1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFCON: Senegal yaicharaza Kameruni 3-1

20 Januari 2024

Kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Ivory Coast, Senegal iliicharaza Kameruni mabao 3-1, huku Cape Verde ikiibwaga Msumbiji 3-0 na Guinea-Bissau ikiipachika Gambia 1-0.

Soka | Afrika Cup | Kameruni vs Guinea
Mechi ya Kameruni na Guinea iliyochezwa tarehe 15 Januari 2024.Picha: Sydney Mahlangu/Sports Inc/picture alliance

Goli lililowekwa kimiani na Aguibou Camara kwenye kipindi cha pili ndilo lililoipa Guinea ushindi wa bao kwa bila dhidi ya Gambia.

Kiungo Camara, anayechezea soka la kulipwa nchini Ugiriki, alipokea pasi maridhawa kutoka kwa Morga Guilavogui na mkwaju wake wa moja kwa moja ukauinuwa uwanja uliofurika watu katika mji mkuu wa Ivory Coast, Yamoussoukro.

Matokeo haya sasa yanaiweka Guinea kwenye nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa na pointi nne, nyuma ya bingwa mtetezi Senegal kwa pointi mbili.

Soma zaidi: AFCON: Ghana walazimisha sare ya 2-2 na Misri

Sasa, Guinea inahitaji kutoka suluhu tu na Senegal katika mechi ya Jumanne ijayo, ili kujihakikishia kuwa miongoni mwa timu 16 zitakazovuuka duru hii ya mtoano. Gambia, ambayo haina pointi hata moja kwa sasa, itabahatisha kete yake ya mwisho mbele ya Kameruni siku hiyo hiyo ili kupata angalau nafasi ya tatu.

Senegal yairambisha mchanga Kameruni

Katika mechi nyengine ya Kundi C hapo jana, Senegal iliibwaga Kameruni 3-1. Ismaila Sarr anayechezea soka la kulipwa nchini Ufaransa ndiye aliyefungua lango katika dakika ya 16, huku Habib Diallo akipachika goli lake kwenye dakika ya 71.

Wachezaji wa Senegal wakishangiria ushindi.Picha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Katika dakika ya 83, Jean-Charles Castelletto aliipatia Kameruni bao la kufutia machozi, kabla ya Sadio Mane kupachika bao la tatu la Senegal kwenye dakika za nyongeza. 

 Kwa ushindi huo, Senegal inaongoza Kundi C ikiwa na pointi sita.

Mshambuliaji Ismaila Sarr alisema baada ya mchezo huo, kwamba alikumbuka kuwa mwaka 2017 walipoteza mchezo kwa Kameruni katika robo fainali, kwa hivyo sasa walipaswa kila wawezalo kuwazuwia kabla hawajafika mbali.

Cape Verde yakaribia kuifungisha virago Msumbiji

Katika mechi ya Kundi B, Cape Verde ilikuwa timu ya kwanza kufanikiwa kuingia kwenye timu 16 zinazosonga mbele kwenye duru ya mtoano kwa kuichabanga Msumbiji 3-0.

Mchezo wa Cape Verde na Msumbiji tarehe 19 Januari 2024.Picha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Bebe, ndiye aliyekuwa wa kwanza kuuona wavu wa Msumbiji katika dakika ya 32 kwa mkwaju wa moja kwa moja katika Uwanja wa Felix Houphet Boigny. 

Soma zaidi: Raundi ya pili ya mechi za makundi kuanza AFCON

Nahodha Ryan Mendes aliongeza goli la pili katika dakika ya 51 na bao la mwisho liliwekwa kimiani na Kevin Pina katika dakika ya 69. 

Ushindi huu mkubwa kabisa kwa Cape Verde umeipandisha hadi pointi sita kwa michezo miwili tu, na hivyo kuwa na uhakika kwenye Kundi B, baada ya kuichapa Ghana 2-1 kwenye mechi ya ufunguzi. 

Kwa upande wake, Msumbizi ambayo inashiriki michuano hii ya AFCON kwa mara ya tano, haijaweza hadi sasa kushinda mechi hata moja.

Tanzania yamfukuza kocha wa Taifa Stars

Hayo yakijiri, Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limemfuta kazi kocha wa kikosi chake kinachoshiriki michuano hiyo  ya Kombe la Afrika, Adel Amrouche, baada ya kupigwa marufuku na Shirikisho la Soka la Afrika, CAF, asishiriki mechi  nane na faini ya dola 10,000 za Kimarekani kwa tuhuma za kusema maneno mabaya dhidi ya Moroko.

Mechi ya Tazania na Moroko siku ya Jumatano (Januari 17, 2024.Picha: Sia Kambou/AFP

TFF imemteuwa hapo hapo Hemed Suleiman kuchukuwa nafasi ya Adel kwa muda wote michuano hiyo inapoendelea nchini Ivory Coast.

Soma zaidi: Moroko yaichabanga Tanzania 3-0 AFCON

CAF inadai kuwa Adel, raia wa Algeria, alisema maafisa wa Moroko ndani ya CAF wanaamua marefa hata kwenye mechi ambazo zinahusisha timu yao ya taifa.

Tanzania ilifungwa 3-0 na Moroko siku ya Jumatano na bado inapaswa kushuka dimbani kupambana na Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenye mechi za Kundi F.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW