1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abiy na kundi la OLA walaumiana juu ya mauaji ya Oromiya

5 Julai 2022

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na waasi wa Jamii ya Oromo wamelaumiana kwa mauaji ya halaiki katika eneo la Oromiya, ambako mamia ya watu wameangamia katika miezi ya hivi karibuni kwenye mvutano wa kikabila.

Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed
Picha: Tiksa Negeri/REUTERS

Kulingana na kamisheni ya kutetea haki za binaadamu nchini humo, mauaji ya hivi karibuni kabisa yalitokea jana Jumatatu katika vijiji viwili katika eneo la Kellem Wollega. Shirika hilo pamoja na Waziri Mkuu Ahmed wamelilaumu kundi la ukombozi la waoromo OLA ambalo ni kundi lililopigwa marufuku na kuorodheshwa kama kundi la kigaidi, kuhusika na mauaji hayo ambayo Abiy ameyaita kama "mauaji ya halaiki".

Hata hivyo msemaji wa kundi la OLA Odaa Tarbii amekanusha madai hayo, akisema wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ndio waliohusika huku akiwalaumu wanajeshi waliopelekwa huko hivi karibuni kukunja mikono wakati maovu hayo yakitokea.

Abiy awatuhumu waasi wa Oromo kufanya mauaji ya kimbari

Moja ya watu walioshuhudia mauaji  hayo aliyenukuliwa na shirika la habari la ndani nchini humo, amesema miili takriban 300 ilichukuliwa kutoka eneo la mapambano yalioanza jana usiku. Bado mpaka sasa hakuna idadi rasmi iliyotolewa na serikali kuhusu walioangamia na kujeruhiwa lakini msemaji wa Abiy Ahmed Billene Seyoum, aliwaambia waandishi habari wiki iliyopita kwamba watu 338 walioangamia tayari wametambuliwa.

Lakini shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha madai ya pande zote mbili kutokana na mawasiliano kukatwa. Msemaji wa kundi la Oromia hakupatikana kutoa maoni yake, na hata msemaji wa serikali Legesse Tulu hakuweza kupatikana kutoa taarifa zaidi juu ya waliojeruhiwa.

Oromiya inaendelea kushuhudia mashambuloizi ya mra kwa mara ya kikabila

Wapiganaji wa kundi la waasi wa TPLF Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Oromiya, iliyo na idadi ya watu milioni 110 imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya kikabila, yanayosababishwa na lawama kuhusu hali ya kisiasa katika eneo hilo na kutelekezwa na serikali kuu ya Ethiopia.

Hali imezidi kuwa mbaya huko tangu kundi la ukombozi wa watu wa Oromo  lilipojiunga na kundi la waasi wa Tigray TPLF linalopambana na wanajeshi wa serikali kaskazini mwa taifa hilo tangu mwezi Novemba mwaka 2020.

soma zaidi: Waasi wa Ethiopia wanasema serikali haiwezi 'kuaminiwa'

Lakini wakati Abiy na vikosi vilivyotiifu kwake wakisema wanajaribu kumaliza vita vya Tigray, umwagikaji wa damu unaoshuhudiwa katika eneo la Oromiya unaonesha wazi kuwa mivutano ya kikabila nchini humo inatishia kukwamisha juhudi za kumaliza migogoro hiyo.

Kwa sasa shirika la kutetea haki za binaadamu nchini humo limetoa wito wa wanajeshi zaidi kupelekwa Oromiya ili kudhibiti hali, kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni yaliyotokea huko.

Mashirika ya ndani ya Ethiopia na mataifa ya Magharibi wametaka uchunguzi huru kufanywa juu ya mauaji hayo ili kuthibitisha ukweli kuhusu unyama unaodaiwa kufanywa na Abiy pamoja na jeshi lake katika eneo hilo la Oromiya.

Chanzo: Reuters/AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW