1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu saba wafariki katika mtafaruku nje ya uwanja wa Kabul

Daniel Gakuba
22 Agosti 2021

Wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema watu saba wamekufa katika mkanyagano nje ya uwanja wa Kabul, wakati Marekani ikitafakari njia nyingine za kuwaondoa watu kutoka Afghanistan na kuwahamishia katika nchi nyingine.

Afghanistan Kabul Airport | Flüchtlinge warten auf Ausreise
Picha: Sayed Khodaiberdi Sadat/AA/picture alliance

Taarifa ya wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema Jumapili kuwa raia saba wa Afghanistan wameuawa katika mkanyagano uliotokea nje ya uwanja wa ndege wa mjini Kabul, wakati umati wa watu waliojawa na taharuki ukijaribu kupanda ndege zinazowahamishia watu mahali salama.

''Hali halisi uwanjani hapo ni ya changamoto kubwa lakini tunafanya kila linalowezekana kuidhibiti kwa njia salama, imesema wizara hiyo katika taarifa yake.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya haulitambui kundi la Taliban

Wapiganaji wa Taliban wamezusha vurugu pale walipofyatua risasi angani kuwatawanya watu waliokuwa wakijaribu kuingia katika uwanja wa ndege.

Katika taarifa yake, wizara ya ulinzi ya Uingereza imetuma salamu za rambirambi kwa familia za Waafghanistan zilizopoteza wapendwa wao.

Mwanamke wa kiafghanistan aliyejifungua ndani ya ndege akipelekwa katika kituo cha afyaPicha: US AIR FORCE/AFP

Mama wa Kiafghani ajifungua ndani ya ndege

Wakati uhamishaji huu wa watu wa kiwango cha kihistoria ukiendelea, wizara ya ulinzi ya Marekani imearifu kupitia mtandao wa twitter, kwamba mwanamke mmoja raia wa Afghanistan amejifungua akiwa ndani ya ndege ya jeshi la Marekani, muda mfupi kabla ya ndege hiyo kutua katika uwanja wa ndege wa Ramstein nchini Ujerumani.

Soma zaidi: Zoezi la kuwahamisha watu kutoka Afghanistan bado ni gumu

Rubani wa ndege hiyo alilazimika kuishusha hadi mwinuko mdogo kutoka usawa wa bahari, kuboresha mgandamizo wa hewa ndani ya ndege, hali iliyosaidia kunusuru maisha ya mama huyo na mtoto wake.

Jeshi la Marekani limesema kuwa baada ya ndege kutua, maafisa wa afya walimhamishia mara moja mama huyo na mtoto mchanga katika kituo cha afya, na kuongeza kuwa wote wawili walikuwa wenye afya nzuri.

Taliban wakiri kudhibiti vurugu uwanjani ni kazi ngumu

Afisa mmoja wa kundi la Taliban linaloudhibiti mji wa Kabul ameliambia shirika la habari la Reuters  kwamba wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kusimamia utulivu kwenye uwanja wa ndege wa Kabul.

Taliban wamekiri kuwa kudhibiti usalama Kabul ni shughuli pevuPicha: Rahmat Gul/AP/picture alliance

''Tunahitaji uwazi katika mpango wa vikosi vya kigeni kuondoka Afghanistan'', amesema afisa huyo.

Siku ya Jumamosi watu 150 walikamatwa na kuwekwa kizuizini kwa muda, saba miongoni mwao wakiwa raia wa India.

Wataliban mara hii wameahidi kuendesha utawala wa sera za wastani, ikilinganishwa na zile za kikatili zilizoshuhudiwa wakati wa utawala wao wa kati ya mwaka 1996 hadi 2001, ambapo waliokutwa na hatia ya uzinzi waliuawa kwa mawe, wezi walikatwa mikono, na wasichana walipigwa marufuku kwenda shule.

Soma zaidi: Biden: Tutawaondoa raia wote Afghanistan

Hata hivyo, ahadi hiyo ya Wataliban haijatuliza hofu ya raia wa Afghanistan, ambao kwa maelfu wananuia kuipa kisogo nchi yao baada ya kuangushwa kwa serikali iliyokuwepo.

Afisa wao aliyezungumza na Reuters amesema  wananuia kufanya majadiliano na magavana wa majimbo 20 kati ya 34 ya Afghanistan mnamo siku chache zijazo, wakitaka kuhakikisha usalama wao na kuwaomba ushirikiano.

Trump amshambulia Biden kwa ''aibu ya Afghanistan''

Wakati Rais Joe Biden wa Marekani akikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutokana na namna alivyoshughulikia mchakato wa kuondoka nchini Afghanistan, mtangulizi wake, Donald Trump ametia chumvi kwenye donda, akisema mwenendo wa Biden ni ''aibu kubwa zaidi katika historia ya sera za nje za Marekani''.

Rais wa Marekani, Joe Biden anakabiliwa na ukosoaji mkubwa sanaPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Trump pia amesema Biden amedhihirisha udhaifu mbaya sana kuliko kiongozi yeyote mwingine wa taifa. Hayo Trump ameyasema katika mkutano wa kisiasa alioufanya karibu na mji wa Cullman jimboni Alabama.

Ilikuwa wakati wa utawala wa Trump wakati Marekani ilipojadili na Taliban kuhusu mpango wa Marekani kuwaondoa wanajeshi wake kutoka Afghanistan ambao ulisababisha kuanguka kwa serikali iliyokuwepo mjini Kabul, lakini amekuwa akitumia ghasia katika utekelezaji wa mpango huo kama fimbo ya kumpigia mpinzani wake wa kisiasa, Rais Joe Biden.

''Tungeweza kuondoka Afghanistan kwa heshima, lakini tunachokishuhudia ni kinyume chake'', amesema Donald Trump anayedhaniwa kuwa na nia ya kugombea tena wadhifa wa urais alioupoteza kwa Biden katika uchaguzi uliopita.

 

afpe, rtre, ape

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW