Afrika, Asia wanyimwa Visa mkutano wa wakunga EU
13 Juni 2026
Mkutano mkubwa wa kimataifa wa wakunga unaotarajiwa kuanza Jumapili nchini Ureno umeingia dosari baada ya wataalamu kadhaa kutoka Afrika na Asia kunyimwa visa, jambo ambalo waandaaji wanasema linaweza kudhoofisha juhudi za kuokoa maisha ya mamilioni ya mama na watoto wachanga.
Kongamano hilo la International Confederation of Midwives, ICM, hufanyika kila baada ya miaka mitatu, linajikita katika kutafuta mbinu za kupunguza vifo 260,000 vya wajawazito na zaidi ya watoto milioni 4 wanaokufa kabla au ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa.
Zaidi ya wataalamu 20 kutoka Nigeria, Rwanda, Uganda, Ethiopia, Sierra Leone, DRC, Bangladesh na India wamezuiwa kuingia Ulaya.
Harriet Akello kutoka Uganda anasema alinyimwa viza licha ya kuomba mapema, na sasa hawezi kuwasilisha mada kuhusu miongozo ya kuokoa maisha katika mazingira magumu.
Wakati huo huo, wanaharakati wanajiandaa kufanya maandamano mjini Lisbon kuangazia uhaba mkubwa wa wakungaduniani, huku sauti muhimu kutoka nchi zinazoathirika zaidi zikikosekana.