1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani AfCFTA

Zainab Aziz Mhariri: Sekione Kitojo 
28 Juni 2019

Baadhi ya masuala na matukio ya barani Afrika yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na kuanzishwa kwa utaratibu wa biashara huru barani Afrika.

Ruanda Kigali Unterzeichnung Afrikanisches Freihandelsabkommen
Picha: picture-alliance/Xinhua/G. Dusabe

Frankfurter Allgemeine

Matarajio ni makubwa juu ya mradi huo lakini vizingiziti virefu vinachomoza. Ukweli ni kwamba nchi nyingi za Afrika zimekuwa zinazuia kufanya biashara na jirani zao. Nchi 52 kati ya 55 zimeuidhinisha mkataba wa kuanzishwa mradi huo lakini tatu bado hazijafanya hivyo. Nigeria,Benin na Eritrea. Eneo hilo la biashara huru lina watu bilioni 1.2 na lenye pato jumla la dola trilioni 2.5.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema mradi huo wa biashara huru ni muhimu sana kwa bara la Afrika kwa sababu hadi sasa jumla ya biashara inayofanyika kati ya nchi za Afrika ni asilimia 12 tu. Hata hivyo gazeti linatilia maanani kwamba jumuiya hiyo inaweza kutatizika kutokana na mikataba ya kibiashara  na kiuchumi iliyotiwa saini kati ya baadhi ya nchi za Afrika na Umoja wa Ulaya.

Süddeutsche

Gazeti la Süddeutsche linatupeleka nchini Ethiopia ambako wiki iliyopita lilifanyika jaribio la kuiangusha serikali ya jimbo la Amhara la kaskazini mwa Ethiopia. Gazeti hilo linatuarifu zaidi. kwamba katika muktadha wa jaribio hilo, Rais wa jimbo hilo la Amhara Ambachew Mekonnen aliuliwa na  mkuu wa majeshi ya Ethiopia jenerali Seare Mekonnen pia alipigwa risasi na kuuawa.

Matukio hayo yanatokana na mivutano ya miaka mingi kati ya makabila ya nchini Ethiopia. Kwa muda wa miaka mingi nchi hiyo ya watu wapatao milioni 100 ilikuwa chini ya udikteta wa watu waliotoka kabila la Tigray ambalo ni la watu wachache. Kwa muda wa miaka mingi watu wa makabila mengine na hasa waoromo na  waamhara walijaribu kupambana na udikteta huo uliomalizika baada ya kuchaguliwa kwa waziri mkuu  mpya Abiy Ahmed kutoka kabila la oromo ambaye ameleta mageuzi kadhaa nchini Ethiopia.

Gazeti hilo a Südeutsche linasema pamoja na mageuzi hayo ni kuachiwa huru kwa wafungwa wa kisiasa.Na miongoni mwao alikuwa jenerali Asamnev Tsige aliyeongoza jaribio la kuiangusha serikali ya jimbo la Amhara wiki iliyopita. Gazeti hilo la Südedeutsche linatilia maanani kwamba wakati wa udikteta waandamanaji walikandamizwa kikatili lakini sasa baada ya waziri mkuu Abiy Ahmed kuleta mazingira ya uhuru makundi kadhaa yamezuka yanayodai mamlaka makubwa zaidi na maeneo kwa ajili ya watu wa makabila yao. Kwa kuwa Ethiopia ni nchi inayojitawala katika mfumo wa shirikisho la majimbo kila kabila linawapendelea watu wake jambo ambalo husababisha migogoro nchini humo. Waziri mkuu Abiy Ahmed amesema atafanya mabadiliko ya katiba lakini bado hajatoa ufafanuzi.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung wiki hii linazungumzia juu ya mvutano unaoendelea baina ya Uganda na Rwanda. Gazeti hilo, limekariri tamko kutoka ofisi ya Rais wa Uganda kwamba nchi hiyo iko tayari kwa  vita. Gazeti hilo linaeleza kwamba katika tamko hilo, ofisi ya Rais wa Uganda imesema Rwanda imeweka mazingira ya kivita kwenye mpaka baina ya nchi mbili hizo jirani. Uganda imetoa tamko hilo kujibu aliyosema Rais wa Rwanda Paul Kagame alipokuwa anajibu maswali ya gazeti la die tageszetung. Kagame ameliambia gazeti hilo kwamba haoni iwapo vita baina ya nchi hizo vitazuka!

Hata hivyo Rwanda imeufunga mpaka wake na Uganda tangu miezi kadhaa iliyopita na imeishutumu Uganda kwa kuwasaidia waasi wanaoendesha harakati dhidi ya Rwanda kutokea Uganda. Gazeti la die tageszeitung linasema wakati Uganda inailumu Rwanda kwa kufanya uchokozi, Rais wa nchi hiyo Paul Kagame amesema nchi yake itadumisha busara. Kagame amekaririwa na gazeti la die tageszeitung akisema kwamba watu wanahofia vita kwa sababu wanayajua madhara yake. Gazeti hilo la die tagesezitung linasema licha ya Rais Kagame kuyarudia tena madai kwamba Uganda  imewatia ndani raia wa Rwanda, Kagame ameondoa kabisa uwezekano wa kuzuka vita baina ya nchi yake  na Uganda.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen - Magazeti ya Ujerumani

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW