ADDIS ABABA: Ghana yachaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika
29 Januari 2007Umoja wa Afrika umeichagua Ghana kuwa mwenyekiti wake kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao baada ya Sudan kupingwa kwa sababu ya mzozo wa Darfur.
Kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia hii leo, rais wa halmashauri ya umoja huo, Alpha Oumar Konare, amesema rais wa Ghana John Kufuor atakuwa mwenyekiti kwa mwaka mmoja.
´Rais Kufor wa Ghana ameteuliwa kwa ridhaa ya wote kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika pakiwepo azma ya kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Ghana. Pendekezo hilo limeungwa mkono pia na Sudan.´
Hapo awali katika mkutano huo wa mjini Addis, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, aliwatolea mwito viongozi wa Afrika wasaidie kumaliza machafuko yanayoendelea katika jimbo la Darfur kwa kuunga mkono pendekezo la kutuma wanajeshi wa Umoja wa Afrika na wa Umoja wa Mataifa kulinda amani Darfur.
´Tangu nilipochukua uongozi kama katibu mkuu nimeupa mzozo wa Darfur kipaumbele. Ushirikiano baina ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa ni muhimu kutafuta njia za kukabiliana na mzozo huu mkubwa wa kibinadamu duniani.´
Sudan bado inapinga azimio la Umoja wa Mataifa linalotaka wanajeshi elfu 22 wa kulinda amani wapelekwe Darfur kuchukua nafasi ya jeshi la Umoja wa Afrika linalolinda amani katika eneo hilo.
Aidha Ban Ki Moon ametaka wafanyakazi wa kutoa misaada waruhusiwe kutoa huduma zao katika eneo la Darfur. Mashirika ya misaada yamekuwa yakionya kwamba shughuli zao zinakaribia kusambaratika katika eneo hilo.