1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFCON 2013 : Sare yatawala

20 Januari 2013

Hali ya baridi , mvua iliyonyesha kutwa nzima, soka lisilovutia na ukame wa magoli vilitawala katika siku ya kwanza ya ufunguzi wa fainali za kombe la mataifa ya Afrika Jumamosi (19.01.2013).

epa03544465 Artists perform during the opening ceremony of the African Cup of Nations soccer tournament at Soccer City in Johannesburg, South Africa, 19 January 2013. EPA/KIM LUDBROOK +++(c) dpa - Bildfunk+++
Michezo ya 29 ya kombe la Afrika yafunguliwaPicha: picture-alliance/dpa

Tamasha la soka la 29 katika bara la Afrika ambalo limekuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa, ambalo lilianza katika mazingira ya dhalili mwaka 1957 na kuwa tukio linaloleta mvuto duniani kote , lilianza kwa sare ya bila kufungana katika mchezo dhaifu baina ya wenyeji Afrika kusini Bafana Bafana na timu iliyopata nafasi kwa mara ya kwanza kuingia katika kinyang'anyiro hicho Cape Verde.

Mchezo huo wa kwanza wa ufunguzi ulifuatiwa na mchezo bora zaidi baina ya Morocco na Angola katika uwanja huo huo lakini pia ukamalizika kwa sare ya bila kufungana.

Timu ya taifa ya Cape VerdePicha: DW/Daniel Almeida

Kocha afurahi

Watu pekee ambao walionekana hasa kuridhika na siku ya kwanza ya fainali hizo, ambapo wengi watapendelea kuisahau haraka , ni kocha wa Cape Verde Lucio Antunes na kikosi chake.

Amefurahishwa na ukweli kwamba wamemaliza mchezo huo kwa imani ya kweli kwamba wanaweza kupata matokeo zaidi mazuri dhidi ya Morocco na Angola katika michezo yao iliyobaki katika kundi A na kuepuka kurejea nyumbani na mapema.

Mpambano kati ya Bafana Bafana na Cape VerdePicha: DW/Daniel Almeida

"Kwangu mimi ilikuwa kazi iliyokamilika," amesema Antunes. "Kikosi changu kilikuwa safi kabisa, tulifanya kazi tuliyokuja kuifanya na tumekamilisha matarajio yetu na sasa tunaweza kuelekeza mawazo yetu katika mchezo ujao dhidi ya Morocco.

"Nina furaha , wachezaji wanafuraha na benchi la ufundi limefurahi. Leo tumeipa hadhi nchi yetu. Ni nchi ndogo ya visiwa yenye wakaazi 500,000, lakini leo tumewafanya wajisikia fahari.

Afrika kusini yainamisha kichwa

Kocha wa Afrika kusini Gordon Igesund ana mtazamo mwingine kabisa baada ya pambano hilo lililodorora, lililojaa makosa kadha lililochezwa katika mazingira ya baridi kama wakati wa majira ya baridi huku mvua ikinyonyota katika uwanja huo.

Wachezaji wa Angola wakipambana na MoroccoPicha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo hali hiyo haikuweza kuzuwia matarumbeta ya Vuvuzela kuhanikiza uwanjani, kelele zake ambazo mara nyingine hazivumiliki zinatoa burudani kwa watazamaji katika michezo ya soka nchini Afrika kusini.

"si wachezaji wengi walikuwapo katika tamasha hili katika nusu ya kwanza , na hatukuwa katika hali nzuri katika kipindi cha pili," Igesund amewaambia waandishi habari baada ya kile ambacho kilikuwa mchezo mbovu wa ufunguzi wa mashindano haya ambao ulionekana moja kwa moja katika televisheni na mamilioni ya watu duniani kote.

Kocha wa Cape Verde Lucio AntunesPicha: DW/Nélio dos Santos

"Baadhi ya wachezaji walionekana kama wameganda wakati firimbi ya mwisho ilipolia , walionekana kuwa hawajiamini. pengine kwa baadhi yao tukio hilo lilikuwa kubwa mno, ameongeza kocha Igesund.

Leo (20.01,2013) ni zamu ya Ghana ikitiana kifuani na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, na baadaye Mali itaonyeshana kazi na Niger.

Mwandishi : Sekione Kitojo

Mhariri : Stumai George

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW