Afghanistan na Pakistan zafanya mazungumzo ya amani
8 Aprili 2026
China imesema Afghanistan na Pakistan zimefanya mazungumzo na kukubaliana kusaka suluhu ya mgogoro uliozuka kati yao mwezi Oktoba mwaka jana.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China Mao Ning amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya mazungumzo ya amani yaliyofanyika huko Urumqi nchini China na kwamba pande zote mbili zimeafikiana kutouchochea au kuuzidisha mzozo huo.
Mao ameongeza kuwa China itaendelea kuwasiliana na nchi hizo mbili ili kuwezesha mazingira ya kuendelea na mazungumzo. Mzozo uliozuka mwaka jana kati ya Afghanistan na Pakistan ulisababisha maafa makubwa ikiwa ni pamoja na mamia ya watu kuuawa.
Pakistan yasema operesheni ya kijeshi itaendelea
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan Amir Khan Muttaqi alikutana na balozi wa China nchini Afghanistan Jumanne na kuishukuru Beijing kwa kupanga na kuandaa mazungumzo hayo.
Muttaqi pia aliishukuru Saudi Arabia, Uturuki, Qatar na Falme za Kiarabu kwa juhudi zao za upatanishi.
"Kwa kuzingatia kwamba mazungumzo muhimu yamefanyika hadi sasa, Muttaqi alielezea matumaini kwamba tafsiri ndogo hazitazuia maendeleo ya mazungumzo," Wizara ya Mambo ya Nje ilichapisha kwenye X.
Maafisa wa Pakistan hawakujibu moja kwa moja ombi la kutoa kauli kuhusu mazungumzo hayo. Siku ya Jumanne, Mkuu wa Jeshi la Pakistani Asim Munir alikutana na makamanda wakuu wa jeshi.
Wakuu wa mkutano waliapa kuendelea na operesheni yao ya kijeshi hadi "maficho ya magaidi yatapoangamizwa na matumizi ya ardhi ya Afghanistan dhidi ya Pakistan yatakapokomeshwa kabisa."
Mgogoro kati ya Pakistan na Afghanistan waongezeka
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Afghanistan inakadiria kwamba mzozo huo umesababisha jumla ya watu 94,000 kuhama makwao, huku watu wapatao 100,000 katika maeneo mawili ya Afghanistan karibu na mpaka yakikatizwa kabisa tangu Februari kutokana na mapigano.
Mapigano ya hivi karibuni yanazingatiwa kuwa makali zaidi kati ya nchi hizo mbili, ingawa mvutano umekuwa ukiibuka tangu Taliban waliporejea madarakani mwaka wa 2021 nchini Afghanistan. Kundi hilo lina uhusiano na, lakini katika njia tofauti na kundi la wanamgambo wa Taliban wa Pakistan, linalojulikana kama Tehrik-e-Taliban Pakistan au TTP.