1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika: Je, mradi mkubwa wa reli wa bara hilo umechelewa?

4 Oktoba 2022

Umoja wa Afrika unapanga kujenga mtandao mkubwa wa reli kuunganisha miji mikuu barani humo kufikia 2033. Lakini mradi huo mkubwa unahitaji ufadhili, jitihada kubwa na utashi wa kisiasa.

Kenia | Madaraka Express
Picha: Reuters/Stringer

Treni ya kwanza kabisa ya mwendo kasi barani Afrika inayoitwa "Al Boraq" inazunguka katika maeneo ya pwani ya Morocco, ikiwa na kasi ya kilometa 320 kwa saa.

Jina la treni hilo linatokana na simulizi za kidini na hasa yule farasi aliyekuwa na nguvu isiyo na kifani aliyempanda Mtume Mohammed kutoka Makka hadi Jerusalem.

Treni hiyo inatumia muda wa masaa mawili kati ya Tangier na Casablanca. Ilizunduliwa mwaka 2018 na kutimiza ndoto ya Morocco katika sekta ya usafiri.

Morocco iliingia ubia na Umoja wa Ulaya ili kupanua mtandao wake wa usafiri wa reli.Picha: Wilfrid Esteve//Hans Lucas/IMAGO

Ndoto hiyo imo katika kada ya Umoja wa Mataifa lakini katika uwanja mpana zaidi. Miaka tisa iliyopita umoja huo ulizindua mradi mkubwa: "Mtandao wa Reli ya Mwendo Kasi Barani Afrika."

Soma pia: Kenya yazindua reli nyingine mpya ya kisasa SGR

Lengo lilikuwa ni kujenga mtandao mpana wa reli kwa bara zima ifikapo mwaka 2033, kuunganisha miji mikuu muhimu na mikoa. Lakini kwa  zingatio la jitihada hiyo, miunganisho zaidi inaweza kuongezwa itakapofikia 2063.

Safari ndefu

Sehemu ya kwanza ya mpango huo inajumuisha maungano ya reli 19 ambayo itachukua urefu wa kilometa 16,970.

Younes Touitha kutoka wakala wa maendeleo wa Umoja wa Afrika-NEPAD ameliambia shirika la utangazaji la DW, kwamba asilimia 25 ya urefu wa reli katika mpango jumla wa mradi huo unapaswa kutekelezwa katika kipindi hiki.

Miunganisho mingine 62 inapaswa kufanyika ifikapo 2063, na hivyo kufikia jumla ya kilomita 74,000.

Reli za zamani kama reli ya Sena nchini Msumbiji zinahitaji ukarabati wa haraka.Picha: Getty Images/AFP/G. Guercia

Umoja wa Afrika uliteua maeneo matatu ya miunganisho kama miradi ya majaribio: Kutoka bandari ya Tanzania ya Dar es Salaam hadi mji mkuu wa Rwanda Kigali, Kampala nchini Uganda hadi Bujumbura nchini Burundi, na kitovu cha uchumi cha Afrika Kusini Johannesburg hadi Walvis Bay, nchini Namibia, kupitia mji mkuu wa Botswana Gaborone.

Miradi mingine kumi na moja itafanyiwa upembuzi yakinifu haraka iwezekanavyo, kwa mujibu wa mpango kazi wa umoja huo, ambao uliwasilishwa huko Kenya mwanzoni mwa 2022. Ingawa hadi sasa, mpango huo unasalia kwenye karatasi bila ya kuonekana utekelezaji wake.

Soma pia: Mkataba Mkubwa wa reli watiwa saini kati ya China na Tanzania

Hata hivyo ukweli halisi wa ujenzi wa reli mpya barani Afrika unahitaji kushinda vikwazo vingi. Toutha anasema vingi vya hivyo vinategemea kanda au nchi husika.

Lakini aliendelea kusema "Kama ifikapo 2030 tutakuwa tumefanikiwa asilimia 60 hadi 70 ya malengo yetu, jambo hilo litakuwa jema."

Reli zilizojengwa na fedha za China

Katika sehemu nyingi za Afrika, mitandao ya reli ilianza kujengwa nyakati za ukoloni. Katika nyakati hizo hazikujengwa kwa ajili ya abiria, bali kusafirisha malighafi kama vile mbao au dhahabu hadi bandarini na kuzisafirisha hadi Ulaya.

Uwekezaji katika reli unaweza kuimarisha biashara kati ya mataifa ya Afrika.Picha: Peter Morey/AP Photo/picture alliance

Wakati huu reli hizo  hutumikia kwa malengo mengine, kama kuwezesha biashara na usafirishaji wa abiria kati ya nchi za Kiafrika.

Lakini Younes Touitha ambae anatoka wakala wa maendeleo wa Umoja wa Afrika-NEPAD anasema upatikanaji wa fedha katika kuendeleza miradi hiyo imekuwa changamoto.

Soma pia:Kenya yazindua reli nyingine ya SGR kupunguza msongamano

Hadi wakati huu, miradi mingi mipya katika eneo la  Kusini mwa Jangwa la Sahara imefadhiliwa na China. Mfano mmoja ni ile wa treni mpya ya mwendo kasi inayounganisha bandari kuu ya Kenya ya Mombasa na mji mkuu, Nairobi.

Mikopo ya fedha ya China kwa Afrika inayaweka mataifa ya Afrika katika wakati mgumu. Baadhi ya wataalam wanahofia kwamba kuyalipa madeni hayo kutayaweka mataifa ya Afrika katika hali ngumz kwenye bajeti zake.

Chanzo: DW

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW