1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan: Wataliban wafurushwa kutoka mji wa Ghazni

10 Agosti 2018

Wanajeshi wa Afghanistan wanaendesha operesheni ya kuwatafuta wapiganaji wa Taliban baada ya kutokea shambulio kubwa katika jiji la kusini mashariki ya mkoa wa Ghazni.

Afghanistan Angriffe in Ghasni
Picha: Getty Images/AFP/Z. Hashimi

Majeshi maalum ya Afghanistan yalipelekwa Ghazni baada ya jaribio la hivi karibuni la wapiganaji waTaliban la kutata kuliteka eneo moja katikati ya mji. Mashambulio hayo yanafanyika wakati ambapo waasi wanakabiliwa na shinikizo la kuwataka wakubali kushiriki katika mazungumzo ya amani.

Wapiganaji wa Taliban waliokuwa na silaha nzito walishambulia mji mkuu wa Ghazni uliko katikati ya Afghanistan siku ya Ijumaa. Walichoma vizuizi kadhaa vya polisi na kwa muda walidhibiti sehemu za kati za mji huo kabla ya kufurushwa na majeshi ya nchi hiyo yakisaidiwa na vikosi vya Marekani. Wapiganaji wa kundi la kigaidi laTaliban walifanya mashambulizi kwa saa kadhaa katika jitihada za kuuchukua mji mkuu wa mkoa wa Ghazni nchini Afghanistan.

Wapiganaji hao walijificha kwenye nyumba za watu kabla ya kuingia kwenye barabara za mji huo  na kuanzisha mapigano yaliyochukua siku nzima huku majeshi Afghanisatan yakisaidiwa na vikosi vya Marekani yaking'ang'ana kuwarudisha nyuma wapiganaji hao wa Taliban.

Moshi mnene katika mji wa Ghazni baada ya Taliban kuushambulia mji huoPicha: Getty Images/AFP/AFPTV

Polisi wa Afghanistan wapatao 14 wameuwawa katika shambulio lililotokea katika mji mkuu wa jimbo la Ghazni. walijeruhiwa. Mkuu wa polisi wa mkoa huo Farid Ahmad Mashal ameliambia shirika la habari la AFP kwamba polisi wengine 20 walijeruhiwa kwenye shambulizi hilo. Mkuu huyo wa polisi ameeleza kwamba mashambulizi yalianza karibu saa nane alfajiri usiku wa kuamkia Ijumaa na kulikuwa na majibizano ya risasi pamoja na maduka kadhaa kuchomwa moto katika eno la makazi ya watu katika mji huo.

Mapigano yaliendelea kwa siku nzima ambako wakati wa mchana wapiganaji wa Taliban walilichoma moto jengo lenye stesheni ya televisheni.  Kulingana na mbunge Ali Akbar Kasemi, kutoka  jijini humo wapiganaji hao wa Taliban pia waliharibu mnara wa mawasiliano ulioko nje ya jiji na kusababisha kukatika mawasiliano yote ya simu za mkononi na zile za mezani katika mji wa Ghazni.

Wanajeshi wa nchi kavu wa Afghanistan waliomba usaidizi wa kikosi cha wanaanga ili kupambana na mashambulizi hayo. Ndege za kivita za Marekani. na ndege zinazoruka bila rubani ziliviongezea nguvu vikosi vya serika. Lakini kutokana na kuwa wapiganaji wa Taliban waliokuwa wamejificha katika maeneo ya makazi, haijulikani iwapo vikosi vya serikali vimepata udhibiti kamili wa mji huo.

Rais wa Afghanistan Ashraf GhaniPicha: Getty Images/AFP/W. Kohsar

Naibu msemaji wa wizara ya Mambo ya Ndani Nasrat Rahimi, amesema  Wataliban walizitumia nyumba za watu kujificha, na kuvifanya vikosi vya usalama vikabiliwe na hali ngumu kuweza kuwakabili wapiganaji hao. Wakazi wa jiji la Ghazni waliripoti juu ya milio ya bunduki huku wakiwa na hofu ya usalama wao iwapo watajulikana.

Mashambulizi katika jiji la Ghazni lililo katika barabara kuu inayogawanya mji mkuu wa Kabul na kusini mwa Afghanistan iyalilenga  kuonyesha nguvu za Wataliban, na kuonyesha jinsi hali ya usalama ilivyo tete miezi mitatu kabla ya uchaguzi wa bunge kufanyika hapo mwezi Oktoba.

Wizara ya ulinzi mjini Kabul imesema wapiganaji wa Taliban wamerejeshwa nyuma lakini bado baadhi yao wapo katika eneo moja la mji huo na wamejificha kwenye nyumba za raia ambako wanaendelea kuwafyatulia risasi askari wa serikali wanaowasaka ili kulidhibiti eneo hilo kwa ajili ya kurejesha hali ya usalama.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/APE/RTRE

Mhariri:Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW