ADDIS ABABA : Wajadili kikosi cha Dafur
12 Juni 2007Umoja wa Afrika,Umoja wa Mataifa na serikali ya Sudan hapo jana wameanza mazungumzo mjini Addis Ababa Ethiopia juu ya uwekaji wa wa kikosi mchanganyiko cha takriban wanajeshi 23,000 katika jimbo lililokumbwa na vita la Dafur nchini Sudan.
Mazungumzo hayo yanakusudia kufunguwa njia ya kuwekwa kwa haraka kikosi hicho mchanganyiko cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.Umoja wa Mataifa umekuwa ukitaka kukiongoza kikosi hicho wakati Sudan inasisitiza kwamba kiongozwe na Umoja wa Afrika.
Wakati huo huo serikali ya Sudan imekataa mpango wa Ufaransa kuandaa mkutano wa kimataifa mjini Paris baadae mwezi huu juu ya mzozo huo wa Dafur kwa madai kwamba wakati sio muafaka.
Inakadiriwa kwamba watu 200,000 wameuwawa kutokana na mzozo huo wa Dafur.