Afghanistan yakubali wafungwa 400 wa Taliban kuachiwa
9 Agosti 2020Wito wa kuanza mara moja mazungumzo ya amani na usitishaji mapigano, ulisomwa katika lugha zote rasmi za Afghanistan yani Kipashto na Kifarsi. Hatua hiyo inaonekana kuisogeza karibu Marekani katika kuwaondoa wanajeshi wake na kumaliza shughuli zake za muda mrefu za kijeshi ndani ya taifa hilo.
Hadi sasa hakuna tarehe maalum iliyopangwa, lakini mazungumzo baina ya uongozi wa kisiasa wa Kabul na Taliban, yanatarajiwa kuanza mapema wiki ijayo na huenda yakafanyika nchini Qatar ambako kundi la Taliban lina ofisi zake.
Mazungumzo ya Afghanistan yamechochewa na mkataba wa amani uliosainiwa baina ya Marekani na kundi la Taliban mnamo mwezi Februari. Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani amesifu wajumbe wa mkutano wa Jumapili kwa uamuzi waliofikia na kuwataka Taliban kukomesha mapigano.
Msemaji wa kisiasa wa Taliban Suhail Shaheen, amesema uamuzi huo "ni hatua nzuri na chanya", akiongeza kuwa majadiliano huenda yakaanza ndani ya wiki moja ambayo wafungwa wao watakuwa wakiachiwa.
Aidha, kuhusu usitishaji mapigano Shaheen amesema kuwa, kundi la Taliban linaheshimu makubaliano iliyofikia na Marekani, na kulingana na makubaliano hayo "usitishaji mapigano ulikuwa miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa katika mazungumzo ya ndani ya Afghanistan".
Marekani ilitoa wito kwa baraza la kijadi linalojulikana kama "Loya Jirga" siku ya Ijumaa kuchukua uamuzi mgumu ili kutoa mwanya wa mazungumzo kuanza tena na kuhitimisha vita.
"Kuondoa viunzi, kuanza mazungumzo ya amani na kusimamisha umwagaji damu, Jirga inathibitisha kuwaachia wafungwa 400 wa Taliban", alisema Atefa Tayeb katibu wa baraza hilo, aliyesoma tangazo hilo.
Mkataba uliofikiwa baina ya Marekani na Taliban unataka serikali kuwaachia wafungwa 5000 na Talibani yenyewe kuwaachia maafisa 1000 wa serikali na kijeshi kama ishara ya uaminifu kuelekea kuanza kwa mazungumzo. Kabul iliwaachia wafungwa wengine na kubakiza 400 ambao kwa mujibu wa rais Ghani, anasema hakuwa na mamlaka ya kuwaachia kwasababu wana makosa makubwa na hivyo kuliomba baraza la Jirga kuamua.