Adui aliyetangazwa na Trump: Antifa ni nini?
23 Septemba 2025
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza rasmi vuguvugu la Antifa kuwa shirika la kigaidi.Kwa mujibu wa Ikulu ya White House, Trump alisaini amri inayolitaja Antifa kama shirika la "kivita na la machafuko” linaloitisha kuiangusha serikali ya Marekani, vyombo vya utekelezaji wa sheria na mfumo wa mahakama kwa njia za vurugu. Hivyo, limetajwa kuwa "shirika la kigaidi la ndani.” Uchunguzi utaanzishwa dhidi ya Antifa na pia wale wanaolisaidia kwa namna ya kiutawala au kifedha.
Trump alikuwa ametangaza hatua hiyo muda mfupi baada ya kuuawa kwa Charlie Kirk, mwanaharakati wa mrengo wa kulia, mnamo Septemba 10. Pia, katika ibada ya mazishi ya Kirk kwenye uwanja uliojaa watu katika jimbo la Arizona, Trump alirudia madai yake kwamba "mrengo wa kushoto wenye misimamo mikali” ndiyo uliosababisha kifo cha Kirk.
Mkusaniko usio rasmi badala ya shirika lenye muundo
Neno Antifa ni kifupi cha "Antifaschistische Aktion” (Harakati ya Kupinga Ufasisti); si chama au shirika lililo na uongozi wa kati, bali ni vuguvugu lililo huru linalojumuisha makundi na watu binafsi wanaopinga ufasishti, ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Wayahudi, utaifa wa kikabila, upotoshaji wa kihistoria wa mrengo wa kulia na aina nyingine za itikadi za mrengo wa kulia.
Antifa hujinasibisha na mrengo wa kushoto hadi ule wa mrengo mkali wa kushoto na inafanya shughuli zake kote duniani — hasa barani Ulaya na Amerika Kaskazini. Mizizi yake inarudi nyuma hadi Ujerumani ya miaka ya 1920 na 1930, katika nyakati zenye misukosuko ya kisiasa za Jamhuri ya Weimar, ambapo wanaharakati na makundi ya mrengo wa kushoto walipinga ueneaji wa harakati za kinazi.
Ilitangazwa mwaka 1932 na Chama cha Kikomunisti cha Ujerumani (KPD) — si kama shirika, bali kama vuguvugu la pamoja dhidi ya NSDAP. Vuguvugu kama hilo pia zilijitokeza katika nchi nyingine, kwa mfano Italia dhidi ya utawala wa kifashisti wa Benito Mussolini au Uhispania kama majibu ya udikteta wa Franco.
Kutoka kupinga ubepari hadi uliberali wa kiraia
Hadi leo, Antifa ni zaidi ya mkusanyiko usio rasmi wa makundi madogo kutoka mrengo wa kushoto hadi ule wa mrengo mkali wa kushoto. Kihistoria, "ufashisti” ulikuwa ni dhana ya mapambano ya kikomunisti, iliyohoji pia uhalali wa ubepari. Ndiyo maana nembo ya vuguvugu la Antifa ina bendera mbili zilizogeuzwa kushoto na kuelekea kulia: nyekundu inayowakilisha ujamaa/ukomunisti, na nyeusi inayoashiria machafuko.
Hata hivyo, dhana ya kupinga ufasisti imeendelea kubadilika kwa miongo kadhaa; leo pia kuna "ufashisti wa kiliberali wa kiraia” unaopigania kulinda demokrasia na utawala wa sheria, ambavyo unaona viko hatarini kutokana na misimamo mikali ya mrengo wa kulia.
Amani au msimamo mkali? Malengo ya Antifa
Kama ilivyo pana dhana ya "kupinga ufasisti,” ndivyo pia ulivyo mkusanyiko wa vuguvugu la "Antifa.” Makundi mengi yanayojitambulisha kama sehemu ya harakati hiyo hupinga vikali mrengo wa kulia na mifumo ya kiimla bila kutumia vurugu; kwa mfano, hufanya utafiti na kuchapisha taarifa kuhusu mitandao ya mrengo wa kulia, kuandaa maandamano na mikutano ya kupinga au kuondoa propaganda za mrengo wa kulia.
Wakati huohuo, kuna makundi ya kijeshi yanayoruhusu matumizi ya nguvu kutimiza malengo yao au hata kutumia vurugu yenyewe kwa namna mbalimbali. Makundi haya hujitambulisha kama "huru,” "wapiganaji,” au "Antifa isiyo tegemezi,” yakijitenga kwa makusudi na wapinga ufashisti wa kiraia au wale wanaofuata sheria za dola.
Kwa hivyo, Antifa ni mkusanyiko wenye taswira nyingi, unaojumuisha miungano midogo-midogo bila muundo wa kudumu wa shirika. Swali la iwapo na kwa kiwango gani matumizi ya nguvu dhidi ya mrengo wa kulia ni halali, limekuwa likijadiliwa mara kwa mara ndani ya harakati hizi — jambo ambalo mara nyingi limezua ukosoaji mkubwa wa umma dhidi ya vuguvugu hili.
Antifa nchini Marekani
Antifa sasa ipo katika nchi nyingi za ulimwengu wa (Magharibi) — ikiwemo Marekani. Hata hivyo, pia huko hakuna shirika kuu lililo na uongozi wa kati; badala yake, Antifa Marekani inaundwa na makundi ya kienyeji yanayounganishwa kiitikadi kupitia dhana ya kupinga ufashisti.
Kuanzia miaka ya 1980, makundi haya yalianza kupinga kwa vitendo shughuli za Wanazi mamboleo wa Marekani, makundi ya Skinhead wenye ubaguzi wa rangi na pia chama cha Ku-Klux-Klan.
Leo hii, yanayojulikana zaidi ni pamoja na "Rose City Antifa” lililoanzishwa mjini Portland, Oregon mnamo mwaka 2007; kundi la "Anti-Racist Action (ARA)” linalofanya shughuli katika miji mingi ya ukanda wa Midwest; na pia "Refuse Fascism,” kundi lililoundwa baada ya uchaguzi wa kwanza wa Donald Trump kuwa rais wa Marekani mwaka 2016, na tangu hapo limekuwa likiandaa mara kwa mara maandamano dhidi ya ufasisti na mifumo ya kiimla.
Tangu mwanzo Antifa imekuwa kikwazo kwa Donald Trump. Mara kadhaa — hata wakati wa muhula wake wa kwanza — Trump alitangaza kuwa na nia ya kuliorodhesha vuguvugu hilo kama "shirika la kigaidi.” Hata hivyo, wataalamu na taasisi kama FBI na Wizara ya Usalama wa Ndani wanasema mpango huo hauwezi kutekelezeka kisheria kwa urahisi.
Mashaka makubwa ya kisheria
Tayari mwaka 2017, Mkurugenzi wa FBI wa wakati huo, Christopher Wray, alieleza kwamba haiwezekani kuipa Antifa hadhi ya shirika la kigaidi kwa sababu haina muundo rasmi wala uongozi wa juu. Hata hivyo, taasisi hiyo huichunguza Antifa kama "harakati zenye uwezekano wa kutumia vurugu” na hufanya uchunguzi dhidi ya wahusika binafsi wanaojinasibisha na "itikadi za Antifa.” Kwa ujumla, vuguvugu hili linaelezwa kuwa na mchanganyiko mkubwa mno kiasi kwamba haliwezi kufafanuliwa kama shirika lenye mipaka wazi.
Uchunguzi uliofanywa mwaka 2020 na Kitengo cha Utafiti cha Bunge la Marekani ulifikia hitimisho linalofanana: Antifa nchini Marekani haina viongozi wala muundo wa shirika kitaifa. Badala yake, linaundwa na "makundi na watu binafsi huru, wenye misimamo mikali na wanaoshirikiana kiitikadi.”
Jinsi ambavyo serikali ya Marekani itaweza kutekeleza uchunguzi ilioahidi dhidi ya vuguvugu hili bado haijulikani, hasa ikizingatiwa kutokuwepo kwa muundo wa shirika ulio thabiti.
Aidha, kuna Kifungu cha Kwanza cha Katiba ya Marekani kinacholinda uhuru wa kujieleza na kukusanyika pamoja na uhuru wa imani za kisiasa — hata maoni yenye misimamo mikali, ya kupinga mfumo au ya kupinga serikali yanalindwa na katiba.
Hivyo kuipa Antifa hadhi ya kigaidi kunaweza kutafsiriwa kama jaribio la kufanya maoni ya kisiasa yanayolindwa kisheria yaonekane kama uhalifu — jambo ambalo lingekiuka Kifungu cha Kwanza cha Katiba ya Marekani.