Afghanistan yafurahishwa na uamuzi wa Trump
22 Agosti 2017
Akizungumza na wanajeshi kusini mwa Kandahar Rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani amesema hotuba rasmi ya kwanza ya Trump kama amiri jeshi mkuu, imeonyesha kwamba Marekani iko pamoja na wananchi wa Afghanistan bila kikomo.
''Natumai wote mmeisikia hotuba iliyotolewa na rais wa Marekani. Ujumbe wake ni kwamba, hakuna muda au masharti yatakayowekwa katika kuiunga mkono Afghanistan. Marekani itasimama na Afghanistan hadi mwisho,'' alisema Ghani.
Hayo yanajiri wakati ambapo wapiganaji wa Taliban wakiapa kuifanya nchi hiyo kuwa makaburi kwa wanajeshi wa Marekani. Ghani amewaambia wapiganaji wa Taliban kwamba hawatoshinda vita hivyo, huku akiwataka washiriki katika mazungumzo kwani nchi yake inataka amani na majirani zake wa Pakistan, nchi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikishutumiwa kwa kuchochea mashambulizi.
Trump: Pakistan inawafadhili magaidi
Katika hotuba yake aliyoitoa jana, Trump aliitaja Pakistan kuwa inatoa hifadhi kwa mashirika yanayosababisha machafuko, kauli iliyopokelewa kwa shangwe na India, adui mkubwa wa Pakistan, lakini imekosolewa na China, mshirika wa karibu wa Pakistan.
Wizara ya mambo ya nje ya India imepongeza juhudi za Trump za kuikabili Pakistan, huku China ambayo imewekeza kiasi cha Dola bilioni 50 nchini Pakistan, ikisema nchi hiyo inahitaji msaada wa jumuiya ya kimataifa baada ya kujitoa kwa dhati katika kupambana na wanamgambo wenye itikadi kali.
Kwa upande wake Pakistan leo imetoa wito wa kuwepo kwa amani kati yake na Afghanistan na imeahidi kufanya kazi na jumuiya ya kimataifa kuutokomeza ugaidi. Maneno hayo makini yamo katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya mambo ya nje ya Pakistan ikitaka kuwepo kwa amani na utulivu nchini Afghanistan.
Katika hotuba yake, Trump pia amefuta kauli zake za awali ambapo alikosoa kuwa vita vya Afghanistan vilivyodumu kwa karibu miaka 16 vilikuwa ni kupoteza muda pamoja na fedha. Hata hivyo, Trump hajaeleza idadi kamili ya wanajeshi watakaopelekwa Afghanistan, lakini maafisa waandamizi wa Ikulu ya Marekani wamesema tayari kiongozi huyo alimpa idhini waziri wake wa ulinzi kupeleka wanajeshi 3,900 zaidi nchini humo.
Hatua hiyo ya Rais Trump imeendelea kupongezwa na viongozi mbalimbali duniani, ambapo Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Ursula von der Leyen ameupongeza mpango huo wa Marekani kulibakiza jeshi lake nchini Afghanistan, akisema Ujerumani tayari imeongeza idadi ya wanajeshi wake inayowapeleka katika nchi hiyo inayokumbwa na vita.
Akizungumza leo katika kituo cha mafunzo ya kikosi cha jeshi la wanamaji kaskazini mwa Ujerumani, Von der Leyen amesema uamuzi wa Marekani umeonyesha njia nzuri na kwamba ni vizuri kuunganisha operesheni za kijeshi pamoja na msaada wa kimaendeleo na kidiplomasia nchini Afghanistan na kuizingatia kama dhana moja.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA
Mhariri: Caro Robi