1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazerti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Babu Abdalla
16 Julai 2021

Yaliyoandikwa juu ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na makala juu ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na bomu lililokuwa linatokota nchini Afrika Kusini limelipuka!.

Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed
Picha: Mulugeta Ayene/AP Photo/picture alliance

Der Freitag

Gazeti la Der Freitag limeandika makala juu ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, linasema waziri mkuu huyo amekwama. Kutokana na sera zake, yaliyotokea kwenye jimbo la Tigray yamesababisha mgogoro wa kikanda. Sudan na Eritrea sasa pia zinahusika. Gazeti la Der Freitag linasema Abiy Ahmed aliyeingia madarakani mnamo mwaka 2018 na sifa ya kuwa mleta mageuzi amegeuka kuwa bwanavita!

Ethiopia: Kina mama wa jimbo la Tigray miongoni mwa raia waliogueka kuwa wakimbizi wa ndaniPicha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Gazeti hilo pia linakumbusha kwamba Abiy Ahmed alitunukiwa nishani ya amani ya Nobel. Gazeti la Der Freitag linatilia maanani kwamba mkataba wa amani ambao bwana Ahmed aliufikia na nchi jirani ya Eritrea ni muhimu. Bila ya mkataba huo gazeti linasema ingelikuwa vigumu kwa Ethiopia kuvutia misaada na vitega uchumi kutoka nje. Hata hivyo gazeti linasema waziri mkuu Abiy Ahmed amekwama kutokana na mgogoro wa jimbo la Tigray. Linaeleza kwamba Abiy hawezi kulitelekeza jimbo hilo lenye jeshi linaloweza kuutishia utawala wake. Linasema jimbo la Tigray halipo tayari kufikia mapatano ya amani na serikali kuu ya waziri mkuu Abiy Ahmed. Gazeti la Der Freitag linaeleza kwamba bwana Ahmed anakabiliwa na migogoro ya ndan,i na ya nje  kutoka Sudan, Eritrea na Misri.

die tageszeitung,

Gazeti la die tageszeitung linasema bomu lililokuwa linatokota nchini Afrika Kusini limelipuka. Maandamano yaliyofanywa na wafuasi wa rais wa zamani, Jacob Zuma yalikuwa ufunguo wa bomu hilo. Gazeti hilo linasema yanayotukia nchini Afrika Kusini yametifua mizizi ya matatizo ya kijamii na kuichumi yanayoikabili nchi hiyo.

Gazeti linasema tofauti kati ya waliopo juu na waliopo chini ni kubwa sana nchini humo. Gazeti la die   tageszeitung linaeleza kwamba tangu rais wa zamani Jacob Zuma ajisalimishe mbele ya idara ya sheria ili kutumikia kifungo cha miezi 15 jela kwa kosa la kudharau mahakama, wafuasi wake wamekuwa wanafanya maandamano ya ghasia. Watu kadhaa wameshauawa.

Jacob Zuma rais wa zamani wa Afrika KusiniPicha: Shiraaz Mohamed/AP Photo/picture alliance

Gazeti hilo linasema ni wazi kwamba tangu bwana Zuma alipokamatwa na tangu watu kuanza kuwatenga watu wake, chama tawala cha ANC pamoja na nchi nzima imeingia katika msukosuko. Linasema Zuma hana mamlaka yoyote serikalini au kwenye chama lakini bado anao ushawishi mkubwa nchini Afrika Kusini. die tageszeitung linaeleza kuwa kukamatwa kwake kulikuwa cheche iliyolipua baruti ya kijamii na kiuchumi kama jinsi raia wengi walivyonukuliwa wakisema.

Neue Zürcher

Neue Zürcher linasema Ufaransa imeamua kujiondoa kutoka ukanda wa Sahel baada ya kupoteza askari na washirika wake wengi. Gazeti la Neue Zürcher linatufahamisha hayo katika makala yake. Gazeti hilo linasema rais Emmanuel Macron mwezi uliopita alitangaza kuifunga operesheni ya kijeshi ambayo ilikuwa inaendeshwa kwa lengo la kuzisaidia nchi za Afrika magharibi katika harakati za kupambana na makundi ya magaidi.

Rais Macron aliwaambia viongozi wa nchi za ukanda wa Sahel kwamba Ufaransa itawapunguza wanajeshi wake waliowekwa kwenye nchi hizo za Sahel kuanzia mwishoni mwa mwaka huu. Wanajeshi hao wanashirikiana na wenzao kutoka Mali, Niger, Burkina Faso, Chad na Mauritania.

Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Blondet Eliot/ABACA/picture alliance

Neue Zürcher linatuarifu kwamba wanajeshi wa Ufaransa 5100 walioko kwenye nchi za Sahel wataondolewa hatua hatua. Gazeti hilo limemnukulu rais Emmanuel Macron akisema si wajibu wa Ufaransa kulitekeleza jukumu la wanajeshi wa nchi hizo za Afrika. Macron ameeleza kwamba katika siku za usoni, uhusika wa askari wa Ufaransa utakuwamo katika msingi wa ushirikiano na majeshi ya nchi za Sahel na kwamba Ufaransa haitaongoza operesheni ya "Barkhane" iliyoanzisha mnamo mwaka 2014 ili kupambana na makundi ya magaidi yanayoisumbua sehemu ya Sahel.

Gazeti la Neue Zürcher linatilia maanani kwamba rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amefanya uamuzi wa kuyaondoa majeshi ya nchi yake baada ya matukio hasi ya nchini Mali na Chad. Nchini Mali wanajeshi waliiangusha serikali kwa mara ya pili mbele ya macho ya wanajeshi wa Ufaransa na nchini Chad mshirika  mkubwa wa Ufaransa hayati Idriss Deby aliuliwa alipokuwa anawaongoza wanajeshi wake kwenye uwanja wa mapambano. 

Der Tagesspiegel

Gazeti la Der Tagesspiegel limechapisha makala inayotambua mchango wa Princess Marilyn Douala Manga Bell wa Cameroon. Mama huyo ambaye ni mtaalamu wa maswala ya kiuchumi na kijamii amechaguliwa mwaka huu kutunukiwa medali ya Goethe. Marilyn Manga Bell anatoa mchango wa kufafanua historia ya ukoloni wa wajerumani nchini Cameroon. Ameanzisha miradi mbalimbali mashuleni ili kuangazia historia ya Cameroon ya wakati wa ukoloni.

Princess Marilyn Douala Manga BellPicha: Goethe-Institut/R. Bisse Essomba

Der Tagesspiegel linatufahamisha kwamba mnamo mwaka  2016 Princess Manga Bell alikuwa miongoni mwa watu stadi kutoka Afrika waliotoa mapendekezo juu ya kuunda jukwaa la Humboldt ambalo ni nyumba ya kumbukumbu ya Sanaa na historia ya nje ya bara la Ulaya. Linasema miaka mitano baadae Manga Bell amechaguliwa kutunukiwa medali ya Goethe, amenukuliwa akisema kwamba mkabala wa jengo hilo la kumbukumbu lililopo mjini Berlin unakumbusha uhalifu uliotendwa na wakoloni wa kijerumani nchini Cemeroon ikiwa pamoja na kuuliwa kwa babu yake Rudolf Duala Manga mnamo mwaka 1914.

Gazeti hilo linafahamisha kwamba Duala Manga aliuliwa na wajerumani kwa sababu ya kuendesha kampeni ya kudai haki. Medali ya Goethe inatolewa na taasisi ya Goethe kila mwaka kutambua mchango unaotolewa na watu ambao si wajerumani katika kuendeleza lugha ya kijerumani na kuendeleza mahusiano ya tamaduni kimataifa.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen