1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Afghanistan: Shule za sekondari zafunguliwa bila wasichana

Daniel Gakuba
18 Septemba 2021

Shule za sekondari zimefungua milango tena nchini Afghanistan, lakini kwa wavulana tu, bila wasichana. Watawala wapya wa nchi hiyo, Taliban wameamuru wavulana na walimu wa kiume tu ndio warejee madarasani.

Pressebild Maarif Schools of Afghanistan
Picha: Maarif Schools of Afghanistan

Walipoingia madarakani baada ya kuitimua serikali iliyoungwa mkono  na Marekani mwezi uliopita, Taliban walikuwa wameahidi kuachana na sera za mrengo mkali wa Kiislamu kama ule walioushikilia miaka ya 1990. Wakati huo kwa sehemu kubwa, wanawake na wasichana walitengwa katika vyuo vya elimu na kwenye nafasi za ajira.

Kabla ya kuanza upya kwa shughuli za masomo Jumamosi (18.09.2021), wizara ya elimu ilitoa tangazo, ambalo liliwataka ''walimu wote wa kiume na wanafunzi wavulana'' wanapaswa kuripoti katika taasisi za elimu.

Tangu mwaka 2001, wasichana wengi wamesajiliwa shuleni AfghanistanPicha: DW/A. Akramy

Tangazo hilo lililochapishwa jana halikusema chochote kuhusu walimu wanawake na wanafunzi wa kike.

Nchini Afghanistan, ni kawaida kuwatenganisha kwa msingi wa jinsia yao, wanafunzi wa sekondari ambao huwa ni kuanzia umri wa miaka 13 hadi 18. Shule hizo zilikumbwa na changamoto ya kufungwa mara kwa mara wakati wa janga la Covid-19, na tangu Taliban walipochukua hatamu za uongozi, shule hizo zilikuwa zimefungwa kabisa.

Pigo kwa hatua iliyopigwa kwa miaka 20

Elimu ya wasichana nchini Afghanistan ilipiga hatua kubwa tangu Marekani na washirika wake walipoivamia Afghanistan mwaka 2001, ambapo idadi ya wasichana walioko shuleni iliongezeka kwa asilimia 30. Hata hivyo, maendeleo makubwa yalijikita katika maeneo ya mijini.

Umoja wa Mataifa umesema unao ''wasiwasi mkubwa'' juu ya hatima ya elimu ya wasichana nchini Afghanistan.

Ingawa Taliban wameahidi kubadili misimamo yao mikali, bado hatma ya elimu ya wasichana iko mashakaniPicha: DW/F. Zahi

''Ni jambo lenye umuhimu mkubwa kabisa kwamba wasichana wote, wakiwemo wale wenye umri mkubwa, wanaruhusiwa kuendelea na elimu yao bila kucheleweshwa zaidi. Ili hilo kufanikiwa, tunataka walimu wa kike warejee kazini,'' limesema shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Watoto, UNICEF.

Elimu ya msingi rukhsa kwa wasichana

Tayari shule za msingi zimekwishafunguliwa, wavulana na wasichana waliruhusiwa kuhudhuria lakini katika madarasa tofauti. Kwenye ndazi hiyo, baadhi ya walimu wa kike wameruhusiwa kurudi kazini.

Taliban vile vile wamewaruhusu wanawake kusoma katika vyuo vikuu vinavyomilikiwa na watu binafsi, wakitakiwa kuheshimu masharti makali ya uvaaji wa nguo, na namna wanavyotembea.

Baraza la mawaziri la Taliban ni wanaume watupuPicha: Government of Afghanistan

Katika kile kilichochukuliwa kama ishara ya wazi kuwa Taliban hawajalegeza msimamo wao mkali, wameonekana kuifuta wizara ya masuala ya wanawake, na katika nafasi yake wameweka taasisi ambayo wakati wa utawala wa kwanza wa Taliban, ilikosolewa sana kwa kushinikiza utekelezwaji wa sheria kali za Kiislamu.     

Wizara ya maadili katika nafasi ya wizara ya wanawake     

Wafanyakazi walionekana mjini Kabul siku ya Ijumaa, wakiweka bango la Wizara ya Maadili na Kuzuia utovu wa nidhamu, katika jengo ambalo siku za nyuma lilikuwa la ofisi za Wizara ya Masuala ya Wanawake.

Picha za vidio zilizowekwa mitandaoni ziliwaonyesha wanawake waliokuwa wakiandamana baada ya kupoteza kazi zao. Hakuna tangazo lolote rasmi kutoka utawala wa Taliban kuhusiana na hatua hizo mpya.

Ingawa bado walikabiliwa na changamoto, wanawake nchini Afghanistan walipiga hatua kubwa mnamo miaka 20 iliyopita, baadhi yao wakifanikiwa kuajiriwa kama majaji, marubani na maafisa wa polisi.

Vile vile mamia kwa maelfu wameingia katika nafasi nyingine za ajira, suala la lazima ikizingatiwa kuwa wengi ni wajane kutokana na vita na machafuko vya muda mrefu.

Taliban hawaonyeshi dhamira ya kuendeleza haki hizo kwa wanawake hao. Hakuna mwanamke hata mmoja aliyeteuliwa katika baraza lao la mawaziri, na maelfu wamezuiliwa kuripoti tena kazini kwao.

 

Vyanzo: afpe, ape