AFCON 2013 : Cote D'Ivoire yaanza vizuri
27 Januari 2013Gervinho alihitimisha ushindi kwa timu yake inayopewa nafasi kubwa ya kushinda taji hili kwa goli lililofungwa katika dakika ya 88 na kuipatia Cote di'divoire ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Togo. Msakni alisubiri hadi dakika ya mwisho kuipa Tunisia ushindi wa goli moja dhidi ya mahasimu wao wa Afrika Kaskazini, Algeria.
Hadi sasa mechi tano kati ya nane zilizochezwa zimemalizika kwa sare, na tatu zimepata ushindi wa dakika za mwisho - Seidou Keita akiifungia Mali katika dakika ya 84 katika ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Niger siku ya Jumapili. Wakati ushindi wa jana Jumanne unamaanisha Cote di'divoire na Tunisia wako sawa katika uongozi wa kundi, walishinda katika namna tofauti.
Cote D'Ivoire yatamba
Cote di'voire ilishinda mchezo wa kufurahisha dhidi ya Togo wakati Tunisia na Algeria hazikuonekana kama zingefunga magoli hadi Msakni alipofunga goli maridhawa kutoka umbali wa mita 20.
Kitu zilichokuwa nazo timu mbili zilizoshinda ni kwamba hazikucheza vizuri kama zilivyotarajiwa. Cote di'voire ambayo nyota wake kama Didier Drogba, Kolo Toure, Didier Zokora na Emmanuel Eboue wanajaribu kwa mara ya mwisho kushinda kombe la mataifa ya Afrika walilolikosa tangu mwaka 1992, walifanya makosa kadha na walionekana kukosa mwelekeo.
Drogba mwenye umri wa miaka 34, alishindwa kuonyesha mchezo wa kuridhisha na alipumzishwa zikiwa zimesalia dakika 16 mchezo kumalizika. Mwenyewe alikiri kuwa mchezo ulikuwa mgumu, na kuongeza kuwa walifanya makosa mengi dhidi ya Togo. Shabiki mmoja wa timu ya Cote di'Voire alisema.
"Haikuwa rahisi, lakini Mwenyezi Mungu ametusaidia tukashinda mechi hii kwa magali mawili kwa moja".
Cote di'voire wamekuwa wakipewa nafasi ya kushinda kombe hilo katika mashindano manne yaliyopita, lakini wameshindwa kutimiza matarajio kila mara, wakipoteza katika mikwaju ya penati mwaka 2006 na 2012. hata hivyo, jana Jumanne walionyesha ubora unaohitajika na bingwa mtarajiwa - kwa kushinda mechi licha ya kucheza chini ya kiwango.
Nusura Togo ipate goli la mapema
Togo ingeongoza mchezo baada ya dakika mbili pale nahodha wake Emmanuel Adebayor, alipopata nafasi akitumia makosa ya Kolo Toure. Lakini badala ya kufunga goli, alijaribu kumpiga chenga mlinda mlango Boubacar Barry, ambaye alifanikiwa kuuondoa mpira kutoka kwa mshambuliaji huyo. Shabiki wa Togo naye anaamini timu yake ilifanya vya kutosha.
"Nadhani Togo imejaribu kucheza vizuri, tumefanya tulichopaswa kufanya, na mimi bado ni Mtogo na najivunia kuwa Mtogo".
Mzunguko wa pili wa mechi hizo unaanza leo Jumatano(23.01.2023) ambapo wenyeji Afrika Kusini wanacheza dhidi ya Angola na Morocco ikipambana na visiwa vya Cape Verde katika kundi A katika uwanja wa Moses Madhida mjini Durban. Timu zote katika kundi hilo ziko sawa zikiwa na pointi moja baada ya sare mbili tasa mjini Johannesburg Jumamosi wiki iliyopita.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Josephat Charo