1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AfD na mwanzo mpya wenye utata

24 Aprili 2017

Chama cha siasa kali za kizalendo nchini Ujerumani (AfD) kinataka kuendelea kuwa chochote ambacho wapigakura wanakitaka kiwe lakini kuelemea kwake mrengo mkali wa kulia kunaweza kukiweka hatarini zaidi.

Köln AfD Bundesparteitag Alice Weidel und Alexander Gauland
Picha: picture-alliance/dpa/R. Vennenbernd

"Kwa sasa AfD ni kama kwamba inaning'inia kama balbu la umeme katikati ya msitu, na hivyo linavutia kila aina ya viumbe," ndivyo mwanachama wa ngazi za kati wa AfD anavyokielezea chama chake kwa wapigakura walioegemea siasa kali za mrengo wa kulia.

Lakini kiongozi wa chama hicho, Frauke Petry, ameonesha kushindwa kuweza kuwavutia wapigakura kwenye jambo hilo. Badala ya kujifungia chenyewe kwenye duara la mrengo wa kulia, hivi punde chama hicho kimejichagulia uongozi wenye mchanganyiko wa kuogofya kuelekea uchaguzi mkuu wa Septemba; naye ni Alexander Gauland, mtu mzima wa miaka 76 na aliyekuwa afisa kwenye chama cha CDU cha Kansela Angela Merkel. 

Kwa ndani, anaweza kuonekana kama anakiongoza chama hicho cha mrengo wa kulia, lakini kiuhalisia Gauland anaonekana zaidi ana hamu ya kumshinikiza Kansela Merkel kukubaliana na fasili yake ya dhamira ya kihafidhina kwenye siasa, kwa namna ile ile anayotaka kukijenga chama chake cha AfD kama nguvu ya kisiasa ya muda mrefu.

Gauland atapiga kampeni akiwa jukwaa moja na nyota inayochipukia kisiasa ya AfD, Alice Wiedel, mwanamke wa miaka 38 na mshauri wa kibiashara anayeishi na mpenzi wake wa kike na mtoto mmoja. Mtu anaweza kujikuta anamtafuta kiongozi mwengine wa chama kinachofahamika kwa mitazamo yake dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, na asimuone.

AfD haitahimili siasa kali muda wote

AfD inaweza kuwa kweli imeamua hasa kukaa upande wa siasa kali za kulia, lakini hakuna anayeweza kukishutumu kwa kukosa mvuto.

Kiongozi mwenza wa AfD, Frauke Petry, ameangushwa kisiasa lakini anasalia madarakani kwa matumaini ya kuubadilisha muelekeo wa chama chake.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kilichomtokea shujaa wa kwanza wa AfD, Frauke Petry, ni kwamba wajumbe wapatao 600 wa chama hicho waliamua siku ya Jumamosi kumtia adabu kwa namna ambayo kamwe hakuwahi kuiwazia. Adabu kama hiyo ndiyo ambayo yeye mwenyewe Frauke alimtia mwasisi wa chama hicho, Bernd Lucke, aliyelazimika kuondoka baada ya kushindwa kukwepa fitina iliyopandikizwa na yeye Frauke.

Sasa matakwa ya Frauke kujenga ngome imara ya siasa za mrengo wa kulia hayakupata hata nafasi ya kujadiliwa ndani ya mkutano wa chama chake mwenyewe. Hapana shaka, hilo lilikuwa jambo la aibu sana kwake, maana kama alivyokuwa kwa mtangulizi wake aliyempindua, Bernd Lucke, naye pia alijidhani ana nguvu kubwa zaidi kuliko hali halisi ilivyo mbele ya wanachama wenzake.

Badala yake, aliyepigiwa makofi mengi ya hamasa alikuwa ni kiongozi mwenza wa AfD, Jörg Meuthen, aliyetoa wito wa "kuirejesha Ujerumani kwa Wajerumani wenyewe", maana akikaa kwenye ghorofa yake ya Stuttgart, huwa ni nadra kumuona Mjerumani hasa mitaani.

Ni hotuba hiyo iliyoshangiriwa kwa wingi ndiyo iliyoonesha hasa muelekeo wa chama kuelemea zaidi upande mkali wa kulia kuliko dhana ya uhafidhina wa kiliberali ambayo ilikuwapo kabla.

Lakini licha ya kuadhiriwa huko, Frauke Petry ameapa kubakia na wadhifa wake kama kiongozi mwenza wa chama, akiamini kwamba yumkini wakati fulani kabla ya uchaguzi mkuu wa hapo Septemba, wenzake kwenye uongozi wa juu watakubaliana na khofu zake kwamba kuzidi kujiegemeza kwenye siasa kali za mrengo wa kulia, kutakigharimu chama hicho, na pengine kuja kujikuta kwenye mahala ambapo hakiwezi tena kuwa hai kama taasisi ya kisiasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW English
Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW