1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Goma njia panda baada ya mazungumzo ya Geneva

22 Aprili 2026

Waasi wa AFC M23 watoa mrejesho wa mazungumzo ya Geneva, huku wakazi wa Goma wakiendelea kuishi kwa hofu na kutokuwa na uhakika wa mustakabali wa usalama wao.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Goma 2025 | Kiongozi wa waasi Corneille Nangaa atishia kuelekea mji mkuu Kinshasa
Kiongozi wa AFC-M23 Corneille Nangaa akizungumza katika mmoja ya mikutano na waandishi wa habari mjini Goma.Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Mjini Goma, waasi wa AFC M23 wamefanya mkutano na waandishi wa habari kutoa mrejesho wa mazungumzo yaliyofanyika Geneva kuanzia Aprili 13 hadi 17, 2026.

Mkutano huo umefanyika wakati ambapo imepita mwaka mmoja tangu kundi hilo lilipoanza kudhibiti mji wa Goma pamoja na maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Licha ya juhudi za mazungumzo ya amani, hali ya usalama bado haijaimarika, na wakazi wengi wanaishi katika hofu huku wakikosa uhakika wa mustakabali wao.

Kongo yaadhimisha mwaka mmoja wa kutekwa kwa Goma

03:18

This browser does not support the video element.

Mafanikio ya awali lakini maswali bado yapo

Katika awamu ya kwanza ya mazungumzo iliyofanyika Montreux, pande husika ziliripoti mafanikio ya awali katika baadhi ya masuala muhimu.

Miongoni mwa yaliyojadiliwa ni kuachiliwa kwa wafungwa waliotambuliwa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ambapo wafungwa 778 walitajwa na 311 tayari wamepatikana.

Aidha, kulikuwa na makubaliano ya kuanzisha utaratibu wa kuthibitisha usitishaji wa mapigano chini ya usimamizi wa Mkutano wa Kimataifa kuhusu Kanda ya Maziwa Makuu, ukihusisha wanajeshi sita kutoka kila upande.

Masuala ya misaada ya kibinadamu na uhuru wa mashirika ya misaada kufanya kazi bila vikwazo pia yalijadiliwa, ingawa utekelezaji wake bado haujaonekana wazi.

Viongozi wa kikanda wajadili amani ya DRC Uganda

02:10

This browser does not support the video element.

Msimamo wa AFC M23 na hofu ya wakazi

Hata hivyo, bado kuna sintofahamu kuhusu mustakabali wa uasi huo—iwapo AFC M23 wataendelea kusonga mbele au kubaki katika maeneo wanayodhibiti.

Katibu Mkuu wa kundi hilo, Benjamin Mbonimpa, amesema lengo lao ni kubaki pamoja na raia na kuhakikisha usalama wao, huku wakisisitiza umuhimu wa mazungumzo na serikali ya Kinshasa.

"Sisi tutabaki pamoja na raia… na hatutaondoka kamwe,” amesema, akiongeza kuwa suluhisho la mgogoro linahitaji mazungumzo ya kina na serikali.

Kwa upande wa wakazi wa Goma, matumaini yanaonekana kupungua. Wengi wanaona mazungumzo haya kama marudio ya juhudi zilizopita ambazo hazikuleta mabadiliko ya kudumu.

Baadhi ya wakazi wanasema wamechoshwa na mazungumzo yasiyozaa matunda, wakihofia kuwa hali itaendelea kuwa ile ile licha ya mikutano ya mara kwa mara.

Vita vyarindima Kongo licha ya mkataba wa Trump

02:43

This browser does not support the video element.

MONUSCO yatarajiwa kuingilia kati

Wakati huo huo, mwakilishi wa Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuleta utulivu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, James Swan, anatarajiwa kuwasili Goma Aprili 24.

Ziara hiyo inalenga kujionea hali halisi ya usalama Mashariki mwa DRC na kutathmini hatua zinazoweza kuchukuliwa kusaidia kurejesha utulivu.

Kwa sasa, licha ya mazungumzo kuendelea, hali ya sintofahamu bado imetawala Goma, huku wakazi wakingoja kwa hamu kuona kama juhudi hizi zitaleta amani ya kudumu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW