1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Afisa wa UN asema wanawake wakimbizi Sudan wanahitaji ulinzi

14 Septemba 2024

Afisa wa Umoja wa Mataifa alierejea kutoka Sudan ameelezea namna wanawake na watoto wanaokimbia vita wanavyokosa mahitaji yao ya msingi.

Sudan | Durch den Vormarsch der RSF vertriebene Familien
Picha: Faiz Abubakr/REUTERS

Afisa wa Umoja wa Mataifa alierejea kutoka Sudan ameelezea namna wanawake na watoto wanaokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe walivyopokwa mahitaji yao ya msingi, wakipambania chakula, maji na usalama.

Afisa huyo Laila Baker, mkurugenzi wa shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa ameitaja hali nchini Sudan kuwa mbaya kabisaa kuwahi kushuhudiwa, akisimulia maelfu ya wanawake walivyolundikana kwenye mahema pasina maji safi, hakuna usalama, hakuna chakula cha kutosha na hakuna huduma ya afya.

Soma pia: Sudan yatuhumu Umoja wa Falme za kiarabu kuendeleza mzozo

Akizungumza kwa njia ya vidio kutokea Jordan, Baker amesema mzozo huo unateketeza Sudan, na kukosoa ufadhili mdogo wa juhudi za kiutu. Amesimulia pia kisa cha mwanamke mwenye miaka 20, kwa jina la Sana, ambaye alimuambia alibakwa na kundi la wanaume wakati akikimbia kutoka Khartoum, ambako alipoteza kila kitu.

Vita vya zaidi ya miezi 16 kati ya majenerali hasimu wa Sudan vimesababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa umekitaja kuwa mgogoro mbaya zaidi wa wakimbizi, ambapo watu zaidi ya milioni 10 wameathirika.