Afghanista haitawaachia huru wafungwa ''hatari'' wa Taliban
8 Julai 2020Chini ya masharti ya mkataba huo kati ya Marekani na Taliban, Serikali ya Afghanistan iliahidi kuwaachia huru takribani wanachama elfu 5 wa Taliban katika hatua ya kubadilishana wafungwa ambayo ingeshuhudia kundi hilo la waasi kuwaachia huru takriban mateka elfu 1 wa vikosi vya usalama vya Afghanistan.
Lakini msemaji wa baraza la usalama wa taifa NSC Javid Faisal ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wafungwa 600 ambao kundi la Taliban limetaka waachiwe huru walikuwa na ''kesi nzito za uhalifu'' dhidi yao. Wafungwa hao wanahusisha watu walioshtakiwa kwa mauaji, wizi wa kimabavu katika barabara kuu na pia ulawiti pamoja na mamia ya wapiganaji wa kigeni, haya ikiwa ni kwa mujibu wa afisa mwengine ambaye hakutaka kutambulishwa.
Afisa huyo aliongeza kuwa watu hao ni hatari sana kuachiwa huru.
Siku ya Jumatano, kundi la Taliban liliishtumu serikali ya Afghanistan kwa kutunga kesi za uhalifu dhidi ya wafungwa hao. Msemaji wa kundi hilo Zabihullah Mujahid, amesema kuwa iwapo serikali hiyo itaendelea kusababisha matatizo zaidi kuhusiana na suala hilo, itaonyesha kuwa hawataki kutatua masuala hayo kwa njia nzuri.
Lakini Faisal, amesisitiza kuwa serikali imejitolea katika mazungumzo hayo. Ameongeza kuwa wako tayari kwa amani na kwamba watawaachia huru wafungwa waliosalia kulingana na makubaliano hayo na wala sio mamia ya wafungwa hao walio na kesi kubwa za uhalifu katika mahakama.
Pande zote mbili zimeahidi kufanya mazungumzo ya moja kwa moja yanayolenga kumaliza mzozo wa miongo kadhaa nchini Afghanistan baada ya kukamilishwa kwa shughuli hiyo ya kubadilishana wafungwa.Tayari serikali imewaachia huru zaidi ya wapiganaji elfu 4 wa kundi la Taliban huku kundi hilo la waasi likiwa limekamilisha thuluthi mbili ya shughuli hiyo ya kuwaachia huru mateka wake.
Mapema wiki hii, msemaji wa rais Ashraf Ghani Sediq Sediqqi alisema kuwa uamuzi ni wa mamlaka ya nchi hiyo kuamua wanaotaka kuwaachia huru na wala sio kundi la Taliban kuiambia kuhusu wafungwa wanaopaswa kuachiwa huru.