1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Abiy atangaza uwezekano wa mazungumzo na waasi wa Oromo

29 Machi 2023

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema serikali yake, inajaribu kuandaa mazungumzo na kundi la waasi la jeshi la ukombozi la Oromo, linalofanya operesheni zake katika jimbo linalokumbwa na machafuko la Oromia.

Äthiopien ehrt seine Polizeikräfte
Picha: Michael Tewelde/XinHua/dpa/picture alliance

Matamshi ya Abiy Ahmed kwa wabunge kuhusu hatua hiyo ya kufanya mazungumzo na kundi la Oromo, yamekuja kufuatia juhudi za kuyafuata yale yaliyoafikiwa katika makubaliano ya amani katika jimbo lililokumbwa na mzozo la Tigray, yaliyosababisha kutiwa saini makubaliano hayo mwezi Novemba na kusitisha mapigano kaskazini mwa nchi hiyo.

Ethiopia yamteua afisa wa TPLF kuongoza Tigray

Waziri Mkuu huyo wa Ethiopia amesema serikali ina nia ya kweli ya kutatua kwa amani mgogoro kati yake na kundi la waasi la Jeshi la Ukombozi la Oromo. Amesema tayari kumeundwa kamati iliyopewa jukumu la kuongoza mchakato huo akitumai kuwa raia wa Ethiopia wataunga mkono hatua hiyo.

Abiy ameongeza kuwa wamejaribu kulifikia kundi hilo mara kumi ili kuwasogeza ndani ya mchakato huo, lakini tatizo lililopo ni kwamba, kuna makundi mengi na kila kundi lina maono na misimamo tofauti. Hata hivyo, ameonesha matumaini kwamba kamati iliyoteuliwa itaongoza mazungumzo hayo na matokeo yatajulikana baadaye.

Msemaji wa Oromo asema matamshi ya Abiy yamepitwa na wakati

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Picha: Ethiopian Prime Minister Office

Hata hivyo, msemaji wa waasi wa Oromo, Odaa Tarbii, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba, matamshi ya waziri mkuu huyo yamepitwa na wakati na hayaendani na hali halisi ilivyo kwa sasa.

Tarbii ameijibu kauli ya Abiy akisema kwamba hatua ya kujaribu kuufikia uongozi wao haikuwa ya kweli. Amesema baadaye serikali ya shirikisho ya Ethiopia iliunda kamati kadhaa zilizokuwa na wapatanishi wa ndani waliopewa jukumu la kuwasiliana na maafisa kadhaa wa kundi hilo kujaribu kuwashawishi kujisalimisha.

Msemaji huyo amesema wako tayari kwa mazungumzo lakini wameweka wazi kwamba lazima kupatikane mpatanishi wa tatu wa kimataifa ili kuhakikisha ufanisi wa makubaliano yoyote yatakayofikiwa. Amesema kuna kila ishara ya kuonesha kwamba mazungumzo baina ya pande hizo mbili yatafanikiwa.

Waasi wa Oromo washutumiwa kufanya mauaji ya wengi

Picha: Maria Gerth-Niculescu/DW

Kundi la Oromo limeorodeshwa kama kundi la kigaidi na serikali ya Ethiopia, iliyoishutumu kufanya mauaji ya maangamizi dhidi ya jamii ya wachache hasa Amhara katika eneo la Oromia mwezi Juni. Walioshuhudia wanasema zaidi ya watu 200 waliuawa.

Hata hivyo, kundi hilo limeendelea kukanusha madai hayo na kurejesha lawama kwa wanajeshi wa serikali ya Ethiopia na washirika wake. Wanajeshi hao waliwashambulia mara kadhaa waasi hao na kusababisha pia mauaji ya raia.

TPLF yaondolewa katika orodha ya makundi ya kigaidi Ethiopia

Itakumbukwa kwamba wakati wa mgogoro wa Tigray, waasi wa Oromo walitangaza kujiunga kwa muda mfupi na wapiganaji wa Tigray. Lakini wiki iliyopita wabunge wa Ethiopia walikiondoa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF, katika orodha ya makundi ya kigaidi, ikiwa ni zaidi ya miezi minne baada ya makubaliano ya amani kuumaliza mgogoro uliosababisha mauaji ya maelfu ya watu nchini humo.

Chanzo: afp/ap

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW