40 wauwawa Syria
26 Oktoba 2013Mamia ya watu wamejeruhiwa katika shambulio la bomu lililotegwa katika gari katika mji wa Suq Wadi Barada, shirika lenye makao yake makuu nchini Uingereza la kuangalia haki za binadamu nchini Syria limesema, na ambalo linategemea mtandao wa wanaharakati na watu wengine ambao wameshuhudia matukio.
Serikali ya Syria na upinzani wamelaumiana kutokana na mauaji hayo. Suq Wadi Barada ni mji ambao unadhibitiwa na waasi na umezingirwa na majeshi tiifu ya utawala wa rais Bashar al-Assad.
"Idadi ya watu waliouwawa kutokana na shambulio la bomu lililotegwa katika gari ambalo liliripuka baada ya sala ya Ijumaa katika mji wa Suq Wadi Barada imepanda hadi watu 40, ikiwa ni pamoja na watoto na wanawake," limesema shirika hilo la uchunguzi wa haki za binadamu.
"Idadi ya waliofariki huenda ikapanda kwasababu kuna watu kadha ambao wamejeruhiwa, wengi wao wako katika hali mbaya sana,"Limeongeza.
Magaidi wanahusika
Shirika la habari la Syria SANA , hapo kabla liliripoti kuhusu mripuko huo, na kulaumu kile lilichokiita kuwa ni "magaidi", neno linalotumiwa na utawala wa Assad kuwaelezea wapiganaji wanaojaribu kuuondoa utawala wake. Shirika la habari la SANA limesema "gari hiyo iliripuka wakati magaidi wakiwa wanaweka miripuko ndani ya gari hiyo ".
Kundi la muungano wa kitaifa wa upinzani wakati huo huo limeilaumu serikali ya Assad kwa mauaji yaliyosababishwa na kile ilichosema kuwa ni miripuko miwili ya mabomu yaliyotegwa katika magari yaliyowekwa nje ya msikiti wa Osama bin Zeid mjini Suq Wadi Barada. Mashambulio ya mabomu yaliyotegwa katika magari yamekuwa yakitokea mara kwa mara nchini Syria katika miezi ya hivi karibuni, na kuuwa watu kadha nchini humo.
Televisheni ya Syria wakati huo huo imeripoti kuwa Abu Mohammed al-Jawlani , kiongozi wa kundi la al-Nusra Front , kundi la waasi lenye nguvu la Waislamu wanaofuata nadharia za jihad ambalo linamahusiano na al-Qaeda, ameuwawa kaskazini magharibi ya jimbo la Latakia, lakini kundi hilo baadaye limesema yuko katika hali nzuri.
Ghasia zaongezeka
Katika tukio jingine la ghasia shambulio la kushtukiza mashariki ya Damascus limewauwa waasi 24, limesema shirika hilo la kuangalia haki za binadamu nchini Syria , wakati shirika la habari la SANA limesema idadi ya waasi waliouwawa ni 40.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa na wa Marekani wameeleza wasi wasi wao kuhusiana na eneo la Ghouta ya mashariki pamoja na maeneo mengine ya vitongoji vya mji mkuu Damascus ambavyo vimezingirwa, kufuatia ripoti kuwa kuna uhaba mkubwa wa chakula na kiwango ambacho kinaongezeka cha utapia mlo.
Mkuu wa idara ya Umoja wa Mataifa inayotoa misaada ya kiutu Valerie Amos siku ya Ijumaa (25.10.2013) amelitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuweka mbinyo dhidi ya serikali ya Syria kuruhusu misaada kuingia katika eneo hilo ambalo lina wakaazi raia milioni 2.5 ambao wamekwama kutokana na mzozo huo.
Amos ameliambia baraza hilo lenye wanachama 15 kuwa "maneno , bila ya kuwa na uwezo wa kutoa msukumo, hayawezi kutengeneza picha ya madhila na mateso yanayotokea nchini Syria.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga