wakati huo wamepoteza maeneo yao mengi. Lakini wanaendelea kudhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya vijijini nchini humo na wanaendelea kupambana katika vita vya chini kwa chini dhidi ya serikali.