1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFRICOM yazungumzia ugaidi Afrika

19 Mei 2017

Uongozi wa jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM unaendeleza uwepo wake barani humo ili kushughulikia wasiwasi wa kiusalama. Lakini makundi ya kigaidi yanaendelea kutoa kitisho kwa mataifa mengi yalio na utawala dhaifu

General Thomas D. Waldhauser
Kamanda wa AFRICOM Jenerali Thomas WaldhauserPicha: Getty Images/J. Ernst

Kamanda wa AFRICOM Jenerali Thomas D. Waldhauser katika mahojiano na DW. Jenerali Waldhauser alikuwa mjini Brussels kukutana na wakuu wa majeshi ya mataifa ya Umoja wa Ulaya wiki hii, kujadilii hali ya sasa ya mambo katika mataifa kadhaa ya Kiafrika, na alizungumza na DW kuhusu jukumu la AFRICOM barani Afrika na hali ya sasa ya usalama.

Makundi kadhaa ya kigaidi yakiwemo linalojiita Dola la Kiislamu IS, Boko Haram na Al-Shabaab yanaendeleza uwepo mkubwa katika maeneo mengi, lakini pia yanazidi kukabiliwa na mbinyo wa kijeshi. Jenerali Waldhauser amesema moja ya mambo muhimu wanayofanya katika AFRICOM ili kufanikisha mapambano dhidi ya makundi hayo ni kujenga uwezo wa mataifa washirika ya Kiafrika, ambao utayasaidia kushughulikia tatizo hilo wenyewe, na kueleza kuwa katika mataifa kama Somalia wanatoa mafunzo na ushauri kwa jeshi ili liweze kukabiliana na vitisho hivyo wenyewe.

Ukubwa wa kitisho cha IS Afrika

Kuhusu ukubwa wa kitisho cha kundi linalojiita Dola la Kiislamu barani Afrika, Jenerali Waldhauser amesema kundi hilo lipo kwa viwango tofauti, akitolea mfano nchini Libya ambako IS iliudhibiti mji wa Sirte kwa muda wa miezi kadhaa iliyopita, kabla ya AFRICOM kuingilia kati na kuwafurusha kwenye maeneo mengi katikati mwa mwezi Januari. Amesema IS kwa sasa hawamiliki maeneo yoyote lakini wanaendelea kuwa kitisho.

Jenerali Waldhauser akimpokea waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattisi (mwenye suti nyeusi anaenyoosha kidole) na wageni wengne katika kambi ya Lemonnier mjini Ambouli, Djibouti.Picha: Getty Images/J. Ernst

"Pia tunaendelea kufuatilia maeneo mengine ya bara, iwe IS katika kanda ya Afrika Magharibi au katika kanda ya Ziwa Chad. Lakini jukumu letu ni kutoa mafunzo kwa mataifa ya eneo la Ziwa Chad ili yashughulikie yenyewe changamoto hiyo. Hivyo IS iko katika maeneo tofauti barani Afrika. Tunaendelea kuwafuatilia na wakati huo tukiendelea kuzingatia ukweli kwamba kitisho kikuu kiko nchini Iraq na Syria. Na pia tunachukuwa fursa hiyo kujenga uhusiano na washirika wetu ili washughulikie shabaha hizo," alisema Jenerali Waldhauser.

Kitisho cha uharamia Somalia

Akizungumzia juu ya uharamia nchini Somalia ambako hivi karibuni mwanajeshi wa kwanza wa Marekani aliuawa tangu 1993, Jenerali Waldhauser alisema siyo kwamba kumekuwa na ongezeko katika vitendo vya uharamia, lakini kumekuwepo na matukio kadha wa kadha katika mwezi uliopita ambayo wanapaswa kuyafuatilia kwa karibu. Amesema Umoja wa Ulaya unatoa mchango mkubwa katika suala hili kwa sababu wanazo hata meli katika kanda hiyo za kupambana na tatizo hilo, lakini akasisitiza ni mapema mno kusema iwapo kuna ongezeko kubwa katika uharamia.

Msako dhidi ya Kony na LRA

Kuhusu hatua ya Marekani kusitisha ushiriki wake katika operesheni ya kumsaka mbabe wa kivita wa kundi la Lord's Resistance Army LRA, Joseph Kony, na hatimaye Uganda pia kutangaza kuhimitisha operesheni hiyo, Jenerali Waldhauser amesema siyo jambo la kushangaza kwamba operesheni hiyo imesitishwa. Amesema ingawa hawakufanikiwa kumkamata Kony mwenyewe, wanajua anaendelea kujificha na kuongeza kuwa yumkini atakamatwa siku moja.

Hali nchini Libya

Na kuhusu Libya, mkuu huyo wa AFRICOM alisema nchi hiyo inaendelea kuwa changamoto lakini kuna maendeleo makubwa yaliofikiwa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika kipindi sawa na hiki mwaka uliopita, akiorodhesha kupungua kwa kiasi kikubwa, uwepo wa IS mjini Sirte, na mkutano wa hivi karibuni kati ya viongozi hasimu, Jenerali Khalifa Haftar na Fayez Serraj, akisema mkutano huo unatoa fursa ya kuutatua mgogoro wa Libya kwa njia ya kisiasa kuliko kijeshi.

Mahojiano: Teri Schultz

Ripoti: Iddi Ssessanga

Mhariri: Daniel Gakuba