1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA : Waafrika wataka Mugabe ashiriki mkutano

6 Oktoba 2007

Wanadiplomasia wa Afrika wamewasilisha msimamo wa pamoja leo hii kuunga mkono kuhudhuria kwa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe mkutano ujao wa viongozi wa Ulaya na Afrika licha ya kuwepo kwa mashaka makubwa ya Ulaya.

Afisa kutoka makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa amesema Umoja wa Afrika unataka nchi zote za Afrika zishiriki kwenye mkutano huo wa viongozi uliopangwa kufanyika mjini Lisbon nchini Ureno hapo mwezi wa Desemba.

Afisa huyo ambaye amekataa kutajwa jina lake amepinga matamshi yaliotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner ambaye amedai kwamba Umoja wa Afrika ulikuwa umependekeza kumshawishi Mugabe asihudhurie mkutano huo.

Mugabe amekuwa chini ya shutuma kali za kimataifa kwa ukiukaji wa haki za kisiasa na kibinaadamu nchini mwake na kuitumbukiza nchi hiyo kwenye mzozo mbaya kabisa wa kiuchumi.