1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFCON itaiathiri vipi ligi kuu ya Bundesliga?

27 Desemba 2023

Wakati Kombe la Mataifa ya Afrika litakapoanza Januari, vilabu kadhaa vya ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga vitalazimika kucheza bila ya wachezaji wake nyota.

Leverkusen
Wachezaji wa Bundesliga ambao huenda wakajumuishwa katika vikosi timu ya taifa, Nathan Tella, Victor Boniface, Edmond Tapsoba.Picha: Chai v.d. Laage/IMAGO

Wachezaji 24 wa Bundesliga watajumuishwa katika vikosi vya muda vya nchi zao kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2023 nchini Ivory Coast kuanzia Januari 13 hadi Februari 11, 2024, timu kadhaa kuu za Ujerumani zitakabiliwa na mwezi mmoja bila wachezaji wao muhimu.

Soma pia:AFCON yaikosesha usingizi Bayer Leverkusen

Ingawa vikosi vya mwisho vya AFCON vya kati ya wachezaji 24-27 havijathibitishwa hadi Januari 3, hakuna uhakika kwamba wachezaji wote 24 watasafiri katika mataifa yao,  lakini idadi ya mwisho bado inaweza kuwa kubwa kuliko wachezaji 11 wa Bundesliga walioshiriki AFCON mwaka 2022 nchini Cameroon.

Sambamba na michuano ya AFCON, wachezaji wengine wanane wa Bundesliga kutoka mataifa ya Japan na Korea Kusini pia wanaweza kukosekana watakaposhiriki Kombe la Asia nchini Qatar kuanzia Januari 12 hadi Februari 10.

Vinara wa Bundesliga, Bayer Leverkusen wanatarajiwa kuathirika zaidi na Kombe la Mataifa ya Afrika, kwa kuwakosa wachezaji watano ikiwa idadi kubwa ikilinganishwa na klabu nyengine.

Soma pia: Wenyeji wa AFCON Ivory Coast wapangwa kundi moja na Nigeria

Miongoni mwao ni Victor Boniface wa Nigeria, Edmond Tapsoba kwa Burkina Faso, Odilon Koussounou wa timu mwenyeji wa AFCON Ivory Coast na Amine Adli wa Morocco wote wana uwezekano wa kujumuishwa katika vikosi vya mwisho vya nchi zao, huku chipukizi Nathan Tella kutoka Nigeria pia akiwa na nafasi.

Mshambuliaji wa Nigeria Boniface amekuwa na jukumu muhimu katika mwanzo mzuri wa Leverkusen  msimu huu akiwa na jumla ya mabao 16 katika mashindano yote hadi sasa. Katika safu ya ulinzi, Tapsoba na Koussouno wamekuwa imara katika safu ya ulinzi ambayo imeruhusu mabao 12 pekee msimu huu.

Soma pia:Leverkusen yaweka rekodi ya mwanzo bora wa msimu

Leverkusen imejipanga?

Kocha wa Leverkusen Xabi Alonso, akijaribu kutoa maelezo kwa wachezaji wake katika mechi ya Bundesliga.Picha: Helge Prang/Getty Images

Safari ya ugenini kuelekea RB Leipzig mnamo Januari 20 itakuwa changamoto ya kwanza kwa kocha Xavi Alonso lakini anaweza kuwa na matumaini kwamba mchezaji mmoja au wawili watarejea kabla ya robo fainali ya Kombe la Ujerumani dhidi ya Stuttgart mnamo Februari 6.

Macho yote yataelekezwa katika mechi ya ugenini dhidi ya Bayern Munich mnamo Februari 10  siku moja kabla ya fainali ya AFCON.

Mnamo Januari 2022, Leverkusen haikupata tabu sana kwa kukosekana kwa Tapsoba na Koussouno,walipokwenda kuwakilisha mataifa yao kwani Leverkusen walitoka sare ya 2-2 na Union Berlin kabla ya kuilaza Borussia Mönchengladbach 2-1 Augsburg 5-1 na Borussia Dortmund 5- 2. Hata hivyo licha ya uwezekano wa kukosekana watano hao wakati huu, Leverkusen inaonekana kujiandaa vyema.

Katika kujaribu kuona vipi atafanikiwa kocha Alonso kwa hiari yake aliwaacha wachezaji wake watakao kwenda kuwakilisha mataifa yao kwenye AFCON, katika mechi dhidi ya Bochum lakini bado walipashinda 4-0 baada ya mshambuliaji wa Czech Patrik Schick kutia kimyani mabao matatu.

Vipi kuhusu klabu nyengine za Bundesliga?

Mshambuliaji wa VfB Stuttgart Serhou Guirassy amekuwa na mchango muhimu kwa timu yake.Picha: Wolfgang Frank/Eibner/IMAGO

Timu nyengine itakayopata pigo ni VfB Stuttgart, msambuliaji wao mwenye mabao 17 Serhou Guirassy huenda ataiongoza Guinea kwenye AFCON huku mshambuliaji Silas Mvumpa akitarajiwa kuungana na DR Congo.

Jambo linalotatiza zaidi timu ya Sebastian Hoeness ni Kombe la Asia, huku beki wa kushoto Hiroki Ito na kiungo Genki Haraguchi wakitarajia kuelekea Japan, na Jeong Woo-yeong huenda akachaguliwa katika kikosi cha Korea Kusini.

Eintracht Frankfurt huenda ikawakosa mshambuliaji wa Misri mwenye kasi Omar Marmoush na kiungo wa kati wa Algeria Fares Chaibi na Ellyes Shkhiri wa Tunisia ambao wamekuwa na mchango mkubwa msimu huu.

Kwa mabingwa watetezi Bayern Munich, Bouna Sarr hajafanikiwa kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Senegal, huku beki Noussair Mazraoui akipigania kuwa katika hali nzuri kimchezo atakapojumuika na Morocco na hakuna uhakika kama Eric-Maxim Choupo-Moting atajumishwa katika kikosi cha timu ya taifa baada ya kukosa mechi za Cameroon mwezi Oktoba.

Borussia Dortmund huenda ikawakosa Rami Bensebaini wa Algeria na mshambuliaji Sebastien Haller wa Ivory Coast. Werder Bremen itakuwa na matumaini kwamba Naby Keita anaweza kutumia muda wake na timu ya taifa ya Guinea kurejea katika fomu nzuri  baada ya kuwa nje ya kikosi cha Bremen kutokana na majeraha.

Hoffenheim huenda ikawakosa Kevin Akpoguma na Diadie Samassekou iwapo wataitwa kwa Nigeria na Mali mtawalia, pamoja na kiungo wa kati wa Morocco Aymen Barkok.

David Datro Fofana anaweza kuwa hasara kwa Union Berlin, kwani mshambuliaji huyo wa Ivory Coast anatoa mwanga wa matumaini kwa timu hiyo inayopambana dhidi ya kushuka daraja.

 

Mwandishi:Ford, Matthew

Tafsiri:Saumu Njama