Addis Ababa. Umoja wa Afrika wakataa miito ya kuishutumu Zimbabwe katika hatua yake ya kuwavunjia nyumba wakazi wa mjini waliojenga ovyo.
25 Juni 2005Umoja wa Afrika umekataa miito kutoka katika mataifa ya magharibi pamoja na muungano wa makundi ya kimataifa ya haki za binadamu kuingilia kati na kusimamisha hatua ya serikali ya kuwachukulia hatua kali watu waliojenga ovyo katika mji mkuu wa nchi hiyo pamoja na sehemu nyingine nchini Zimbabwe.
Msemaji wa umoja wa Afrika AU amesema kuwa umoja huo una masuala mengine mengi muhimu ya kufanya.
Kiasi cha watu 300,000 wameachwa bila makaazi tangu kampeni hiyo ianze mwezi mmoja na nusu uliopita.
Polisi wamekuwa wakiwafukuza wakazi na kuvunja nyumba zao katika mji mkuu Harare , pamoja na miji mingine. Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, amesema kuwa uvunjaji huo una lengo la kupambana na uhalifu. Lakini wakosoaji wanasema kuwa operesheni hiyo ina lengo la kuwaadhibu watu wanaounga mkono vyama vya upinzani.