ADDIS ABABA : Upinzani watowa wito wa mgomo wa taifa
2 Oktoba 2005
Makundi mawili makuu ya upinzani nchini Ethiopia hapo jana yametowa wito wa mgomo wa taifa wa siku tatu kupinga sera za serikali na kupigwa marufuku kwa maandamano.
Yacob Hailemariam msemaji wa Muungano wa Umoja wa Demokrasia amewaambia waandishi wa habari kwamba wanatowa wito kwa Waethiopia wote kubakia nyumbani kwa siku tatu kuanzia kesho.Akiongezea Naibu Mwenyekiti wa muungano huo Birtukan Mideksa amesema dhamira ya mgomo huo ni kuonyesha kupinga kwa wananchi ukiukwaji wa taratibu ulioshuhudiwa katika uchaguzi wa Mei 15,ukiukaji wa kila siku wa haki zao za kidemokrasia ikiwemo haki ya kukusanyika na kuweka shinikizo kwa serikali kuacha kufanya hivyo.
Hapo Alhamisi waziri wa habari Berekat Simon amesema maandamano yaliyopigwa marufuku yaliokuwa yamepangwa kufanyika leo hii katika mji mkuu wa Addis Ababa sio halali kwa sababu yalikuwa yanataka kutowa wito wa kupinduliwa kwa serikali iliopo madarakani.
Serikali ya Ethiopia imekuwa ikipinga kabisa wito wa upinzani wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.