AFC/M23 wawateua mamia ya mahakimu mashariki mwa DRC
7 Novemba 2025
Waasi hao wa AFC/M23 wametangaza kuchapishwa kwa orodha ya mwisho ya mahakimu wapatao 378 waliochaguliwa kufuatia tathmini iliyofanywa na tume iliyopewa jukumu la kufufua mfumo wa haki na taasisi za mahakama huko mashariki mwa Kongo.
Hata hivyo, wananchi wameelezea mashaka yao juu ya watu hao walioteuliwa wakihofia vitendo vya upendeleo hasa ikizingatiwa kwamba waasi hao ndio wanaohusishwa na sehemu kubwa ya uhalifu uliofanywa katika maeneo wanayoyakalia ya Kivu Kaskazini na Kusini.
Christian Ciruza, ni mkazi wa Goma anasema hatarajii chochote kutoka kwa mahakimu hao kwa kuwa imani katika taasisi za mahakama imetiwa doa. Ciruza ameendelea kuwa wanachoweza kutarajia kutoka kwa mfumo huo wa haki ni kufunguliwa kwa kesi dhidi ya wale wote ambao wametenda uhalifu na ukiukaji wa haki za binadamu kuanzia mwezi Januari hadi leo hii akisisitiza kuwa kwa bahati mbaya, hilo haliwezi kutokea kamwe.
" Kwa hivyo, hatutarajii chochote cha maana kutoka kwao, mbali na kutatua kesi na migogoro midogo kati ya wananchi."
Mfumo Sambamba wa Haki
Wakili wa Kongo Pascal Shamavu, ambaye alilikimbia eneo la mashariki mwa DRC kabla ya waasi wa AFC/M23 kuliteka eneo hilo, ameelezea pia mashaka yake kuhusu suala la mahakimu hao walioteuliwa na waasi kusimamia haki. Kulingana na mwanasheria huyo, mahakimu hao watalazimika mara kadhaa kukiuka kiapo chao kama wataalamu wa sheria kwa kuwa watafanya kazi katika eneo lililo chini ya udhibiti wa waasi.
"Sio tu kwamba vyombo hivi vya mahakama vitakosa uhalali, lakini pia havitaaminika. Watu wanajiuliza ni kwa misingi gani ya kisheria wameteuliwa. Mahakimu walioteuliwa na waasi hawataweza kuwa waadilifu na watakuwa wakikiuka kiapo chao kila wakati ikiwa watalazimishwa na waasi."
Taasisi zisizo na uhalali
Huku juhudi za kidiplomasia zikiendelea ili kujaribu kurejesha mamlaka ya serikali kote nchini DRC, mtetezi wa haki za binadamu Pecos Kulihoshi anaamini kuwa mbinu hii ya waasi wa M23 haitakuwa na matokeo ya kudumu.
" Uongozi huu mpya unaokalia maeneo hayo si halali hata kidogo. Kwa maana hii, kila wanachofanya ni cha muda tu na kitadumu kwa wakati huu wakiyashikilia maeneo hayo. Na bila shaka, waasi hawa watalazimika kuondoka wakati fulani, hivyo kila walichounda kinaweza kuvunjwa ili serikali halali iweze kurejesha mamlaka yake."
Baada ya mahakimu hao kuteuliwa, sasa inasubiriwa kufahamu ni lini vyombo vya sheria huko Mashariki mwa Kongo vitaanza kufanya kazi kikamilifu. Kimsingi, mahakimu hao watatakiwa kurejesha mfumo wa sheria na haki katika maeneo hayo, ambapo kumekuwa kukiripotiwa mara kadhaa vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.