1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abiy aliamrisha jeshi kuushambulia mji wa Mekele

Yusra Buwayhid
26 Novemba 2020

Hatima ya raia wa mkoa wa Tigray iko mikononi mwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akijiandaa kufanya shambulio kwenye mji mkuu wa Mekelle.

Äthiopien Ministerpräsident Abiy Ahmed Ali
Picha: Tiksa Negeri/REUTERS

  

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema Alhamisi kwamba jeshi limeamrishwa kusonga mbele na mashambulizi katika mji mkuu wa Mekele wa mkoa wa Tigray.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya hapo jana kumalizika muda wa kusalimu amri wa saa 72, waliopewa viongozi wa Tigray.

Soma zaidi: Jeshi la Ethiopia linasonga mbele katika mji mkuu wa Tigray, Makele

Aidha Abiy amewataka wakazi wa mji huo wapatao nusu milioni, kubakia majumbani mwao na kuweka chini silaha.

"Tutachukua tahadhari ya hali ya juu kuwalinda wakazi," imesema taarifa hiyo ya serikali.

Tamko la Abiy limekosolewa vikali na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, yakisema kwamba linaweza kusababisha ukiukaji wa sheria za kimataifa na kuwaweka raia katika hali ya hatari zaidi.

Wakazi wa Tigray waliokimbia makazi yao kutokana na vita katika mkoa huo wa kaskazini.Picha: Mohamed Nureldin Abdallah/REUTERS

Hali ya kibinadamu sio nzuri Tigray

Umoja wa Mataifa umeonya kwamba upungufu wa mahitaji ya msingi umekuwa wa kiwango kikubwa katika mkoa huwo wa Tigray wenye mapigano. Na kwamba wakazi wake wapatao milioni 6 wamezingirwa na mji wake mkuu uko hatarini kuvamiwa na vikosi vya serikali kuu ya Ethiopia, vikiwa na nia ya kuwakamata viongozi wa mkoa huo.

"Ni hali iliyonivunja moyo. Ni tukio linalotisha na ambalo linaniumiza sana kuliko ninavyoweza kulielezea, kuiona nchi yangu ikiwa katika hali kama hii. Jinsi Waethiopia wanavyofanya mashambulizi ya kikatili dhidi ya ndugu zao wa kike kwa kiume. Kwa hivyo ni janga lisilofikirika," amesema mkuu wa tume ya haki za binadamu Ethiopia, Daniel Bekel.

Soma zaidi: Vikosi vya Tigray vyarusha maroketi kuulenga mji wa Bahir Dar

Wakati ulimwengu ukiwa na wasiwasi juu ya yanayoendelea nchini humo, waziri mkuu Abiy amelikataa pendekezo la jumuiya ya kimataifa la kufanyika mazungumzo kati ya serikali yake na viongozi wa Tigray ili kusitisha mapigano hayo.

Taarifa ya Ofisi ya Abiy imeitaka jumuiya ya kimataifa kutoingilia mzozo huo, hadi pale serikali ya Ethiopia itakapoiomba msaada.

Tamko hilo la ofisi ya serikali limetolewa wakati vifaru vya kijeshi vikiwa tayari kwa mshambulizi nje kidogo ya mji mkuu wa Mekele.

Lakini mawasiliano katika mkoa huwo wa Tigray yanatajwa kuwa ni mabaya. Na haijulikani hakika ni watu wangapi waliosikia taarifa hiyo ya onyo la serikali pamoja na kitisho cha mashabilizi makali ya silaha yatakayofuatia.

Vyanzo: (ap,afptv)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW