1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii

Daniel Gakuba
19 Mei 2023

Juhudi za Afrika kuwa msuluhishi kati ya Urusi na Ukraine, kadhia ya Shakahola, na kitisho cha kugawika kwa Sudan kutokana na mzozo wa mapigano, ni miongoni mwa mada zilizomulikwa.

Zeitungsverkaufsstand mit regionaler und internationaler Presse in deutscher und türkischer Sprache
Picha: Hartmut Schmidt/imageBROKER/picture alliance

Natumai hujambo msikilizaji popote ulipo, na ninakukaribisha katika makala nyingine ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani. Ni makala inayokupa mukhtasari juu ya masuala ya barani Afrika yaliyoangaziwa na wahariri wa magazeti ya Kijerumani.

Afrika yataka kuwa msuluhishi kati ya Urusi na Ukraine

Tunaanza na gazeti la DieTageszeitung lililoripoti juu ya mpango wa Afrika kutuma ujumbe wa marais sita kuzitembelea Urusi na Ukraine katika juhudi za kusaka amani. Ujumbe huo wa kidiplomasia ulitangazwa kwa mara ya kwanza na rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ambaye alisema atakwenda Kiev na Moscow akiambatana na marais wa Senegal, Zambia, Congo-Brazzaville, Uganda na Misri.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ataongoza ujumbe wa Afrika kwenda Urusi na UkrainePicha: Justin Tallis/AFP/Getty Images

Gazeti hili limeandika kuwa rais wa Urusi Vladimir Putin na wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy wamekubali kuwapokea kwa mazungumzo viongozi hao wa kiafrika. Mwandishi wa ripoti hii anasema ingawa Ramaphosa hakutangaza tarehe ya ziara yao, inajulikana kuwa kuna mkutano wa kilele kati ya Urusi na Afrika utakaofanyika kuanzia Julai 26 hadi 29 mjini Sochi, ukiwa wa pili baada ya mwingine uliofanyika katika mji huo huo ulio kwenye mwambao wa Bahari Nyeusi mwaka 2019.

Suala jingine lililomulikwa na gazeti la Die Tageszeitung ni wasifu wa nchi ambazo marais wao watakuwa katika ujumbe huo wa Afrika utakaokwenda Urusi, anatoa mfano wa Uganda, ambako mwanaye Rais Yoweri Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amekuwa akinukuliwa kusema Uganda ingepeleka wanajeshi kuisaidia Urusi kuishinda Ukraine, na Afrika Kusini ambayo inakosolewa na nchi za magharibi kuwa na uswaiba na Urusi hasa unapohusika ushirikiano wa kijeshi.

Desemba mwaka jana, Afrika Kusini ilishiriki katika luteka za kijeshi za pamoja na China pamoja na Urusi ambayo ilikuwa tayari chini ya vikwazo vya magharibi. Hali kadhalika, Jumatatu wiki hii vyombo vya habari nchini Afrika Kusini vilifichua kuwa mkuu wa jeshi la nchi hiyo, Luteni Jenerali Lawrence Mbatha alikuwa amesafiri kwenda Moscow, katika mazungumzo juu ushirika wa kijeshi.

Katika mzozo wa Sudan, Darfur ni ukanda wa kifo

Na sasa tunazifunua kurasa za gazeti la Die Zeit, ambalo liliandika kuhusu kizungumkuti kinachowakabili raia wa Sudan, ambao hawajui iwapo wanapaswa kusalia nchini mwao au kukimbilia nje, wakati vita vya zaidi ya mwezi mzima vikiendelea kurindima kati ya jeshi rasmi la serikali, na kikosi maalumu cha wanamgambo cha RSF.

Mapigano nchini Sudan yamewalazimisha raia wengi kukimbiaPicha: AFP

Die Zeit  linasema licha ya makubaliano kati ya majenerali hasimu - ya kulinda maisha ya raia, mamia wanaripotiwa kuuawa katika mkoa wa Darfur katika ghasia zinazozidi kusambaa. Aliyeandika ripoti hii chini ya kichwa cha habari kisemacho, ''Maeneo ya kifo katika ukanda wa Darfur'', anaonya kwamba ingawa macho yote yanaelekezwa katika mji mkuu, Khartoum, yumkini mustakabali wa Sudan utategemea yanayojiri katika jimbo la magharibi la Darfur.

Akifafanua dhana yake, mwandishi huyo anasema kamanda wa wanamgambo wa RSF, Jenerali Mohammed Hamdan Daglo anayejulikana pia kama Hemeti, ana ngome zake katika jimbo la Darfur, na ikiwa vikosi vyake vitashindwa mjini Khartoum, huenda atakimbilia Darfur na hapo kimsingi Sudan itakuwa imegawika katika sehemu mbili. Hali hiyo ikitokea, yeyote atakayeshika hatamu za uongozi mjini Khartoum atakabiliwa na changamoto kubwa kutoka Darfur, kwa sababu uasi kutoka huko utakuwa kitisho kwa dikteta yeyote atakayeudhibiti mji mkuu ulio kwenye kingo za mto Nile.

Shakahola, kifo wa jina la Mungu

Matukio ya Shakahola, ambako watu zaidi ya 200 wamepoteza maisha kutokana na kufunga hadi kufa kwa maelekezo ya mchungaji Paul Mackenzie limeivutia kalamu ya mwandishi wa gazeti la Sueddeutsche Zeitung. Chini ya kichwa cha habari kisemacho, ''Kwa jina la Mungu'', mwandishi huyo anasema Wakenya bado hawajapona kabisa mshituko walioupata baada ya habari za mkasa huu kuanza kujulikana.

Kinachoendeleza mshituko wao, linaeleza gazeti hilo, ni kwamba wachunguzi wanazidi kugundua makaburi mpya walikozikwa wahanga, ambapo Jumamosi ya wiki iliyopita, makaburi 22 yaligunduliwa ka siku moja. Linasema Rais wa Kenya William RUTO amezishutumu mamlaka zinazohusika kushindwa kutimiza wajibu wao, na kuonya kuwa waliotenda makosa watawajibishwa.

Vifo vya mamia ya watu katika msitu wa Shakahola vinaendelea kugonga vichwa vya habariPicha: Stringer/REUTERS

Hapa gazeti hili limekumbusha kuwa Paul Mackenzie ambaye ni mchungaji wa kujiteuwa, alikwishakamatwa mara kadhaa kuanzia mwaka 2017. Linavinukuu vyombo vya habari vya Kenya kuwa mara zisizopungua mbili, polisi waliarifiwa kuwa wafuasi wa Mackenzie walijenga makaazi yenye majina ya kibiblia kama Galilea na Jeriko ndani ya msitu wa Shakahola, lakini polisi hao walifika ndani ya msitu huo na kuondoka bila kuchukua hatua yoyote.

Paul Mackenzie ambaye zamani alikuwa dereva wa teksi, linaarifu gazeti la Sueddeutsche Zeitung katika ripoti hii, alianzisha kanisa la Good News, likiwa moja ya maelfu ya makanisa mengine ya kipentekosti yanayochipua kama uyoga nchini Kenya, na mwanzoni halikuwa na umaarufu hadi lilipoanza kufuata itikadi kali mwaka 2019 na kuhamia msituni.

Dhana ya Mzungu mbaya, mweusi mwema, si sahihi kila mara

Tuhitimishe na gazeti la WeltPlus ambalo linasema, yahusikapo madhila yanayolisibu bara la Afrika, nadharia ya kuwa Wazungu ni wabaya, na Weusi ni wema, sio sahihi mara zote. Gazeti hili linachukua mfano wa vinyago kutoka ufalme wa kale wa Benin, ambavyo waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Analenna Baerbock alivirejesha nchini Nigeria wakati alipoizuru nchi hiyo.

Mwandishi wa gazeti hilo anasema sio tu kwamba vinyago hivyo, badala ya kuwekwa katika miliki ya umma, vimekuwa mali binafsi ya warithi wa ufalme wa Benin, bali pia, watu wa familia hiyo ya ufalme, wamekuja na kauli za kumdhihaki Baerbock, vikisema anaonekana kama kiongozi asiye na uzoefu. Mwandishi huyo anakumbusha kuwa Watawala wa Falme kama huo wa kale wa Benin walijitajirisha kwa kushirikiana na wafanyabiashara ya utumwa.

Chanzo: file:///C:/Users/GakubaD/Downloads/Presseschau%20Afrika%20deutsch%2012.05.-%2017.05.2023.pdf

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW