ADDIS ABABA:Kiongozi wa AU John Kufuor atoa wito wa kuchangia majeshi
31 Januari 2007Matangazo
Kiongozi mpya wa Umoja wa Afrika AU Rais John Kufuor anatoa wito kwa viongozi wenzake kuchangia majeshi yao katika kikosi cha kulinda amani nchini Somalia.Mpaka sasa nusu ya majeshi yote yanayohitajika ndiyo yamepatikana huku kikao cha Umoja huo kikikamilika.
Kikao hicho kiliegemea zaidi majadiliano kuhusu ghasia nchini Somalia na eneo la magharibi la Darfur nchini Sudan.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo aliye pia rais wa Ghana,majeshi hayo yatapelekwa Somalia punde kikosi hicho kitakapokamilika na kuahidi kuwa Umoja wa Afrika AU unajitolea kumaliza kipindi cha ghasia nchini humo kilichodumu miaka 16.
Rais Kufuor alichaguliwa siku ya jumatatu kuongoza Umoja wa Afrika ulio na nchi 53 wanachama.