ACT-Wazalendo yapinga ushindi wa Dkt. Hussein Mwinyi
1 Novemba 2025
Kupitia taarifa rasmi, ACT-Wazalendo imesema, "Wamepora Wazanzibari sauti yao…Suluhisho pekee la haki ni kufanyika kwa uchaguzi mpya."
Afisa mwandamizi wa chama hicho cha upinzani ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, masanduku ya kura yalijazwa mapema, watu waliruhusiwa kupiga kura zaidi ya moja bila ya vitambulisho, na waangalizi wa upinzani walifukuzwa katika vituo vya kuhesabia kura. Madai hayo ya upinzani yametolewa wakati chama tawala, CCM, kinatarajiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari muda wowote hii leo.
"Hakujawahi kufanyika uchaguzi huru na wa kuaminika tangu mwaka 1995,” amesema mzee mmoja mwenye umri wa miaka 70, akiutaja uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini Tanzania.
Hakuna aliyehojiwa na AFP alikuwa tayari kutaja jina lake kamili huku mmoja akisema, "Tunaogopa kuzungumza kwa sababu wanaweza kuja kutuchukua majumbani mwetu.”
Dkt. Hussein Mwinyi alitangazwa mshindi wa urais wa Zanzibar kwa kupata asilimia 74.8 ya kura, akimshinda mpinzani wake wa karibu Othman Masoud Othman wa ACT-Wazalendo aliyepata asilimia 23.2. Mwinyi ambaye alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2020, ataiongoza Zanzibar kwa miaka mingine mitano hadi mwaka 2030 na anatarajiwa kuapishwa rasmi tarehe 3 Novemba.