ADDIS ABABA:Ghasia Addis Ababa watu 27 wameuawa.
3 Novemba 2005Ghasia zinazoendelea baina ya waandamanaji wa upande wa upinzani na askari polisi katika mji mkuu wa Ethiopia,Addis Ababa hadi sasa zimesababisha watu takriban 27 kuuawa.
Hali hiyo imesababisha kutolewe wito na jumuia ya Kimataifa,ukiwemo Umoja wa Afrika na Marekani,kutaka ghasia hizo zikomeshwe mara moja.
Hadi sasa watu 150 wamekwishajeruhiwa kufuatia ghasia hizo,baada ya chama kikuu cha upinzani nchini humo kuitisha maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwezi wa Mei mwaka huu,ukisisitiza kuwa serikali iliiba kura.
Chama kikuu cha upinzani nchini Ethiopia cha Coalition of National Unity and Democracy(CUD),wanachama wake wanaofikia 1,000 pamoja na viongozi wake wote,wamekwishatiwa mbaroni katika operesheni iliyoendeshwa nchi nzima.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Sean McCormack amesema nchi yake inazitaka pande zote kuacha kushambuliana mara moja na kuitaka serikali ya Ethiopia kuunda Tume huru,itakayochunguza maandamano ya jana pamoja na yale ya tarehe 8 mwezi June ambapo watu wengi waliuawa.