1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan – Miaka 100 ya uhuru

19 Agosti 2019

Afghanistan inasherehekea miaka 100 ya uhuru wake. Agosti 1919, baada ya vita vya tatu vya Uingereza na Afghanistan na baada ya miaka 60 ya utawala wa Uingereza, nchi hiyo ilitambuliwa kama taifa huru.

Afghanistan Unabhängigkeitsfeierlichkeiten
Picha: picture-alliance/Photoshot/R. Alizadah

Lakini Wafghanistan wengi hawajihisi kusherehekea. Mmoja wa wasiosherehekea ni Mirwais Alani, bwanaharusi, ambaye harusi yake ililengwa na shambulizi la kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu mwishoni mwa wiki. Zaidi ya wageni 60 na wanafamilia waliuawa na zaidi ya 180 walijeruhiwa. Wakati wahanga wa kwanza wakizikwa jana mjini Kabul, Mirwais alizugumza na ripota kutokea ofisi za shirika la habari la reuters.

"Sina matumaini tena na nchi yangu. Nimempoteza kaka yangu, marafiki waliokuja kwenye harusi yangu. Sina hamu tena na sherehe za uhuru wa nchi yetu. Waache wapambe mji na wauangaze. Sherehe za uhuru ni kwa ajili ya matajiri tu. Kwenye harusi yangu walikuwepo wafanyakazi na watu wa kawaida tu."

Katika mji wa Lashkar Gah, mkoani Helmand, sherehe za uhuru zikiendelea.Picha: picture-alliance/Photoshot/A. A. Safdari

Kwenye siku hii ya Uhuru, mustakabali wa Afghanistan unajadiliwa pia. Marekani na kundi la Taliban wamekaribia kufikia muafaka. Matokeo ya mazungumzo ya amani ambayo yamekuwa yakifanyika mjini Doha kwa zaidi ya mwaka mmoja, yatatangazwa hivi karibuni.

Uondoaji kamili ua kwa sehemu wa vikosi vya Marekani unakaribia. Rais wa Marekani Donald Trump aliwaambia waandishi habari mjini New Jersey jana jioni, kuwa mazungumzo hayo yamefaana.


"Tumekuwa na mazungumzo mazuri na Wataliban pamoja na serikali ya Afghanistan. Hivi sasa tuna watu karibu 13,000 nchini Afghanistan na idadi hiyo tutaipunguza zaidi kidogo na kisha tutaamua iwapo tubakie huko au la.

Tumeweza kudhibiti hali na kikosi hiki kidogo na yumkini tukakipunguza zaidi na kisha tutaamua. Itategemea Watalibani na serikali ya Afghanistan. Lakini kuna hoja ya kujenga na hoja yenyewe ni kwamba tutaacha idadi kubwa ya maafisa wa intelijensia."

Hofu ya raia wa Afghanistan juu ya Wataliban

Haijulikani wazi ni vipi mustakabali wa Afghanistan utakuwa ikiwa Wataliban watashirikishwa kimadaraka. Wafghani wengi wanahofia kuwa mafanikio ya kidemokrasia na kiliberali yaliyofikiwa katika miaka ya karibuni huenda yakapotea, anasema Thomas Rutting kutoka mtandao wa wachambuzi wa Afghanistan.

Raia wakisherehekea uhuru kwa mitindo yao.Picha: picture-alliance/Photoshot/R. Alizadah


"Wataliban ndiyo wamesema machache zaidi kuhusu suala hili. Wanasema kwamba utawala wa Kiislamu uliokuwepo chini ya uongozi wao hadi mwaka 2001 utajengwa tena. Lakini wanasema pia kwamba hawataki kuhodhi madaraka.

Wameonyesha kuwa wako tayari kuitisha uchaguzi. Lakini mashaka ni iwapo kila mwanaume na mwanamke atakuwa na haki ya kupiga kura. Hilo ndiyo suala linaloibuliwa na makundi ya kiraia na wanawake. Wanahofia kwamba haki hii inaweza kupotea."

Iwapo uchaguzi wa rais utafanyika Septemba 28 kama ilivyopangwa ni jambo lisilo na uhakika. Tayari uchaguzi huo umeahirishwa mara mbili. Muda wa rais Ashraf Ghani kukaa madarakani ulikwisha muda mrefu. Taifa hilo ambalo limekuwa huru kwa miaka 100 linaongozwa na rais ambaye uhalali wake unatiliwa mashaka siyo tu na Wataliban pekee.


Chanzo: ARD

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW