Afghanistan: Idadi ya watu wailouawa mjini Kabul yaongezeka
29 Julai 2019Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani nchini Afghanistan Nasrat Rahimi amesema walinda usalama walikabilianana washambuliaji hao ndani ya jengo ambalo ni makao makuu ya chama cha Green Trend kwa saa kadhaa. Mauaji hayo yamefanyika licha ya juhudi kubwa za jumuiya ya kimataifa za kujaribu kuleta amani katika nchi hiyo iliyomo vitani kwa muda wa miaka mingi.
Wizara ya mambo ya ndani imesema watu wengine 50 walijeruhiwa katika hujuma hiyo iliyomlenga makamu wa Rais wa Afghanistan Amrullah Saleh ambaye pia ni mkuu wa zamani wa shirika la ujasusi. Takriban watu wapatao 150 waliokuwa ndani ya jengo hilo walikolewa.
Wizara hiyo imearifu kuwa washambuliaji kadhaa waliuliwa na vikosi vya usalama. Mpaka sasa hakuna kundi au mtu aliyedai kuhusika na mashambulio hayo lakini makundi mawawili ya Taliban na Kundi linalojiita Dola la Kiislmu (IS) yamehusika na mashambulio makubwa katika mji wa Kabul.
Akiwahutubia wafuasi katika mkutano mkubwa mjini Kabul, Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani alielezea kwamba lengo lake kuu ni kuboresha usalama, kutekeleza sheria, kuboresha miundombinu ya usafirishajim na hospitali iwapo atachaguliwa tena kutumikia miaka mingine mitano.
Wanasiasa kadhaa akiwemo mbabe wa kivita wa zamani Gulbuddin Hekmatyar, wamejitokeza kumpinga Rais Ghani ambaye aliunda serikali ya umoja na mpinzani wake mkuu Abdullah Abdullah baada ya uchaguzi wa mwaka 2014 uliokumbwa na shutuma za udanganyifu.
Kadhia hiyo ilitokea katika siku ya kwanza ya kampeni za uchaguzi wa Rais ambao tayari umeshaahirishwa mara mbili mnamo mwaka huu. Matayarisho na usalama wa uchaguzi huo yanatarjiwa kuwa changamoto kubwa kwa serikali ya Rais Ashraf Ghani aliyeingia madarakani mnamo mwaka 2014. Wapiga kura nchini Afghanistan wana mashaka iwapo uchaguzi utakuwa huru na iwapo utafanyika kwa haki.
Vyanzo:/APE/Permalink https://p.dw.com/p/3MsMk