1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii

Angela Mdungu Mhariri:Bruce Amani
26 Januari 2024

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wameangazia ziara ya Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani barani Afrika, sakata la mpango wa Uingereza kupeleka wakimbizi Rwanda na uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Senegal .mwezi ujao

Ziara ya Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani barani Afrika
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Zeit online

Gazeti la mtandaoni la Zeit online limeandika kuhusu ziara ya Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Barani Afrika. Linaanza kwa kuandika kuwa, Waziri wa mambo ya nje Annalena Baerbock, anasafiri Kwenda Sudan ambako maelfu ya raia wanauwawa na wanalazimika kuyahama makazi yao. Kati ya nchi nyingine atakazozitembelea Baerbock kwenye ziara hiyo ni Pamoja na  Djibouti, Kenya Sudan Kusini.

Kabla ya ziara yake, Baeborck alieleza kwamba anataka kutafuta uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo ya kudhibiti vita Sudan. Tangu mwezi Aprili, kumekuwa na vita nchini humo  kati ya jeshi na wanamgambo wa kikosi cha RSF.

Abdel Fattah al-Burhan ni jina la kiongozi wa jeshi huku wanamgambo wa RSF wakiongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo anayejulikana pia kama Hemeti.

Zaidi Zeit Online linakwenda mbali na kuandika, anachokifahamu Baerbock ingawa hakisemi kwa sababu za kidiplomasia ni kuwa, waungaji mkono muhimu na washirika wa kundi la RSF hawako Kenya, Sudan Kusini au Djibouti, bali wako Abudhabi.

Linaongeza kuwa, bila ya Rais wa nchi za falme za kiarabu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, Dagalo asingeweza kuanzisha vita vyenye mafanikio na vilivyosababisha uharibifu mkubwa. Mkuu huyo wa kikosi kilichoasi cha RSF anatumia mfumo wa kibenki wa Falme za kiarabu, viwanja vyake vya ndege na bandari ili kusafirisha dhahabu kutoka kwenye migodi ya Sudan Kwenda kwenye soko la kimataifa.

Frankfurter Allgemeiner

Frankfurter Allgemeiner limeandika kuhusu Sakata la mpango tata wa Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda.

Baraza la juu la bunge la Uingereza limepiga kura kuunga mkono hoja itakayousitisha mkataba uliosainiwa na serikali ya Rwanda wa kuwapeleka wahamiaji wasio na vibali waliopo Uingereza  hivi sasa.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi SunakPicha: Justin Tallis/dpa/picture alliance

Gazeti hilo limeeleza kwamba, sababu za kufikiwa kwa hatua hiyo ni wasiwasi kuhusu hofu ya usalama wa wahamiaji wanaotakiwa kupelekwa katika taifa hilola Afrika ya mashariki.

Mkataba huo uliotengenezwa na serikali ya Uingereza ni mbadala wa makubaliano ya awali kati ya London na Kigali unaohusu pia wahamiaji wanaoingia Uingereza kupitia njia ya bahari ya Uingereza kupelekwa Rwanda. Mkataba huo tata unabainisha kuwa wahamiaji hao wasio na vibali watakaopelekwa Rwanda hawatoweza tena kuomba hifadhi kuingia Uingereza

Kabla ya baraza la juu la bunge kupiga kura iliyounga mkono kusitisha hoja ya Sunak, kamati ya baraza hilo ilitoa ripoti kuhusu maudhui ya mkataba huo. Ripoti hiyo iligundua kuwa katika maandishi, mkataba wa sasa umeboresha usalama na kulindwa kwa hadhi ya wahamiaji watakaopelekwa Rwanda lakini, kuna masuala kadhaa ya kisheria na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwanza kabla ya makubaliano ya mkataba huo kuanza kufanyiwa kazi.

die Tageszeitung

die Tageszeitung  mapema wiki hii lilitupia jicho uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Senegal mwezi ujao kwa kichwa cha Habari kinachosomeka, "Uchaguzi bila viongozi wa upinzani”.

Gazeti hilo limeandika, wanasiasa wawili maarufu wa upinzani wameachwa katika orodha ya wagombea katika uchaguzi wa Rais wa Senegal. Mashirika yasiyo ya kiserikali yanatahadharisha kwamba, nchi hiyo inazidi kuminya uhuru wa kisiasa. Uchaguzi huo unatazamiwa kufanyika Februari 25 bila wanasiasa maarufu wa upinzani Ousmane Sonko na Karim Wade.

Rais wa Senegal Macky Sall na Waziri Mkuu Amadou BaPicha: SEYLLOU/AFP/Getty Images

Hadi sasa mahakama ya katiba imeidhinisha jumla ya wagombea 20. Miongoni mwao ni Meya wa zamani wa mji mkuu Dakar, Khalifa Sall, na Waziri Mkuu Amadou Ba chaguo la Rais Macky Sall ambaye hatogombea tena baada ya awamu mbili madarakani.

Süddeutsche Zeitung

Süddeutsche Zeitung limeumulika mpango wa Waziri wa Mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy Feaser wa ushirika na Morocco katika suala la Uhamiaji unaotazamiwa kuyanufaisha mataifa hayo mawili.

Serikali ya Ujerumani inataka kufanya wepesi kwa wafanyakazi wanaokidhi vigezo kutoka Morocco kuingia katika soko la ajira la Ujerumani, na kuwarejesha makwao haraka kuliko awali waomba hifadhi wa Morocco ambao maombi yao yamekataliwa. Mwezi Oktoba Waziri wa mambo ya ndani alikwenda Rabat kwa mazungumzo ya awali kuhusu mpango huo.

Süddeutsche Zeitung linabainisha kwamba, muwakilishi wa Ujerumani wa masuala ya Uhamijai Joachim Stamp, alikuwa Morocco Jumanne alisema kuwa watashirikiana kupunguza uhamiaji usiofuata utaratibu kwa manufaa ya nchi hizo mbili.

Hata hivyo hakuna makubaliano yaliyofikiwa kwa maandishi kama yale Ujerumani iliyotia sahihi na taifa la Georgia, badala yake ushirikiano wa karibu katika uhamiaji ulikubaliwa kwa maneno pekee na kwamba hakukuwa kabisa na mpango wa mkataba wa kimaandishi.  

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW