Abdullah Gül ni rais mpya wa Uturuki. Amefikia lengo lake.
29 Agosti 2007Hayo ni maneno ya Abdullah Gül punde alipochaguliwa wiki hii na bunge la Uturuki kuwa rais wa nchi hiyo.Lilikuwa jaribio lake la tano kutaka kukamata wadhifa huo, baada ya majaribio mawili yasiofaulu mwanzoni mwa mwaka huu. Jumanne wiki hii alipata kura 336 za wabunge, zaidi kabisa ya zile 276 wa wingi unaohitajiwa.
Jeshi la Uturuki lilitishia kwamba litafanya mapinduzi pindi Abdullah Gül atachaguliwa kuwa rais, upande wa upinzani ulichora picha ya kutisha kwamba Uturuki itarejea nyuma kama ilivokuwa katika karne ya 19, enzi za Khlaifa na kuwa na utawala wa sheria za Kiislamu. Lakini mara hii wapinzani wa Abdullah Gül hawajaweza kuzuwia kuchaguliwa kwake. Pale katika uchaguzi wa bunge wa July 22 mwaka huu asilimia 47 ya wapiga kura walipokichagua Chama tawala cha AKP cha Abdullah Gül na waziri mkuu Tayyip Erdogan, kura hizo, bila ya shaka, ziliashiria kwamba wananchi wanamtaka Gül, aliyekuwa watziri wa mambo ya kigeni wakati huo, awe rais wao.
Kuchaguliwa kwa mtu huyo anayetajwa kuwa ni mcha-mungu, kunafanya sasa chama tawala cha AKP kiloo na mizizi ya siasa za Kiislamu kukamata nyadhifa tatu muhimu katika dola, urais wa nchi, spika wa bunge na waziri mkuu.
Kiongozi wa upinzani wa Uturuki, Deniz Baykal, ameweka wazi kwamba kuchaguliwa aliyekuwa waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo, Abdullah Gül, kuwa rais wa nchi hiyo ni hatua ya kwanza ya kuibadilisha nchi hiyo kuwa na serekali inayoambatana na mafunzo ya dini ya Kiislamu. Kwa Deniz Baykal, mtu ambaye mawazo yake yamejikita katika mawazo ya muasisi wa dola ya kisasa ya Uturuki, Kemal Atatürk, aliyetaka dola isifungamane na dini, Abdullah Gül ni kinyonga ambaye atadhihirisha uso wake halisi wa siasa kali za kidini punde atakapoingia katika Ikulu ya rais mjini Ankara. Lakini, kwa wafuasi wake na Waturuki wengi, Abdullah Gül ni mwanadimokrasia na mwanamageuzi, kwa maslahi ya nchi yake.
Sasa amekuwa ni mwanasiasa anayependwa sana. Tangu chama chake cha AKP kiingie serekalini Novemba 2002. Abdullah Gül, mwenye umri sasa wa miaka 56, amekuwa mbele katika kuibadilisha Uturuki kuwa nchi inayokaribiana sana na misingi ya kidola inayoheshimiwa na nchi nyingi za Ulaya.
Mwanamke mmoja mjini Istanbul anasema:
+Mtu lazima ampime Abdullah Gül kutokana na yale alioyafanya hadi sasa. Amefanikiwa kama waziri wa mambo ya kigeni, hasa kuiambatanisha Uturuki na Umoja wa Ulaya. Namna anavotenda inanifanya nimuamini kuwa yeye ni mwanasiasa mwenye nia safi, na sio mbwa mwitu aliyevaa ngozi ya kondoo.+
Mbunge wa Ulaya kutoka Ujerumani, mwenye asili ya Kituruki, Cem Özdemir, anakubaliana na tathmini hiyo:
+Kwa wanasiasa wa Ulaya, kama vile kamishina wa Ulaya anayeshughulikia kuupanua Umoja wa Ulaya, Olli Rehn, waziri wa mambo ya kigeni, Frank-Walter Steinmeier, au mtangulizi wake, Joschka Fischer, Abdullah Gül anaheshimika na anasifiwa. Anaonekana kuwa ni mshirika wa kuaminika, mtu ambaye unaweza kufikia makubaliano, na akatimiza ahadi. Mtu anaweza kusema kwamba Gül anaaminika zaidi nchi za nje kuliko nchini mwake kwenyewe.+
Na huu mtindo wake wa kuchanganyisha siasa ya kuutambua ukweli halisi wa mambo- kama vile kutaka Uturuki ijiunge na Umoja wa Ulaya kwa haraka kama inavowezekana- na utambulisho wake wa kibinafasi wa ucha mungu umewafanya watu kama Deniz Bakal kuwa na hofu na mwanasiasa huyu.
Abdullah Gül alisomea uchumi katika chuo kikuu cha Istanbul na pia huko Uengereza, baadae akasomesha katika chuo kikuu nchini mwake. Na tangu mapema udugoni, baba yake alimsomesha Quran na kumpa mwamko wa kisiasa.
Ni katika mji alikozaliwa wa viwanda wa Kayseri ndiko alipojuana na mke wake, Hayrünnisa, wakati huo akiwa na umri wa miaka 14, na katika mji huo ndipo alipopigania kwa mara ya kwanza ubunge mwaka 1991. Mwenyewe ana fahari na watu wa mji huo, akisema: Watu wa Kayseri sio wenye kuota, ni watu wenye kuujuwa ukweli wa hali ya mambo, na huo ndio aina ya Uislamu wanaoutaka.
Wapinzani wake wanamkumbusha juu ya matamshi aliyoyatoa katika miaka ya tisini aliposema: Mtindo wa dola kutoelemea dini umekwisha. Sasa yeye anabisha kusema hayo, wapinzani wake wanasema miaka kumi iliopita alisema vingine na vile anavosema sasa.
Alipotangaza kwamba anataka kupigania urais, alisema:
+Pale bunge litakaponichagua kwa wadhifa huu wenye heshima, zitoelemea chama chochote cha kisiasa, na, nikifuata mwangaza wa katiba yetu, nitawatendewa usawa raia wote.+
Baada ya kupinduliwa serekali ya Erbakan na wanajeshi mwaka 1997, Abdullah Gül amebadilisha mawazo yake. Pamoja na wenzake walimfuata aliyekuwa meya mkuu wa jiji la Istanbul, Recep Tayyip Erdogan, ambaye alihisi kwamba ajenda ya siasa kali za Kiislamu haiwezi kuungwa mkono na wingi wa watu katika Uturuki. Hivyo mwaka 2001 wakaunda chama cha Haki na Maendeleo, AKP, kikiitambua misingi ya kidemokrasia na kutaka mabadiliko, lakini bado kikibakia na mizizi yake ya Kiislamu. Chama cha AKP kilijiona kama vile chama cha Christian Democratic, CDU, cha hapa Ujerumani.
Matokeo yalikuwa ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa bunge mwaka 2002. na ilivokuwa Tayyip Erdogan wakati huo bado alipigwa marufuku kufanya shughuli za kisiasa, nafasi ya waziri mkuu ilichukuliwa na Abdullah Gül. Baada ya miezi mitano alimwachia Erdogan achukuwe nafasi hiyo. Lakini licha ya utiifu wake, isichukuliwe kwamba Abdullah Gül atamfuata Erdogan kama kipofu. Kama rais, atabakia na mwazo yake ya Ki-Conservative na ya ucha mungu, na huenda akataka amri ya kupiga marufuku kuvaa mitandio katika Ikulu ya Rais iondoshwe, lakini itabidi aangalie kwamba yeye sio mwakilishi wa sehemu ya kidini ya jamii ya Kituruki. Asipotahadhari huenda kukatokea mikwaruzano na marafiki zake wa zamani katika serekali ya Chama cha AKP.
Mbunge wa Ujerumani katika Bunge la Ulaya, Cem Özdemir, mwenye asili ya Kituruki, anautathmini utawala wa Chama cha AKP ambapo Abdullah alikuwa waziri muhimu:
+Mtu lazima atilie maanani miaka mine na nusu iliopita ya siasa ya serekali ya AKP. Haijachangia katika kuifanya jamii ya Kituruki iwe yenye siasa kali. Kinyume na hivyo. Jamii ya Kituruki imejifungua zaidfi kuliko wakati wowte katika historia. Kumefanyika marekebisho mengi, katika upande wa demokrasia na haki za binadamu. Kwamba Abdullah Gül haaminiwi, ni kitu kinachojulikana, na sasa ni juu yake kuiondosha hioyo hali ya kutoaminiwa.+
Baada ya kuhamia katika Ikulu, familia ya Abdullah Gül itakuwa machoni mwa watu. Mke wa Gul, Hayrünnisa, mwenye umri wa miaka 42, aliye mcha mungu, ataendelea kuvaa mtandio. Yeye anasema mtandio anaouvaa, jambo ambalo linapingwa na wapinzani wa Abdullah Gul, ni chaguo lake la kibinafsi linalofaa kuheshimiwa. Kila wakati anasema mtandio wake unafunika kichwa chake , lakini sio ubongo wake. Binti yake, Kübra, mwenye umri wa miaka 21, karibuni, bila ya kujali amri ya kukataza kuvaaa mitandio katika majengo ya chuo kikuu, aliingia kwenye ukumbi wa kufanyia mitihani huku akivaa mtandio.
Imetajwa kwamba Kübra anataka kuolewa na mchumba wake , Mehmet Sarimermer, mwezi ujao wa Septemba, na atafanya hivyo akivaa mtandio, na tena huko kwenye Ikulu mjini Ankara.
Lakini tusikubali kuyaingiza maneno katika mdomo wa Abdullah Gül. Hebu tumsikie mwenyewe:
+Katiba itakuwa dira yangu. Jamhuri ya Uturuki ni nchi ya kidemokrasi, isioelemea katika dini, yenye kueshimua hakli za kijamii na utawala wa sheria. Kuyalinda na kuyaendeleza mambo hayo ndio litakuwa jukumu langu. Hasa kulinda dola isielemee dini ndio msingi wangu, kwa hivyo hana haja mtu yeyote kuwa na wasiwasi.+