1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshambuliaji azidiwa nguvu na wanajeshi wa Marekani

22 Agosti 2015

Mtu aliekuwa na silaha aliwajeruhi abiria watatu ndani ya treni iliyokuwa inatoka mji wa Amsterdam kwenda Paris. Lakini mtu huyo alizidiwa nguvu na abiria wengine miongoni mwao wanajeshi wawili wa Marekani.

Maafisa wa Ufaransa baada ya abiria wa treni kushambuliwa
Maafisa wa Ufaransa baada ya abiria wa treni kushambuliwaPicha: picture-alliance/dpa/P. Bonniere

Milio ya risasi ilisikika ndani ya treni ya mwendo wa kasi na abiria mmoja alijeruhiwa, katika shambulio lililofanywa na mtu mmoja ambae baadae alizidiwa nguvu na abiria wengine.

Kampuni ya reli ya Ufaransa imesema shambulio hilo lingeliweza kusababisha maafa makubwa zaidi laiti, mshambuliaji huyo asingelizidiwa nguvu na watu wengine.

Mshambuliaji huyo alizuiwa na abiria kadhaa miongoni mwao wanajeshi wawili wa Marekani waliokuwamo ndani ya treni iliyokuwa inatoka mji wa Amsterdam nchini Uholanzi kwenda Paris,Ufaransa.

Rais Obama atoa pongezi:

Rais wa Marekani Barack Obama amewapongeza wanajeshi hao wa Marekani kwa ushujaa wao na amesema kama wanajeshi hao na watu wengine walioingilia kati, maafa yangelikuwa makubwa zaidi ndani ya treni hiyo. Rais Obama amewashukuru wanajeshi wake kwa ujasiri wao, na hatua ya haraka waliyoichukua katika kumzidi nguvu mshambuliaji ambae vinginevyo angelisababisha maafa makubwa zaidi.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Bernard Cazeneuve pia amesema bila ya wamarekani hao mambo yangelikuwa mabaya zaidi.Hata hivyo mmoja wa Wamarekani hao alikuwa miongoni mwa watu waliojeruhiwa vibaya na mwengine anaetibiwa amejeruhiwa kidogo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Bernard CazeneuvePicha: Reuters/B. Tessier

Treni hiyo ilisimama ili kuwateremsha abiria katika mji wa Arras kaskazini mwa Ufaransa baada ya shambulio kutokea saa 12 za jioni.

Vyombo vya habari vya mji huo vimeripoti kwamba mshambuliaji ambae mpaka sasa hajatambulika, alikuwa na visu na bunduki, ikiwa pamoja na bunduki kama ya Kalanishnikov. Wachunguzi kutoka kitengo maalumu cha Ufaransa cha kupambana na ugaidi wanaongoza uchunguzi.

Mshambuliaji anatuhumiwa kutoka Morocco:

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa polisi Sliman Hamzi, mshambuliaji ni mtu mwenye umri wa miaka 26 na anatoka Morocco.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ni mapema mno kuzungumzia juu ya ugaidi. Msemaji huyo ameeleza kuwa sababu iliyomfanya mtuhumiwa awashambulie watu wengine haijajulikana. Lakini mtu huyo amewekwa ndani kwenye kituo cha polisi.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema kila linalopasa linafanywa ili kutoa habari zote juu ya kadhia hiyo. Maafisa wa Ufaransa wamethibitisha kwamba Mmarekani na Mwingereza mmoja ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa.

Na shirika la habari la AFP limefahamisha kuwa mwigizaji wa sinema wa Ufaransa Jean-Hugues Anglade pia alijeruhiwa kidogo. Mwigizaji huyo alijikata na kipande cha kioo kilichovunjika, alipokuwa anajaribu kupiga kengele ya kuashiria hatari.

Wafaransa na Wabelgiji watafanya uchunguzi wa pamoja:

Ofisi ya Rais nchini Ufaransa imesema shambulio lilifanyika wakati treni ilipokuwa inapita Ubelgiji.Rais wa Ufaransa Hollande amesema amewasiliana na Waziri Mkuu wa Ubelgiji Charles Michel na viongozi hao wameahidi kushirikiana kwa undani katika kufanya uchunguzi.

Nchini Ufaransa polisi wamewekwa katika hali ya tahadhari tangu kutokea mashambulio yaliyofanywa na waislamu wenye itikadi kali waliowaua watu 20 mnamo mwezi wa Januari.

Mwandishi: Abdu Mtullya/afp,dpa,
Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW