1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Adui mkubwa wa Lebanon ni serikali yake.

9 Agosti 2020

Sababu za janga la hivi karibuni la mripuko katika bandari ya mjini Beirut zinahitaji kuchunguzwa, lakini sio na serikali hiyo bali taasisi za nje. Haya ni maoni ya mwandishi wa DW Diana Hodali.

Libanon Beirut | nach Explosion im Hafenviertel
Picha: Reuters/M. Azakir

Lebanon imepitia mengi. Vita, mizozo na majanga. Lakini kile kilichotokea hivi karibuni katika bandari ya Beirut kilishinda chochote kile ambacho raia wa nchi hiyo wangefikiria. Mripuko huo uliharibu sehemu kubwa ya mji huo mkuu kusalia kuwa vifusi, kuwafanya watu laki 3 kupoteza makazi na kuondoa matumaini ya maisha bora ambayo yalifurahiwa hasa na vijana wadogo nchini humo.

Licha ya kila kitu ambacho kimetokea nchini humo hadi kufikia sasa, kushindwa kwa kiasi kikubwa kwa serikali ya nchi hiyo kutimiza majukumu yake kumezidisha hofu ya raia wa nchi hiyo. Kwa siku kadhaa sasa, shughuli ya kutafuta waliopotea katika mkasa huo imekuwa ikiendelea katika mji huo bila ya msaada wa serikali na hakuna hata msamaha uliotolewa na kundi la wanasiasa mashuhuri na pia hakuna aliyejiuzulu. Badala yake, serikali imekuwa ikipongeza ujasiri wa raia wa nchi hiyo.

Ni wazi kwamba hakuna aliye madarakani anayejihisi kuhusika na ukweli kwamba kemikali ya Ammonia Naitreti yenye uwezo mkubwa wa kuripuka ilihifadhiwa katika bandari ya Beirut kwa muda wa miaka sita karibu na maeneo ambayo watu wanafanya kazi na kuishi katikati mwa mji huo. Badala yake wamewakamata baadhi ya maafisa wakuu wa bandari.Kama hali inavyokuwa kila kunapokuwa na matatizo nchini Lebanon, hakuna aliye madarakani anayelaumiwa.

Rais wa Lebanon- Michel AounPicha: picture-alliance/AP/Lebanese government/D. Nohra

Lakini licha ya mitazamo mbali mbali ya watu, mripuko mkubwa uliotokea katika bandari hiyo ya Beirut ulitokana na ufisadi mkubwa katika serikali ya nchi hiyo. Kwa miaka kadhaa sasa, wanasiasa kutoka vyama vyote vya kisiasa wamekuwa wakipora nchi hiyo na kuisukuma katika matatizo. Hata wanasiasa wa upinzani, walishirikiana katika mfumo huo fisadi kujinufaisha. Inapofikia suala la maslahi, walikubaliana.

Masaibu ya Lebanon

Janga hilo ni la hivi punde zaidi na mfano unaotisha wa jinsi serikali moja hadi nyingine ya Lebanon zimeshindwa kutimiza majukumu yao ya kimsingi ambayo ni kuangalia maslahi ya wananchi .Kwa miaka kadhaa sasa, umeme umekuwa ukipotea kwa saa kadhaa kwa siku. Unaweza kujiuliza kwanini, na jibu ni kuwa wafanyabiashara matajiri ambao aidha wanatokea katika siasa ama kushirikiana kwa karibu nazo, hupata faida kila wakati watu wanapolipia umeme wa ziada.

Mbali na hayo kuna mirundiko ya taka. Kwa miaka kadhaa, mirundiko mikubwa ya taka imekuwa ikiongezeka karibu na uwanja wa ndege. Kumekuwa na bidhaa za plastiki zilizotapakaa karibu kila mahali katika fuo za bahari na uchafu wa kemikali haujakuwa ukitupwa kwa njia bora na kuhatarisha maisha ya watu. Wakati mioto mibaya zaidi ya misitu ilipotokea mnamo Oktoba mwaka 2019, serikali haikuwa na ndege yoyote ya kukabiliana na moto. Kuna mtu aliyesahau kuzishughulikia na kuzijaza mafuta. Nini kingine kinahitajika kusemwa?

Mbali na vita vya wenyewe kwa wenyewe, raia wengi wa Lebanon wameshuhudia vita mara mbili na Israeli, mizozo kadhaa ya kiuchumi, viwango vikubwa vya ukosefu wa ajira na mauaji ya kisiasa. Tangu mwezi Oktoba mwaka jana, waandamanaji wamekuwa wakitoa wito kwa wanasiasa mafisadi kujiuzulu. Hii  ni kwasababu wale wanaoshikilia uongozi ni wababe wa kivita waliopigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe  kabla ya kutafuta amani na kuendelea kujinufaisha na kuchochea ghasia katika misingi ya madhehebu.

Hadi pale mizizi ya matatizo nchini humo itakaposhughulikiwa na iwapo wababe hao wa kivita wataendelea kubaki madarakani, kuna tishio kwamba kwa mara nyingine, Lebanon itatumbukia katika mzozo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW