Abiy Ahmed:Vikosi vya Tigray vijisalimishe ndani ya masaa 72
23 Novemba 2020Waziri mkuu Abiy Ahmed ametuma ujumbe akisema anautaka umma wa Mekelle kujinusuru kutokana na mashambulizi ya mizinga na kujikomboa kutokana na wanajeshi wa Tigray,na baada ya hapo hakutokuwepo na huruma.
Katika ujumbe huo wa waziri mkuu wa Ethiopia pia alitowa muda wa saa 72 kwa vikosi vya Tigray wajisalimishe akiwatanabahisha kwamba hawana namna tena.Ujumbe wake huo ulichapishwa katika ukurasa wa Twitta jana Jumapili jioni.
Pamoja na ujumbe huo wa Abiy Ahmed, msemaji wa jeshi la Ethiopia Dejene Tsegaye kwa upande mwingine alitowa maelezo kuhusu operesheni hiyo iliyopangwa dhidi ya mji mjii wa Tigray Mekelle. "Awamu zijazo ni sehemu muhimu ya operesheni ambayo inahusu kuuzingira mji mkuu Mekelle kwa kutumia vifaru,na kumaliza mapambano katika maeneo ya milimani na kuingia katika uwanja wa mapigano'' Alisema Tsegaye.
Jeshi linalenga kuwalazimisha wanajeshi wa Tigray kujisalimisha
Operesheni hiyo kwa mujibu wa msemaji huyo wa jeshi la Ethiopia inalenga kuwalazimisha wanajeshi wa Tigray kujisalimisha. Hata hivyo vikosi vya Tigray vya kundi la TPLF bado havikuweza kupatikana haraka kutoa tamko kuhusiana na suala hilo, ingawa kundi hilo la ukombozi wa watu wa Tigray kaskazini mwa Ethiopia limesema vikosi vyake vinachimba njia za chini kwa chini na viko imara.
Kwa upande mwingine shirika la habari la Reuters limefafanua pia kwamba haliwezi kuthibitisha juu ya matamko yaliyotolewa hivi karibuni kuhusu vita hivyo vya Tigray.Ifahamike kwamba madai yanayoripotiwa kutoka pande zote mbili za mgogoro ni vigumu kuthibitishwa kutokana na kutokuwepo mawasiliano ya simu na mtandao.
Miji kadhaa yadhibitiwa na jeshi la serikali ya Ethiopia
Juu ya hilo inaelezwa kwamba vikosi vya jeshi la shirikisho vimeitwaa miji kadhaa baada ya kufanya mashambulizi ya anga na ardhini na sasa inaelezwa kwamba wanajeshi hao wanawania kuukamata mji mkuu Mekelle,mji ulioko milimani unaokaliwa na kiasi watu 500,000 na ambako ni makao makuu wa TPLF.
Soma zaidi: Ethiopia yaudhibiti mji wa pili kwa ukubwa Tigray
Kufikia sasa inaelezwa kwamba mamia ya watu huenda wameshauwawa na zaidi ya 30,000 wamekimbilia nchi jirani ya Sudan. Jumuiya ya kimataifa imetowa mwito wa kufanyika mazungumzo kuumaliza mgogo huo lakini waziri mkuu Abiy amekataa katakata kukaa na viongozi wa TPLF.
Chanzo: AP