1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFCON: Cameroon yaanza vyema; Ghana yakabwa shati na Benin

Sylvia Mwehozi
26 Juni 2019

Mabingwa mara tano wa kombe la mataifa ya Afrika Cameroon wameanza vyema kampeni yao katika michuano ya AFCON inayoendelea Misri kwa kuwachapa Guinea-Bissau. Ghana ilikabwa shati na Benin baada ya kutoka sare. 

Fußball Africa Cup of Nations 2019 Kamerun - Guinea-Bissau
Picha: picture-alliance/Newscom/U. Pedersen

Magoli mawili ndani ya dakika tatu za kipindi cha pili yalitosha kuipatia ushindi Cameroon dhidi ya Guinea- Bissau. Guinea-Bissau ambayo inashiriki michuano hiyo kwa mara ya pili, walionyesha kandanda safi na kulinda lango lake hadi kipindi cha mapumziko. Christian Bassogog wa Cameroon alipoteza nafasi nyingi kabla ya hapo baadae kumpatia pasi nzuri Joyskim Dawa lakini mlinda mlango wa Guinea, Jonas Mendes akaokoa mpira wa kichwa. Soma zaidi ...

Guinea wakati fulani nao walijaribu bahati yao kwa kuchungulia lango la Cameroon kutokea mbali lakini bahati haikuwa upande wao. Dakika ya 66 ya kipindi cha pili Yaya Banana aliwaamsha mashabiki wa Cameroon baada ya kufunga bao safi la kichwa lililotokana na mpira wa kona. Dakika tatu baadae, Stephane Bahoken aliyeingia kutoka benchi alipachika bao la pili.

Cameroon sasa wamejihakikishia njia kuelekea kampeni ya kutetea ubingwa wa michuano hiyo. Nao mabingwa mara nne wa kombe la Afrika Ghana "The Black star" walishindwa kutamba mbele ya Benin. Mshambuliaji wa zamani wa Dynamo Dresden Michael Pote aliwapatia Benin goli la mapema katika dakika ya pili ya kipindi cha kwanza. Mashambulizi ya Andre Ayew yaliipatia Ghana bao la kusawazisha dakika saba baadae.

Michael Pote wa Benin akifurahia goli la kwanza dhidi ya GhanaPicha: picture-alliance/U. Pedersen

Dakika chache kabla ya mapumziko mchezaji wa Hoffenheim Kasim Adams alitoa pasi nzuri kwa Jordan Ayew aliyepachika bao zuri lisiloweza kuzuilika na kuifanya Ghana kuongoza wakati ikienda mapumziko. Benin ambao hawajashiriki michuano hiyo tangu mwaka 2010, walirejea na kasi kipindi cha pili na dakika ya 63 ya kipindi cha pili Pote kwa mara nyingine aliipatia timu yake bao la pili na la kusawazisha na kufanya ubao wa matokeo kusoma 2-2. Ingawa Benin haikushinda lakini sare hiyo imeiweka katika nafasi nzuri ya michuano ya Afcon.

Jioni hii wawakilishi pekee wa Afrika Mashariki ambao wameanza vyema kwa kupata ushindi, Uganda wataumana na Zimbabwe, wakati Nigeria ikikutana na Guinea. Uganda inaongoza kundi A ikiwa na pointi tatu na Zimbabwe iliyo kwenye kundi hilo iko nafasi ya tatu. Nigeria wanaongoza kundi B na Guinea wako nafasi ya pili kwenye kundi hilo hilo. Baadae pia Misri itakipiga na Congo huku Madagscar wakiwakaribisha Burundi.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW