Abiy yupo 'uwanja wa vita' kupigana na waasi
25 Novemba 2021Mapigano hayo ya kaskazini mwa nchi ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika yamewauwa maelfu ya watu na kuwalazimu mamia ya maelfu ya wengine kuishi katika mazingira yanayofanana na baa la njaa. Serikali za kigeni zimewaambia raia wake waondoke wakati vita vikiongezeka, na hofu kuwa waasi wa Tigray huenda wakaingia mji mkuu Addis Ababa. Shirika la habari la FANA limetangaza kuwa Abiy, ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2019, sasa anaongoza mashambulizi dhidi ya waasi, akiwa katika uwanja wa mapambano tangu jana. Haikubainika wazi yuko sehemu gani ya mapambano.
Shirika la habari la serikali halikuonyesha picha za Abiy akiwa vitani, na maafisa hawajajibu maombi ya kutaka maelezo zaidi kuhusu aliko.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano, kauli aliyoitoa akiwa Colombia, katika maadhimisho ya miaka mitano ya muafaka wa amani kati ya serikali na waasi wa FARC. "Mchakato wa amani nchini Colombia unanihimiza kutoa wito wa dharura kwa pande zote hasimu za mgogoro nchini Ethiopia kusitisha maramoja mapigano bila masharti, kuiokoa nchi na kuruhusu mazungumzo kati ya Waeithiopia, kuutatua mzozo huo na kuiwezesha Ethiopia kuendelea kuchangia kwenye utulivu wa kikanda."
Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imeonya kuwa "hakuna suluhisho la kijeshi” kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia.
Shirika la habari la FANA limesema tangazo la Abiy kwenda katika uwanja wa mapambano, limewahimiza wengi kujiunga na kampeni ya vita. Mamia ya wapiganaji wapya walishiriki hafla jana kwa heshima yao katika eneo la Kolfe la mji mkuu. Mshindi wa dhahabu katika Olimpiki na shujaa wa taifa Haile Gebreselassie ameahidi kujiunga vitani dhidi ya waasi. "Mwanamichezo aghalabu ni balozi wa amani. Sasa ninaposema naenda kwenye uwanja wa mapambano, watu watasema....nini! subiri kwanza. huenda wakasema 'umekuwa mpatanishi na wewe ni mwanamichezo, michezo inahusu amani na upendo. hapana. Ungefanya nini kama uwepo wa nchi yako upo hatarini? Unaweka kila kitu chini. Hakuna kitakachokuzuia. sahamani!"
Wakati ikiwahimiza raia wake kupigana, serikali ya Abiy inasisitiza kuwa mafanikio ya waasi wa TPLF sio makubwa kama inavyoripotiwa, ikisisitiza kile inachosema ni habari za uwongo za vyombo yva habari na tahadhari za kutisha za usalama kutoka kwa balozi za Magharibi. Vita hivyo vimezusha mgogoro wa kibinadamu, huku kukiwa na ripoti za mauaji ya kikatili na ubakaji wa watu wengi
AFP