1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ACT Wazalendo kuchagua mrithi wa Maalim kuwa makamu wa rais

George Njogopa26 Februari 2021

Chama cha ACT Wazalendo nchini Tanzania, kimeanza vikao vyake vya ndani Ijumaa kwa ajili ya kupitia na hatimaye kuchagua jina la atakayerithi nafasi ya makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar.

Zitto Kabwe, Joran Bashange und Salim Abdalla Biman
Picha: DW/Said Khamis

Kiti cha makamu wa kwanza wa rais Zanzibar kiliachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho na mwanasiasa mkongwe, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefariki dunia Februari 17.

Kikao hicho ambacho kitawakutanisha vigogo wa chama hicho kupitia kamati ya uongozi chini ya kiongozi wake mkuu, Zitto Kabwe, ndicho kitakachotegua kitendawili kinachosubiriwa na walio wengi juu ya nani hasa atavaa viatu vya Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, mmoja wa wanasiasa bingwa kabisa wa zama zake na ambaye wengi wanakubaliana kwamba pengo lake ni shida kuzibika.
Soma pia:

Kikao hiki ambacho kinatarajiwa kufanyika mchana huu jijini Dar es Salaam kinafanyika kukiwa kumesalia siku tano tu, kabla ya tarehe ya mwisho ya kuapishwa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais kutimia kama inavyoelekezwa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na katika mabadiliko yaliyofanyika mwaka 2010, ambayo inatoa siku 14 baada ya mtu aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kuondoka.

Hata hivyo, chama hicho hakitarajii kulitaja hadharani jina la kiongozi atakayepitishwa badala yake litapelekwa moja kwa moja kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein All Mwinyi, ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kutangaza uteuzi huo.

Ingawa hakuna anayeweza kubashiri ni nani hasa mwenye nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya nguli huyo wa siasa za Zanzibar aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 77, hata hivyo tayari majina kadhaa yamekuwa yakichomoza ndani ya chama hicho.
Soma pia:

Miongoni mwa wanaopigiwa upatu kuchaguliwa ni Haji Duni HajiPicha: DW/M. Ghassani

Miongoni mwa majina hayo ni pamoja mwanasiasa wa siku nyingi na mwenye uzoefu wa muda mrefu wa purukushani za vyama vya upinzani, Haji Duni Haji, maarufu kama Babu Duni. Yeye ndiye makamu mwenyekiti wa ACT Wazalendo visiwani Zanzibar na anatajwa kwa uhodari wake wa kujenga hoja wakati anaposhiriki mijadala ya aina mbalimbali. Akiwa amezaliwa Novemba 26,1950 alikuwa miongoni mwa mawaziri waliofanya vyema wakati ilipoundwa serikali ya kwanza ya umoja wa kitaifa katika mwaka 2010 hadi 2015.
 

Kando na yeye, jina la Nassor Ahmed Mazrui linachomoza katika kinyang'anyiro hicho na anaelezewa kama mtu anayekubalika ndani ya chama na hata nje yake. Akiwa amezaliwa mwaka 1960, naye pia amewahi kuwa sehemu ya baraza la mawaziri katika serikali ya awali ya Umoja wa Kitaifa iliyokuwa ikiongozwa na Dk. Ali Mohammed Shein.

Nalo jina la Othman Masoud Othman liko sehemu ya wale wanaotajwa kwenye mbio hizo. Licha ya kutokujinasibisha hadharani kuwa sehemu ya vyama vya upinzani, Masoud anatambuliwa kwa msimamo wake usioyumba wa kutetea maslahi ya Zanzibar ndani na nje ya nchi na pia uwezo wake mkubwa kwenye taaluma yake ya sheria.

Othman Masoud OthmanPicha: DW/M. Khelef

Masoud alifanya kazi kama mwanasheria mkuu wa serikali wakati wa utawala wa awamu ya kwanza wa Dk.Shein. Mbali ya kuwa mtu anayetajwa kupenda kuona maslahi ya Zanzibar yakizingatiwa inapokuja suala la Muungano, lakini pia anaheshimika kwa uzoefu wake mkubwa serikalini.

Lakini pia kuna Mansour Yusuph Himid, ambaye kabla ya kwenda upinzani amewahi kuwa mjumbe wa  Baraza la Wawakilishi na waziri kwenye serikali ya CCM.
Soma pia:

Wengi wanaofuatilia kinyang'anyiro hicho wanaona kuwa yoyote kati ya hao atayepitishwa anaweza kulivusha vyema gudurumu la chama chake na hata kusimamia vyema misingi iliyoasisiwa na Maalim Seif aliyeingia kwenye maridhiano ili kunusuru umoja na uhai wa Zanzibar.

Maalim Seif Sharif alizikwa Pemba tarehe 18.02.2021Picha: Salma Said

Mohammed Issa ambaye amekuwa akizifuatilia kwa karibu siasa za Zanzibar anaamini ACT Wazalendo itapita salama kwenye hatua hiyo na hatimaye kumpata mmoja wao kwa vile wote hao wanaotajwa wamebeba misingi ya kulinda na kutetea maslahi ya Zanzibar, ambayo ndiyo siasa iliyomjenga na kumuinuwa kiongozi wao, Marehemu Maalim Seif:
 

Kwa upande mwengine, chama hicho kimepanga kufanya dua maalumu kesho Jumamosi kwa ajili ya kumuombea Maalim Seif Sharif Hamad, dua itakayofanyika nyakati za jioni katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW