AFCON: Cameroon, Misri kuumana katika fainali
5 Februari 2017Mshindi wa kwanza wa taji hilo miaka 60 iliyopita Misri imekuwa mabingwa wa Afrika kwa mara saba lakini walikuwa wanarejea tena katika medani hiyo baada ya kukosa kushiriki katika fainali tatu za kombe la mataifa ya Afrika kutokana na machafuko ya kisiasa nchini humo.
Nyuma yao Cameroon , pamoja na Ghana , mataifa mengine yenye mafanikio makubwa katika historia ya mashindano hayo yana mataji manne kila moja , ambapo mara ya mwisho Cameroon kutoroka na taji hilo ilikuwa mwaka 2002.
Wakati Misri ikionekana kama timu inayofanya maajabu baada ya kurejea kwake katika fainali hizo za kombe la mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza tangu kulinyakua mara tatu mfululizo katika mwaka 2006, 2008 na 2010, Cameroon ilionekana kama timu ambayo haikuwa na nafasi.
Wachezaji waitupa mkono Cameroon
Kutokana na kuathirika na kukataa kwa wachezaji kadhaa muhimu kukubali kujiunga na kikosi hicho cha Simba wanyika cha kocha raia wa Ubelgiji Hugo Broos, badala yake timu hiyo ambayo inawakosa wachezaji nyota iliwaondoa mashindanoni wenyeji wa michuano hiyo Gabon na vikosi vilivyoonekana kusheheni nyota wa kandanda vya Senegal na Ghana na kuvuka hadi hapa ilipofikia.
Mchezo wa leo Jumapili (05.02.2017) katika uwanja wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 40,000 wa Stade de L'Amitie katika mji mkuu wa gabon Libreville utakaoanza saa mbili ya usiku kwa saa za Afrika mashariki utatanguliwa na sherehe za ufungaji mashindano hayo, ambazo zitaanza saa moja na nusu kabla.
Itakuwa ni mara ya tatu kwa timu hizo kukutana katika fainali -- Misri imeshinda kwa mikwaju ya penalti mjini Cairo mwaka 1986 na kushinda tena kwa bao 1-0 mjini Accra mwaka 2008.
Hiyo ilikuwa fainali ya mwisho ya cameroon , lakini wakati wakiwa na wachezaji kama samuel Eto'o na Rigobert Song, timu yao ya sasa haina majina makubwa ya nyota wa kandanda.
"Kwa wachezaji hawa vijana -- 14 kati ya 23 wanacheza kwa mara ya kwanza fainali za kombe la mataifa ya Afrika --- inawezekana kuwa ni fursa yao adimu katika maisha yao ya kucheza soka kushinda taji hilo," Broos alisema.
Akizungumza na waandishi habari siku ya Jumamosi, nahodha Benjamin Muokandjo aliongeza: "Ni dhahiri kwamba wakati ukiifika katika kiwango hiki unataka kushinda lakini nafikiri ukiangalia njia tuliyopitia tayari tumefanya vizuri.
"Sifikiri mtu yeyote hapa angeweza kuagulia kwa kucheza kamari senti yake ya mwisho kwetu kabla ya hapa na hii ni aibu kubwa kwao."
Misri imekuwa imara lakini bila ya kucheza kwa ustadi wa hali ya juu katika mbio sake kwenda katika fainali, goli pekee walilofungwa limekuja katika awamu ya nusu fainali dhidi ya burkina Faso.
Mlinda mlango mkongwe
Baada ya kutoka sare katika mchezo huo kwa bao 1-1,Misri walishinda kwa mikwaju ya penalti , mlinda mlango mwenye umri wa miaka 44 Essam El-Hadary akiokoa mikwaju miwili na kuwachukua Mafarao hao kwenda katika fainali na kuweka matumaini yake hai ya kulinyakua kombe hilo kwa mara ya tano katika kipindi chake akiwa mchezaji.
Kama Broos akiwa na Cameroon , Hector Cuper amefanya kazi nzuri sana katika kufufua matumaini ya wamisri, ambao kikosi chao kina wachezaji wanne tu walioshiriki katika ushindi wao wa fainali za mwaka 2010 wakiwa ni El-Hadary , Ahmed Fathy, Mohammed Abdel-Shafi na wingi wa klabu ya Hull City Ahmed Elmohamady.
"Misri haitakuwa tofauti na vile tulivyoiona hadi sasa, iwapo watu wanapenda hivyo ama la, iwapo hiyo ina maana tutashambulia ama la," Cuper alisema siku ya Jumamosi.
Wakati wake akiwa mchezaji Cuper alishuhudia nyakati za kukatisha tamaa nyingi katika fainali, mojawapo katika misimu mfululizo katika kombe la mabingwa wa Ulaya Champions League akiwa na valencia mwaka 2000 na 2001.
Raia huyo wa Argentina ahkulienda swali jana Jumamosi juu ya idadi ya fainali alizoshiriki na kushindwa, lakini anaweza kupata faraja kutokana na rekodi ya Misri katika fainali -- wameshinda mataji mara saba kati ya mara nane walizofikia katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika.
Majeruhi wamekuwa wakiongezeka katika kikosi hicho, hata hivyo, na kuna shaka kuhusiana na kushiriki mlinzi wa kati Ahmed Hegazy. Washambuliaji Ahmed Hassan na Marwan Mohsen wako nje na Mohammed Elneny kutoka Arsenal ana maumivu ya paja.
"Tutasubiri hadi dakika za mwisho kuona vipi wachzaji wana jisikia . Wamechoka sana , lakini fainali ni tofauti na michezo mingine na kuna idadi kubwa ya mambo katika mchezo," ameongeza Cuper.
Siku ya Jumamosi (04.02.2017) Burkina Faso ilijihakikishia tuzo ya kujifariji ya nafasi ya tatu baada ya kuizaba Ghana kwa bao 1-0 mjini Port-Gentil kwa goli la Alain Traore la mkwaju wa adhabu ya mbali.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Sudi Mnette