1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AfD yaaendeleza mashambulizi dhidi ya Uislamu na wahamiaji

18 Septemba 2017

Chama cha AfD kimetaka hatua za kiusalama kuwekwa hususan kuwalenga wahamiaji. Pia kimeshikilia kuwa Uislamu hauendani na demokrasia. Kiongozi wake Alexander Gauland amesema hatakubali Ujerumani kuwa nchi ya Kiislamu

Deutschland AfD-Pressekonferenz mit Weidel und Gauland
Picha: Reuters/A. Schmidt

Chama chenye siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ujerumani AfD, kimeendeleza mashambulizi dhidi ya wahamiaji na Uislamu. Haya yanajiri wakati ambapo kura ya maoni ya hivi karibuni ikionesha kuwa chama hicho kimeimarika kuelekea katika uchaguzi mkuu. Chama cha Merkel kimepunguza kura.

Kupitia kiongozi wake Alexender Gauland, chama cha AfD kimetaka hatua madhubuti za kiusalama kuwekwa hususan kuwalenga wahamiaji, huku pia kikishikilia kuwa Uislamu hauendani na demokrasia. Kauli hiyo inayojiri wakati kampeni zikifika katika kilele chake wiki hii kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa Septemba 24.

Gauland: "Sitakubali Ujerumani kubadilishwa nchi ya Kiislamu"

Muonekano wa nje wa msikiti wa Merkez mjini DuisburgPicha: AP

Alexander Gauland ambaye amewaambia waandishi wa habari kuwa hawezi kuruhusu Ujerumani kubadilishwa kuwa taifa la Kiislamu ameongeza kuwa: "Haswa kwa sababu Uislamu pia  ni mafundisho ya kisiasa, mtu hawezi kuutizama tu katika msingi wa uhuru wa kuabudu. Kama mafundisho ya kisiasa, Uislamu hauendani na utaratibu wa sheria ya uhuru wa demokrasia. Kwa mantiki hiyo si sehemu ya Ujerumani"

Gauland na mgombea mwengine mkuu wa AfD Alice Weidel wamezusha  utata kabla ya uchaguzi wa Jumapili. Gauland ameshikilia kauli kuwa Ujerumani yapaswa kuwaonea fahari wakongwe  wa vita vikuu vya kwanza na pili vya dunia, naye Weidel mara kwa mara amemuajiri mhamiaji anayetafuta hifadhi bila ya kulipa ushuru, madai ambayo ameyakanusha.

Mabadiliko yanayopendekezwa na AfD

Chama cha AfD kinachojiita chama mbadala kwa Ujerumani, kinaelekea kuingia katika bunge kwa mara ya kwanza katika uchaguzi utakaofanyika Jumapili ijayo, huku kura ya maoni ikionesha kuwa chama hicho kinaungwa mkono na watu kati ya asilimia10 hadi asilimia 12, tofauti na nafasi yake ya awali ambapo kilikuwa na asilimia 10. Gauland amesema miongoni mwa mabadiliko wanayoyapendekeza ni pamoja na kupiga marufuku mavazi yote yanayofunika mwili mzima na vitambaa vya kichwani vinavyofunika pia nyuso kwa wanawake walioajiriwa serikalini, wito wa adhana inayowaita Waislamu kuswali, kupigwa marufuku kwa minara ya msikiti kando na kutaka iwe lazima kwa misikiti yote kusajiliwa.

Wahamiaji wakisubiri kusajiliwa katika kituo cha kuomba uhifadhi mjini Erding karibu na MunichPicha: Getty Images/AFP/C. Stache

Kwa mujibu wa kura hiyo ya maoni ya Sonntagstrend iliyofanywa na taasisi ya Emnid, Chama cha Kansela Angela Merkel CDU kilishuka ngazi kwa kupata 36%. Chama mshirika wa CDU cha SPD kinachoongozwa na Martin Schulz kilishuka pia kwa kupata asilimia 23. Kuimarika kwa AfD kunakiweka katika uwezekano wa kuwa chama cha tatu kwa ukubwa na ushawishi bungeni kando na uwezekano wa kuongoza upinzani.

Kuvuruga mikutano ya Merkel

Wafuasi wa AfD wamekuwa wakivuruga mikutano ya Merkel kwa kupiga kelele na kupuliza firimbi ili kumzamisha kisiasa.

Lakini kiongozi wa chama cha mrengo wa kushoto Die Linke, Katja Kipping amewataka wapiga kura kutoruhusu AfD kuwa chama cha tatu kwa ukubwa cha upinzani. Akizungumza na shirika la habari la hapa Ujerumani DPA, Kipping amewarai wapiga kura kwa kusema kuwa wanaotaka kumzuia kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia ni lazima wategemee mrengo wa kushoto.

Mwandishi: John Juma/AFPE/APE/DPAE

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW